Dar es Salaam. Msanii wa filamu na mfanyabiashara Tausi Mdegela anasema kutokana na kimo chake kifupi, kuna baadhi ya watu katika jamii na mitandao wanaona hastahili kufanya baadhi ya vitu.
Hayo ameyasema wakati akifanya mahojiano na Mwananchi na kuongezea kuwa kwa sasa amezoea kudhihakiwa.
“Nikitaka kufungua mlango ndio nakumbuka mimi ni mfupi, naanza kumuita dada yangu wa kazi anifungulie, nje na hapo sijiwazii kimo changu, napenda kufanya kazi kwa bidii na siangalii uigizaji pekee,” anasema.
Anasema licha ya kumiliki kitanda kikubwa analazimika kulala chini kwa ajili ya kuepukana na hekaheka za kupanda kitandani.
“Nina kitanda kikubwa lakini godoro naweka chini kwa sababu siwezi purukushani za kupanda na kushuka, lengo langu la kukinunua ni kumfanya binti yangu azoee mazingira hayo ili akienda kwa watu asione vitu vigeni.
“Ukiachana na kitanda ndani kwangu hakuna viti vya kukalia, nimeweka zuria na mito kwani siwezi kujitesa kupanda juu, nimeamua kujikubali nilivyo, nitaishi maisha ya furaha na siyo kufurahisha watu, pia nikitaka kushona nguo nakata mita mbili,"anasema
Hataki unyonge kwa binti yake
Tausi amejaaliwa kupata mtoto wa kike jina lake Pavitrah, anasema kipindi cha nyuma alipokuwa akienda kucheza na wenzake walikuwa wanamtania na kumwambia mama yake ana mwili mdogo na mfupi, jambo ambalo lilikuwa linamuumiza.
“Pavitrah mwanzoni alikuwa anakuja kusemelea anavyotaniwa na wenzake ananiambia mama wanasema wewe una kamwili kadogo na mfupi, nikawa namwambia mwanangu ni kweli mimi ni mfupi, ila nakupenda sana wakikwambia tena wajibu ndiyo mama yangu mfupi ila ni staa kuliko mama zenu.
“Siku moja akaenda kucheza wakaanza kumtania akawajibu kama nilivyomwambia, akarudi akanimbia mama nimewaambia kama ulivyonifundisha hawajarudia kunitania tena,"anasema
Changamoto za huduma za kijamii
Anasema kuna wakati akienda kupata huduma za kijamii sehemu zenye majengo ya ghorofa kwake inakuwa changamoto, kwani anaona kuna umbali mrefu kupanda ngazi.
“Hata kama kuna lifti lazima niwe na mtu ambaye anaweza akanisaidia kubonyeza zile namba za lifti kwani siwezi kufikia zilipo.Changamoto nyingine ninayoipata nikitaka kutoa pesa ATM sifikii kwenye mashine ile, hivyo nakuwa namuomba bodoboda wangu ama dereva bajaji anayeniendesha.
View attachment 3204435View attachment 3204436