carbohydates
JF-Expert Member
- Oct 13, 2026
- 260
- 607
TATHMINI YA MATUKIO YA OKTOBA 29. 2025 BAADA YA MWAKA MMOJA:
UKWELI, UWAJIBIKAJI NA HAKI
29 Oktoba 2026, Dar es Salaam
1.0 Utangulizi
Leo, tarehe 29 Oktoba 2026, tunawakumbuka waliopoteza maisha katika matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Tunasimama pamoja na manusura, majeruhi, familia za waliopotea na wote walioathirika kutafuta ukweli kuhusu yaliyowapata, kuhakikisha haki inatendeka na kuwawezesha kujenga upya maisha yao kunapaswa kuwa kipaumbele cha Serikali na taifa. Kurejea kwa shughuli za kawaida hakumaanishi kwamba maumivu yao yamekwisha au haki imepatikana.
Katika taarifa yetu ya pamoja ya tarehe 7 Novemba 2025, tulilaani ukiukwaji wa haki za binadamu na kuitaka Serikali kuruhusu uchunguzi huru, kuwawajibisha wahusika, kuziwezesha familia kuwatambua na kuwasitiri kwa heshima wapendwa wao, kutoa fidia na kulinda haki za binadamu. Mwaka mmoja baadaye, tunarejea madai hayo kutathmini hatua zilizochukuliwa na matokeo yake kwa waathirika na familia zao.
2.0 Tathmini ya hali ya sasa na hatua zilizochukuliwa
2.1 Madhara ya kibinadamu na hali ya familia zilizoathirika
Mwaka mmoja baada ya matukio ya Oktoba 29, familia zilizopoteza wapendwa wao bado zinahitaji ukweli kuhusu mazingira ya vifo, mahali miili ilipo na hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika. Ripoti ya Tume ya Jaji Chande iliripoti vifo vya watu 518. Pia ilieleza kuwa takribani watu 700 walikuwa hawajulikani walipo, na kwamba kulikuwa na miili takribani 39 ambayo ndugu waliripoti kuitambua katika vituo vya afya lakini baadaye hawakuweza kuipata. Takwimu hizi zinaonyesha uzito wa tatizo na umuhimu wa kuendelea na uchunguzi unaowezesha kila kila familia kupata majibu.
Katika thathmini yetu, Azaki hatujaona taarifa za kutosha kuonyesha kuwa Serikali imeweka na kutekeleza mpango wa kina wa kitaifa wa fidia, msaada wa matibabu, huduma za afya ya akili, msaada wa kisheria na msaada wa kijamii kwa familia zote zilizoathirika.Kwa hiyo, Azaki zinaitaka Serikali kuweka wazi hatua zilizochukuliwa, familia zilizonufaika, vigezo vya msaada na namna madai yaliyobaki yatakavyoshughulikiwa.
2.2 Uwajibikaji na hatua za kisheria kwa wahusika
Pamoja na Tume ya Jaji Chande kuripoti vifo 518 na kueleza ukubwa wa madhara, ripoti haikuwataja kwa uwazi watu au mamlaka waliohusika na vifo, walioamuru au kuruhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi, wala taasisi au viongozi walioshindwa kutekeleza wajibu wao. Pia haikutoa mwelekeo wa kutosha kuhusu namna ushahidi uliokusanywa unavyopaswa kupelekwa kwenye hatua za uchunguzi na mashtaka, ilikuhakikisha uwajibikaji wa kisheria unafanyika kwa haki na bila upendeleo. Hadi sasa, hakuna taarifa ya kutosha inayoonyesha kuwa hatua za jinai zimechukuliwa dhidi ya wahusika wa ukiukwaji huo.
Azaki hatukuridhishwa na uamuzi wa kuunda Tume nyingine inayojulikana kama Tume ya Jaji Lila baada ya Tume ya Jaji Chande kukamilisha kazi yake. Msimamo wa Azaki haukuwa wa kupinga uchunguzi wa kina au kutafuta ukweli, bali ulihusu umuhimu, uhalali na tija ya kuanzisha chombo kingine chenye majukumu yanayoweza kuingiliana kwa kiasi kikubwa na yale yaliyokuwa tayari yamefanyiwa uchunguzi. Kwa mtazamo wa Azaki, kuunda Tume nyingine kulihatarisha kurudia kazi, kutumia rasilimali i na na muda zaidi na kuchelewesha hatua za moja kwa moja za uwajibikaji wa kisheria.
Hoja ya msingi ni kwa nini masuala yaliyoibuliwa na Tume ya Jaji Chande hayakushughulikiwa kwa kupeleka ushahidi na mapendekezo yaliyopo kwa vyombo vyenye mamlaka ya kisheria, na kuhakikisha uchunguzi zaidi unafanyika pale inapohitajika, badala ya kuanzisha Tume nyingine yenye wigo unaofanana kwa kiasi kikubwa.
2.3 Ukweli kuhusu idadi ya vifo, majeruhi na waliopotea
Azaki zinatambua kuwa idadi ya vifo 518 iliripotiwa na na Tume ya Jaji Chande. Hata hivyo, uchambuzi wa Azaki kuhusu Tume ulibainisha kuwa Tume ilitegemea kwa kiasi kikubwa vyanzo rasmi kama polisi na vituo vya afya, wakati baadhi ya taasisi hizo zilitajwa katika malalamiko kuhusu matumizi ya nguvu, kuondoa majeruhi au miili na kuzuia taarifa. Tume yenyewe ilikiri kuwa baadhi ya vifo na majeruhi huenda havikuripotiwa. Kwa hiyo, Azaki zinaona kuwa idadi hiyo haiwezi kuchukuliwa kuwa hesabu ya mwisho bila uthibitishaji huru na wa kina.
Uthibitishaji unapaswa kuhusisha kumbukumbu za hospitali na vituo vya afya, taarifa za familia, kumbukumbu za mazishi, mashahidi, ushahidi wa kitabibu na nyenzo za kidijitali zinazoweza kuthibitishwa. Taarifa za waliopotea na miili isiyopatikana zinapaswa kuchunguzwa kando na kwa uharaka, huku usalama, faragha na utu wa familia vikilindwa. Tofauti za takwimu zinazotolewa na vyanzo mbalimbali zinapaswa kutatuliwa kwa mbinu wazi na za kisayansi badala ya kuchukuliwa kama sababu ya kupuuza madai.
3.0 Kuendelea Kuminywa kwa Haki za Kiraia na Kidemokrasia
Azaki tuna wasiwasi kuhusu ukiukwaji na uminywaji wa nafasi ya kiraia unaoendelea hata baada ya matukio ya Oktoba 29 2025. Tumeendelea kushuhudia matukio ya matumizi ya nguvu kupita kiasi hasa kwa vyombo vya dola, ukamataji usiozingatia sheria, utekaji na kupotea kwa watu pamoja na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari. Azaki tulisikitishwa na matukio ya kuelekea maadhimisho ya Saba Saba ya Julai 2026 hasa tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi la tarehe 26 Juni 2026 la kusitisha vibali vya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kukamatwa kwa watu wasiopungua 130 na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.
Hali hii inaonyesha umuhimu wa kuhakikisha kuwa wananchi wanaweza kutoa maoni ya kisiasa, kukusanyika kwa amani, kupata habari na kuwawajibisha viongozi bila hofu ya kukamatwa kiholela, vitisho au matumizi yasiyo halali ya nguvu. Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa mazuio yoyote yanayohusiana na haki za binadamu yanatokana na msingi wa sheria na yanazingatia uwiano na malengo halali.
4.0 Msimamo na mapendekezo ya Azaki
Kwa takribani mwaka mmoja sasa Azaki tunaona hakuna mabadiliko makubwa yanayoonekana katika masuala ya msingi ya ukweli na uwajibikaji. Bado hakuna uwazi wa kutosha kuhusu hatua zilizochukuliwa kufuatilia ushahidi, kubaini na kuwawajibisha waliohusika na vifo au ukiukwaji mwingine, au kutoa majibu kwa familia kuhusu waliopotea na miili isiyopatikana. Kuundwa kwa Tume nyingine hakujatoa badiliko la wazi na linalopimika katika uwajibikaji wa kisheria. Umma unahitaji kuona hatua mahsusi zinazotokana na ushahidi, si kuongezeka kwa michakato bila matokeo yanayoeleweka.
Kwa kuzingatia ukubwa wa madhara yaliyojitokeza na hali ya uwajibikaji Azaki tunatoa mapendekezo yafuatayo:
1. Fidia kwa manusura na familia zilizoathirika: Serikali ianzishe Mfuko Maalum wa Fidia kwa manusura hasa walioachwa na ulemavu wa kuduma na kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Mfuko utoe fidia stahiki, huduma za matibabu, vifaa saidizi, msaada wa kisaikolojia na kijamii, msaada wa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisheria. Vigezo vya kupata fidia viwe wazi, mchakato wa madai uwe rahisi na matumizi ya fedha yakaguliwe kwa uhuru.
2. Ukweli, uwajibikaji na uchunguzi huru: Ripoti ya Tume ya Jaji Chande na ushahidi uliokusanywa viwasilishwe kwa mamlaka husika za kikatiba na kisheria kwa hatua zinazostahili. Wote watakaobainika kuwajibika kwa mauaji au matumizi ya nguvu kupita kiasi wawajibishwe kwa mujibu wa sheria na bila upendeleo.
3. Tume huru ya Kutafuta Ukweli, Uwajibikaji na Maridhiano ya Kitaifa: Azaki zinatoa wito wa mchakato huru na jumuishi wa kutafuta ukweli, kuweka wazi yaliyotokea na kuimarisha maridhiano ya kitaifa. Mchakato huu uongozwe na watu wenye uadilifu na uaminifu kwa pande zote, uwashirikishe waathirika, familia, vyama vya siasa, Azaki, taasisi za dini, vijana na makundi mengine ya kijamii. Maridhiano yasiwe mbadala wa uwajibikaji wa jinai pale ushahidi unapoonyesha kuwa makosa yalitendeka.
4. Siku ya kitaifa ya kumbukumbu na maombolezo: Tarehe 29 Oktoba ya kila mwaka itangazwe kuwa siku ya kumbukumbu na maombolezo ya kitaifa kwa wahanga wa matukio ya 2025, kwa heshima ya waliopoteza maisha na familia zilizoathirika.
5. Kuwatafuta waliopotea na kutoa majibu kwa familia: Uanzishwe utaratibu maalum, huru na unaowajibika wa kuchunguza madai ya utekaji na kupotea kwa watu, kubaini walipo na kufafanua mazingira ya kupotea kwao.
6. Mageuzi ya Katiba na mfumo wa uchaguzi: Serikali ishughulikie sababu za msingi zilizotambuliwa na Tume ya Jaji Chande, ikiwemo madai ya Katiba mpya na uchaguzi huru, wa haki, wazi na unaoaminika. Mchakato wa mageuzi uwe jumuishi, uwe na ratiba ya wazi na utekelezwe kwa ushiriki wa wananchi na wadau wote. Azaki zinatilia mkazo umuhimu wa kufikia muafaka wa kitaifa na kushughulikia uwajibikaji wa matukio ya 2025 sambamba na maandalizi ya mageuzi ya muda mrefu.
7. Kulinda uhuru wa kiraia na utawala wa sheria: Serikali ihakikishe haki za kujieleza, kukusanyika kwa amani, kupata habari na kushiriki katika mifumo ya kidemokrasia zinalindwa. Vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu wafanye kazi bila vitisho. Ukamataji, vizuizi vya mikutano na hatua za kiusalama zifuate sheria, taratibu za haki na viwango vya haki za binadamu.
8. Mazungumzo ya kitaifa na ushirikiano wa kimataifa: Serikali ianzishe mazungumzo ya dhati na jumuishi na vyama vya siasa, Azaki, taasisi za dini, waathirika na makundi mengine muhimu ili kujenga upya imani na mshikamano. Jumuiya ya kimataifa iendelee kuunga mkono juhudi za ukweli, haki, uponyaji na mageuzi kwa nam namna inayoheshimu sauti na umiliki wa Watanzania.
9. Hatua za haraka na uwazi wa utekelezaji: Serikali iweke wazi mpango wa utekelezaji wa uwajibikaji unaotaja taasisi zinazowajibika, hatua zinazopaswa kuchukuliwa, muda wa utekelezaji na namna umma utakavyopata taarifa za maendeleo. Taarifa za utekelezaji zitolewe mara kwa mara na zijumuishe maendeleo ya uchunguzi na hatua za uwajibikaji; idadi ya madai ya waliopotea yaliyofanyiwa kazi na majibu yaliyotolewa kwa familia; idadi ya familia na majeruhi waliopata msaada au fidia; na hatua zilizochukuliwa kulinda uhuru wa kujieleza na kukusanyika.
10. Haki za kidijitali: Serikali iweke wazi msingi wa kisheria na mamlaka iliyoamuru kuzimwa kwa intaneti mwezi Oktoba 2025, na itoe ahadi ya wazi ya maandishi kuwa haitazima tena intaneti wala kuzuia mitandao kwa ujumla, kwa kuzingatia wito wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (Azimio Na. 640 la mwaka 2025) wa kuhakikisha intaneti inapatikana bila vikwazo wakati wa uchaguzi. Pia, Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta na kanuni zake zirekebishwe ili kizuizi chochote cha mawasiliano kiwe na msingi wa sheria, kiwe cha lazima na chenye uwiano, kiwe na muda maalum, kitangazwe hadharani pamoja na sababu zake, na kiweze kupingwa mahakamani.
5.0 Hitimisho
Mwaka mmoja baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, Tanzania bado inakabiliwa na wajibu wa kimaadili na kisheria wa kutoa majibu kwa familia, kubaini ukweli kamili, kuwawajibisha waliohusika na kurejesha imani ya umma.
Azaki tunasisitiza kuwa haki na maridhiano vinapaswa kwenda pamoja. Maridhiano ya kweli yanahitaji ukweli kuwekwa wazi, waathirika kuheshimiwa na kusaidiwa, wahusika kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria, na mageuzi ya kimuundo kufanyika ili kulinda haki za binadamu na kuzuia matukio kama haya kujirudia. Oktoba 29 isiwe kumbukumbu ya maumivu pekee, bali iwe chachu ya kujenga Tanzania yenye haki, uwajibikaji, usawa na utawala wa sheria.
Imesainiwa na:
1. Legal and Human Rights Centre
2. Twaweza
3. Foundation For Civil Society
4. JamiiAfrica
5. Msichana Initiative
6. Tanganvika Law Society
7. Internet Governance Tanzania Working Group
=====
Soma Pia: Tume ya Jaji Lila kuanza uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29
Nakala imeambatishwa hapa chini👇