Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Oktoba 2018
- Idadi ya watu wenye ugonjwa wa kisukari imeongezeka kutoka milioni 108 mnamo 1980 hadi milioni 422 mwaka 2014.
- Ugonjwa wa kisukari * miongoni mwa watu wazima zaidi ya miaka 18 kumepanda kutoka asilimia 4.7 mnamo 1980 hadi 8.5% mwaka 2014 (1).
- Ugonjwa wa sukari umekuwa ukikua kwa kasi zaidi katika nchi zenye kipato cha kati na cha chini.
- Ugonjwa wa kisukari ni sababu kubwa ya upofu, kuharibika kwa figo, mshtuko wa moyo, kiharusi na kukatwa miguu.
- Mnamo mwaka wa 2016, wastani wa vifo milioni 1.6 vilisababishwa moja kwa moja na ugonjwa wa sukari. Vifo vingine milioni 2.2 vilitokana na sukari kubwa ya damu mnamo 2012 **.
- Karibu nusu ya vifo vyote vinavyotokana na sukari kubwa ya damu kutokea kabla ya umri wa miaka 70. WHO ilikuwa sababu ya saba ya kusababisha vifo mnamo 2016.
- Lishe yenye afya, mazoezi ya kawaida ya kiwmili, kudumisha uzito wa kawaida wa mwili na epuka tumbaku ni njia za kuzuia au kuchelewesha mwanzo wa ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2.
- Ugonjwa wa kisukari unaweza kutibiwa na madhara yake kuzuiliwa au kucheleweshwa kwa lishe, shughuli za mwili, dawa na uchunguzi wa mara kwa mara na matibabu.
UFAHAMU UGONJWA WA KISUKARI NA TIBA YAKE
Ugonjwa wa kisukari (Diabetes Mellitus) hutokea pale tezi kongosho (pancrease) inaposhindwa kutengeneza homoni au kichocheo aina ya Insulin, au pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri kichocheo hicho cha insulin na kusababisha kuongezeka kiwango cha sukari kwenye damu (hyperglycemia).
Insulin ni kichocheo au homoni inayotengenezwa na kongosho ili kudhibiti kiwango cha sukari.
Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababishwa kuwa na kiwango kidogo cha Insulin mwilini, mwili kutosikia kichocheo hicho au yote mawili. Ili kuelewa vyema ugonjwa wa kisukari ni muhimu kwanza kuelewa namna chakula kinavyovunjwa vunjwa na kutumiwa na mwili ili kuzalisha nguvu.
Wakati chakula kinapoyeyushwa matukio kadhaa hutokea.
1.Tukio la kwanza ni sukari inayoitwa glucose ambayo ni chanzo cha nguvu mwilini huingia katika damu.
2.Tukio la pili ni kiungo kinachoitwa kongosho (pancrease) kutengeneza kichocheo cha Insulin. Kazi ya Insulin ni kuondoa glucosei katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumiwa kama nishati.
Watu wenye ugonjwa wa kisukari huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kwa sababu miili yao haiwezi kupeleka sukari kwenye seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha nguvu.
Hii ni kutokana sababu zifuatazo.
1.Kongosho kutokuwa na uwezo wa kutengeneza insulin ya kutosha, au--->
2.Seli za mwili haziathiriwi na insulin kama inavyotakiwa ama sababu zote hizo mbili.
AINA ZA KISUKARI
KISUKARI AINA YA KWANZA(TYPE 1 DIABETES MELLITUS)
Hii ni aina ya kisukari inayowaathiri zaidi watoto na vijana. Aina hii hutokea iwapo seli maalumu zinazotengeneza homoni ya insulin zinapokosekana katika tezi kongosho au zinapoharibika kutokana na sababu yeyote ile, na hivyo kusababisha ukosefu kabisa au upungufu wa kichocheo hicho kwenye damu.
Mambo yanayoweza kusababisha uharibifu wa seli hizi katika tezi kongosho ni pamoja na kushambuliwa tezi kongosho kunakoweza kufanywa na magonjwa ya kinga ya mwili ya mtu mwenyewe au autoimmune diseases, au kushambuliwa na vyanzo visivyojulikana.
KISUKARI AINA YA PILI (TYPE 2 DIABETES MELLITUS)
Hii ni aina ya kisukari inayotokea zaidi ukubwani. Aina hii ya kisukari husababishwa na kupungua utendaji kazi wa homoni ya insulin, au seli kushindwa kutumia insulin ipasavyo.
Hali hii mara nyingi husababishwa na unene uliopitiliza yaani obesity, au hali ya kutoushughulisha mwili kabisa (physical inactivity).
Kwa vile, katika aina hii ya kisukari, insulin huzalishwa kwa kiwango cha kutosha isipokuwa tatizo lipo kwenye ufanisi na utendaji kazi wake,
KISUKARI CHA UJAUZITO (GESTATIONAL DIABETES MELLITUS)
Ni aina ya kisukari kinachotokea pindi kunapokuwa na ongezeko la kiwango cha sukari katika damu (hyperglycemia) wakati wa ujauzito. Aina hii ya kisukari huathiri karibu asilimia 2 hadi 5 ya mama wajawazito wote ingawa wengi wao hupata nafuu na kupona kabisa mara tu baada ya kujifungua.
Hata hivyo karibu asilimia 20 mpaka 50 ya mama wajawazito wanaopata aina hii ya kisukari huweza kuendelea kuwa na ugonjwa huo hata baada ya ujauzito na hatimaye kuwa na aina ya pili ya kisukari.
SABABU ZA KISUKARI
Sababu za kisukari hutofautiana kulingana na aina ya ugonjwa huo.
Aina ya kwanza ya kisukari ina uhusiano mkubwa sana na kurithi. Aidha aina hii pia husababishwa na maambukizi virusi kama vile Coxsackie virus type B4.
Visababishi vingine ni pamoja na sumu inayotokana na kemikali za
baadhi ya vyakula (food borne chemical toxins), na kwa baadhi ya watoto wachanga maziwa ya ng'ombe yanaweza kuchochea kinga ya mwili wa mtoto uushambulie mwili wenyewe na hivyo kusababisha uharibifu katika tezi kongosho.
Aina ya pili ya kisukari kwa ujumla husababishwa zaidi na jinsi mtu anavyoishi na pia matatizo ya kijeneteki. Aidha kuongezeka uzito na unene kupita kiasi (obesity).
Sababu nyingine ni pamoja na kuongezeka umri, maisha ya kivivu na kutofanya mazoezi na pia ugonjwa wa tezi kongosho (pancreatitis) ambao hufanya insulin inayozalishwa kuwa na ufanisi mbovu au ya kiwango cha chini.
DALILI ZA UGONJWA WA KISUKARI
Kukojoa mara kwa mara
Kuhisi kiu kali na kunywa maji kwa kiwango cha kupitiliza (polydipsia).
Kuhisi njaa na kula mara kwa mara (polyphagia).
Kuchoka haraka
Kupungua uzito
Vipele mwilini (diabetic dermadromes).
Kutoa harufu ya acetone inayofanana na harufu ya pombe.
Kuhisi maumivu ya tumbo na kupoteza fahamu
Na wagonjwa wa kisukari pia huwa katika hatari ya kupata maambukizi katika kibofu cha mkojo, ngozi na kwa wanawake sehemu za siri.
Baada ya mtu kuwa na dalili za ugonjwa wa kisukari matibabu huanza baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitisha kwamba kweli ana ugonjwa huo.
Chini ya 5.6 mmol/l au 100 mg/dl: Sukari kwenye damu yako ni sawa.
Zaidi ya 5.6 mmol/l au 100 mg/dl lakini chini ya 6.9 mmol/l au 125 mg/dl: Hii ni ishara ya tahadhari-unapaswa kufanya mabadiliko katika maisha yako sasa ili kupunguza hatari ya kupata kisukari. Kama matokeo yamekaribia kiwango cha juu, ni muhimu hasa kufanya juhudi za ziada za ulaji wenye afya, na kupata mazoezi au kujishughulisha.
Zaidi ya 6.9 mmol/l au 125 mg/dl: Una kisukari na unahitaji matibabu. Kadri kiwango kinavyopanda, ndivyo kuongezeka kwa hatari ya dharura kutokana na kiwango cha sukari kwenye damu kuzidi kupita kiasi, au matatizo makubwa ya kiafya
Madhara ya Kisukari
Kisukari huweza kusababisha madhara yafuatayo kwa muhusika iwapo hakitatibiwa inavyopaswa.
- Kuziba kwa mishipa mikubwa ya damu kutokana na kuzungukwa na mafuta (Atherosclerosis)
- Mgonjwa kushindwa kuona vizuri au kushindwa kuona kabisa na kuwa kipofu (diabetic retinopathy)
- Kushindwa kufanya kazi vizuri kwa figo
- Mgonjwa kuhisi ganzi na kupoteza kuhisi mikononi na miguu kwa sababu ya kuharibika kwa neva (diabetic neuropathy)
- Kupungua kwa nguvu za kiume.
- Vidonda (diabetic ulcers) hususani vidoleni. Hali hii wakati mwingine hupelekea mgonjwa kukatwa viungo vyake.
- Mgonjwa kuwa hatarini kupata maambukizi ya vimelea mbalimbali hasa bakteria kutokana na kuharibiwa na kushindwa kufanyakazi vizuri kwa chembe nyeupe za damu (White Blood Cells)
Matibabu
Matibabu ya kisukari hutegemea na aina ya kisukari ingawa kwa ujumla kuna hujumuisha matumizi ya dawa na njia ya kubadilisha mfumo (staili) wa maisha.
Kwa aina ya pili ya kisukari (type 2 DM au NIDDM): Aina hii ya kisukari huweza kutibiwa kwa ama dawa au kubadili mfumo wa maisha au vyote viwili kwa pamoja. Katika kubadili mfumo wa maisha, ni muhimu mgonjwa kutilia maanani na kuwa makini na vitu kama aina ya vyakula anavyokula, na kujitahidi na kuongeza kufanya mazoezi ya mwili ili kuepuka kuongezeka uzito kupita kiasi. Kuhusu aina ya vyakula inashauriwa sana
- kupunguza kula vyakula vyenye lijamu (cholesterol) ambayo ni mafuta mabaya yaani kula walau chini ya miligramu 300 za lijamu kwa siku.
- kujitahidi sana kula vyakula vya kujenga mwili (protein) angalau kwa asilimia 10-15. Vyakula hivi ni pamoja na nyama na mboga za majani.
- kuwa makini na ulaji wa vyakula vya wanga (carbohydrate). Hakikisha visizidi asilimia 50-60 ya chakula unachokula kwa siku. Yaani visiwe ndiyo chakula kikuu kwa siku.
- kupunguza utumiaji wa chumvi katika chakula.
- Kuacha na kuwa muangalifu kutumia pombe.
Suala la ufanyaji mazoezi ni jambo la muhimu kwa vile mazoezi husaidia sana kupunguza uzito, kuondoa mafuta mwilini yanayopunguza utendaji kazi wa insulin na hivyo kuongeza ufanisi na utendaji wa insulin mwilini.
Hali kadhalika, mgonjwa mwenye aina hii ya kisukari anaweza pia kupewa dawa ambazo atatakiwa kunywa kila siku huku akiendelea kufuata ushauri mwingine kama ilivyoelezwa hapo juu.
Dawa hizo ambazo huitwa pia dawa za kushusha kiwango cha sukari mwilini (Oral Hypoglycemic drugs) ni pamoja na zile za kundi la Biguanides kama vile Metformin, za kundi la Sulphonylureas kwa mfano Glipizide, za kundi la Meglitinides, za kundi la Alpha glucosidase inhibitor, zinazojulikana kama Thiazolidinediones, Incretin-mimetic au za kundi la Dipeptidyl peptidase IV inhibitors kwa mfano sitagliptin
Ifahamike pia kuwa wapo baadhi ya wagonjwa wa aina hii ya pili ya kisukari (Type 2 DM) ambao pamoja na kutumia dawa za kunywa za kushusha sukari na kufuata ushauri wa daktari kuhusu mfumo wao wa maisha bado njia hizo zinaweza zisishushe sukari inavyotakiwa. Katika hali kama hiyo, wagonjwa hawa huweza kudungwa pia sindano za insulin kwa muda ili kushusha kiwango cha sukari.
Matibabu maalum
- Matibabu ya hyperosmolar non-ketotic coma (HONKC): Matibabu haya hutolewa hospitali. Mkazo huwekwa katika kusahihisha upungufu wa maji mwilini ambapo mgonjwa hupewa kati ya lita 8 hadi 10 za maji aina ya Normal saline. Aidha, lita kati ya 1 hadi 2 hutolewa katika masaa ya mwanzo tangu mgonjwa kufkia hospitali. Iwapo kuna ugumu katika kusahihisha kiwango cha kisukari mwilini kwa kutumia dawa za kunywa, Insulin inaweza kutolewa.
- Matibabu ya Diabetic ketoacidosis (DKA): Kama ilivyo kwa hyperosmolar non-ketotic coma, matibabu ya DKA nayo hutolewa hospitali chini ya uangalizi maalum wa madaktari. Hii ni hali ya hatari, ambapo kama isipotibiwa kwa umakini, inaweza kupelkea kifo cha mgonjwa. Jambo la muhimu katika matibau ni kusahihisha upungufu wa maji mwilini kwa kutumia Normal saline, ambapo lita 1-3 hutolewa ndani ya masaa mawili ya mwanzo, kusahihisha kiwango cha potassium kilichopo katika damu na kurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu kwa kutumia Insulin.