Kumekuwepo kilio na maswali mengi ya wadau mbalimbali wakitaka kujua masuala kadhaa kuhusu ugonjwa wa kisukari; tumetengeneza mnakasha huu ili kurahisisha majibu (si yote) kwa wenye uhitaji wa maswali yao.
Zingatia: Ni vema kwenda hospitali kwa tiba ya uhakika, hapa utapata majibu yanayokupa mwanga wa nini cha kufanya.
Case studies, mapendekezo ya tiba, waliopata kutibiwa, madaktari wanaopendekezwa na wadau kwa tiba n.k ndivyo vitawekwa kwenye bandiko la kwanza
===
UFAFANUZI WA KINA KUHUSU UGONJWA HUU
Kisukari ni nini? Kisukari ni ugonjwa unaosababisha glukosi kuzidi kwenye damu (damusuziada) kwa sababu ya ukosefu wa insulini au kongosho kutoa insulini isiyotosheleza mahitaji ya mwili.
Kuna aina ngapi za ugonjwa wa kisukari?
Kuna aina tatu za ugonjwa wa kisukari:
Aina ya kwanza ya kisukari:
Ugonjwa wa kisukari unaosababishwa na kongosho kushindwa kutoa insulini kabisa. Katika ugonjwa kisukari wa aina hii mgonjwa lazima achome sindano ya insulini kila siku kwa sababu kongosho haitoi insulini kabisa.
Aina ya pili ya kisukari:
Ugonjwa wa kisukari unaosababishwa na kongosho kutoa insulini isiyotosheleza mahitaji ya mwili. Aina hii ya kisukari inaweza kutibiwa kwa kutumia vidonge au kwa kupunguza tu kiasi cha sukari kwenye chakula ua kiasi cha chakula chote unachokula.
Kisukari cha ujauzito: Kuna baadhi ya wamama ambao sukari kwenye damu zao hupanda wakati wa uja uzito na huteremka mara wanapojifungua. Baadhi ya wamama hao sukari inaweza isiteremke tena hata baada ya kujifungua na wakabakia wagonjwa kisukari moja kwa moja hasa kama ni wanene kupitiliza na baada ya kujifungua mimba nyingi. ·
Nini tofauti ya aina ya kwanza na ile ya pili ya kisukari?
Dalili |
Aina ya kwanza |
Aina ya pili |
| Umri wa kuanza ugonjwa | Miaka chini ya 40. | Miaka zaidi ya 50. |
| Muda wa dalili za ugonjwa kabla hajagundulika kuwa na kisukari. | Wiki | Miezi hadi miaka. |
| Uzito wa mgonjwa wakati anagulika kisukari | Wa kawaida au pungufu | Mnene. |
| Ketoni kwenye mkojo | Zipo | Hazipo. |
| Kifo cha haraka hasipotumia insulini. | Ndiyo. | Hapana. |
| Matokeotata ya kisukari wakati anagulika kisukari | Hakuna. | Yapo. |
| Mtu mwingine mwenye ugonjwa wa kisukari katika familia. | Kwa kawaida hayupo | Yupo. |
Je, Ugonjwa huu unasababishwa na kula sukari nyingi?
La hasha. Kula sukari nyingi sio sababu ya ugonjwa kisukari. Lakini lazima tuseme kwamba kula sukari nyingi si nzuri kwa afya yako kwani utaongeza uzito na kuweza kuathiri uwezo wa mwili wako kujikinga na maradhi tofauti. Hivyo sukari tutumie lakini kwa uangalifu.
Kitu gani husababisha ugonjwa wa kisukari?
- Magonjwa ya ini.
- Unene kupita kiasi.
- Msongo wa mawazo.
- Kurithi kutoka kwa wazazi.
- Kuvuta sigara wakati wa ujauzito.
- Kutumia nyama ilivyofukizwa moshi.
- Kuondolewa kongosho kwa upelesheni.
- Kuharibika kongosho kwa ajali au moto.
- Magonjwa ya kongosho mfano uvimbe kwenye kongosho unaosababishwa na pombe au virusi (mfano: Rubella, mumps, HIV
- Dawa: § Phenytoin. § Thiazide mfano bendrofluazide. § Steroidi mfano prednisolone, dexamethasone n.k.
- Utapia mlo wa mtoto kabla hajazaliwa (intrauterine malnutrition).
- Utumiaji wa maziwa ya ngombe kwa mtoto kabla ya umri wa miezi 3.
- Magonjwa ya yanayotengeneza antibodizi zinazoshambulia mwili (autoimmune disease).
Nini dalili za kisukari na damusuziada?
- Kukonda.
- Kutoona vizuri.
- Kuumwa na kichwa.
- Kuchoka bila ya kufanya kazi.
- Kula sana kwa sababu ya kusikia njaa sana.
- Kunywa maji sana kwa sababu ya kujisikia kiu mara kwa mara.
- Kusikia ganzi, kuchomwachomwa au maumivu kwenye mikono na miguu.
- Kujisaidia haja ndogo mara kwa mara, Mgonjwa hujisaidia zaidi ya mara tatu usiku.
Utafahamuje kama ugonjwa wa kisukari umeutawala vizuri?
Kama huna dalili zozote na unajisikia vizuri. Huamki usiku kujisaidia haja ndogo zaidi ya mara moja. Kama unapima glukozi kwenye damu na unakuta hakuna damusuziada (hyperglycaemia). Glukozi kwenye damu ni sawa ikiwa kati ya miligramu 80-144 kwa kila desilita ya damu (kati ya milimoli 4-8 kwa kila lita ya damu).
Kwa nini uhangaike kuutawala ugonjwa wako wa kisukari?
Utakuwa huna dalili zozote. Utaishi maisha marefu zaidi. Kwa hiyo utaweza kuishi maisha karibu ya kawaida. Mwili utakuwa na nguvu zaidi za kupigana na maambukizo. Utazuia matokeotata (complications) mengi yanyoweza kusababishwa na ugonjwa wa kisukari.
Je, ugonjwa wangu wa kisukari unaweza kupona?
Kwa ujumla, ukishapata ugonjwa wa kisukari utakuwa nao maisha. Lakini hakuna sababu kwa nini usiweze kuishi maisha ya kawaida na mazuri.
Kwa dawa za hospitali mpaka sasa hakuna dawa ya kuondoa moja kwa moja ingawa hasa kwa aina ya 2 watu baada ya kurekebisha vyakula wanaweza kujiweka katika hali hali ambayo mwili unaweza kutumia insulin yake kidogo bila ya kula vidonge au sindano.
Kuna utafiti wa kufanya transplant ili kuongeza insulin mwilini kwa kutumia sehemu (pancreas) ya mtu mwengine lakini bado haujafanikiwa kuweza kutumika kama ni matibabu.
Je, watoto wangu wanaweza kuurithi?
Wakati mwingine zaidi ya mtoto mmoja katika familia wanaweza kuwa na ugonjwa huo. Lakini urithi wa ugonjwa huu kwa watoto ni mdogo sana kwa kawaida. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi.
Je, nikiwa na ugonjwa wa kisukari ninaweza kuoa au kuolea na kuwa na watoto?
Ndiyo. Ugonjwa huu haumzuii mtu kuoa au kuolewa.
Je, ni zipi athari za ugonjwa huu?
Baada ya muda mrefu ugonjwa wa sukari huleta athari ya mishipa ya fahamu na kusababisha kupoteza hisia za ngozi na viganja au nyayo na kupungua nuru ya macho. Pia athari ya mafigo huweza kujitokeza na uzungukaji wa damu unaweza kupungua katika baadhi ya sehemu na kusababisha kufa kwa sehemu za mwili.
Kujitokeza kwa dalili hizi kunategemea ni kiasi gani matibabu yamefanikiwa na wakati wa kuanza kwa matibabu hayo baada ya kujuilikana kwamba mtu ana ugonjwa huu.
Je, ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa wa kuambukiza kama vile kifua kikuu au ukoma? Hapana. Huwezi kuambukizwa ugonjwa wa kisukari.
Vipi naweza kujikinga na ugonjwa huu?
Ikiwa unayo historia katika familia sio lazima kwamba utapata ugonjwa huu. Lakini kwa wale ambao wanaweza kuupata wanaweza kuuchelewesha kwa kujitahidi kuishi maisha ya afya nzuri kwa kula chakula bora, mazoezi, kula mboga mboga kwa wingi na kujiepusha na uzito wa mwili. Pia kupima damu baada ya kila muda ikiwa una historia katika ukoo au una wasi wasi kutokana na dalili zilizotajwa hapo juu.
===
1. AINA YA MLO UFAAO KWA WAGONJWA WA KISUKARI
---
2. MATOKEO YA KUTODHIBITI UGONJWA WA KISUKARI
===
UFAFANUZI, USHAURI NA MAONI YA WADAU KUHUSU TATIZO HILI:
---
---
---
---
===
PIA UNASHAURIWA KUSOMA MADA HIZI:
- Tambua siri ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari - JamiiForums
- Dawa nyingi mbadala za Ugonjwa wa kisukari zinazotangazwa ni utapeli mtupu, fuata ushauri huu - JamiiForums