MH. JOB NDUGAI: MTANZANIA ATOKAE FAMILIA ILIYOGUBIKWA NA LINDI LA UFUKARA NA UMASKINI ULIOKITHIRI AWA SPIKA WA KWANZA TANZANIA KUBWAGA MANYANGA !!!
_______________________________________
Januari 6, 2022
Na Mzee wa Atikali ✍️ ✍️✍️
"Mimi nimetokea Kongwa, Dodoma eneo lenye ukame sana. Dodoma kuna mvua chache hivyo umaskini ni changamoto kubwa. Mimi nimekulia maisha ya shida na dhiki kubwa mno. Nilikuwa natembea maili kumi kwenda na kurudi toka shule kila siku. Hata siku moja sikuwahi kuwaza kuwa nitakuja kuwa Mwanasiasa, Mbunge au Spika wa hili Bunge letu. Ni kutokana na kusoma kwa bidii na kudra za Mwenyezi Mungu nimefika hapa nilipo leo".
Mh. JOB NDUGAI, Juni 15, 2020
1.
Usuli
Mh. JOB YUSTINO NDUGAI
"JYN" ni Spika wa 7 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mmoja wa Wakuu wa Mihimili Mitatu ya Serikali.
Hata hivyo, leo Alhamis, Januari 6, 2022, Mh.
JYN amebwaga manyanga kwa kuamua kujiuzulu uspika kwa hiari yake mwenyewe na kwa maslahi mapana ya Taifa.
Kwavile kuna baadhi ya Watanzania ambao humwonaga tu akiongoza bunge lakini hawamjui kiundani,
"Atikali" hii inamuelezea Mh.
JYN toka kuzaliwa kwake hadi siku ya leo alipojiuzulu uspika.
2.
JYN Azaliwa
JYN alizaliwa siku ya Alhamis, Januari 21, 1960 huko Kongwa, Idodomia akiwa mtoto pekee kwa mama yake.
3.
JYN Atokea Familia ya Kifukara
JYN ni Mtanzania aliyetokea kwenye familia yenye maisha yaliyogubikwa na lindi la ufukara.
3.1
JYN Alalia Ngozi ya N'gombe
Ufukara ulipelekea
JYN alale nyumba ya tembe yenye kitanda kikuukuu cha kamba ambapo juu yake ilitandikwa ngozi ya ng'ombe badala ya godoro hivyo usingizi wa mang'amung'amu hasa miezi ya baridi (Juni & Julai) lilikuwa jambo la kawaida kwake.
3.2
JYN Aamka na Ng'ombe Usiku
Siku za Jumamosi & Jumapili ilikuwa ni zamu ya
JYN kuchunga ng'ombe. Kutokana na ukame mkubwa na hivyo ng'ombe kukosa maji ya kunywa, ilibidi
JYN awe analazimika kuamka saa 9 usiku kwaajili ya kuwapeleka ng'ombe milimani kwenye chemchem ya maji!. Hadi kuyafikia maji hayo ilikuwa ni mwendo wa masaa 3. Baridi kali lilikuwa likimpiga kwani mavazi yake makuukuu yaliyo na viraka hayakufua dafu mbele ya baridi la alfajiri. Huko kwenye chemchem kulikuwa na makundi mengine ya ng'ombe yaliyoletwa na watu wengine hivyo ilibidi kusubiriana. Wakati wa kurudi, baada ya kuwanywesha maji, alikuwa akiwalisha ng'ombe njiani. Hii ilipelekea awe anafika nyumbani usiku huku tumbo likiwa tupu! Kwa hakika, ilikuwa ni shughuli pevu sana kwake kwani alikuwa na umri mdogo!.
4.
Elimu ya Msingi
JYN alianza elimu ya msingi mwaka 1971 akiwa na miaka 11 kwenye shule iliyoitwa Sagara.
4.1
Shule Ilikuwa Umbali wa Maili 5
Shule ya Sagara ilikuwa iko umbali wa maili 5 toka kijiji cha Laikala alikokuwa akitokea
JYN. Hii ilipelekea
JYN awe anatembea jumla ya maili 10 kwa siku kwa maana ya 5 kwenda na 5 kurudi.
JYN akiongea na BABY KABAYE wa Clouds FM katikati ya Juni 2020, alifafanua-:
"Ilikuwa si kazi ndogo kwenda na kurudi toka shuleni kwani kijijini kwetu ni swekeni kwelikweli".
4.2.
JYN Afaulu Mtihani Darasa la 7
JYN alikuwa ni kijana aliyekuwa na bidii sana ya masomo kwani aliamini kuwa ni elimu tu ndiyo ingemtoa kwenye maisha ya kifukara. Hivyo, mwaka 1977,
JYN alifanya mitihani wa darasa la saba na kuwa mmoja wa wanafunzi wachache wa shule hiyo waliofaulu.
5.
Elimu ya Sekondari
5.1
Kibaha
Mwaka 1978,
JYN alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Kibaha. Mmoja kati ya wanafunzi aliosoma nao shule hiyo ni Bw. FREEMAN MBOWE.
Shuleni hapo, hali ya ufukara ya
JYN haikujificha bali ilionekana wazi.
JYN alisoma kwenye shule hiyo kwa miaka 4 na alimaliza masomo yake mwaka 1981 alipofanya mtihani wa kumaliza elimu ya
"O Level".
5.2
Old Moshi
JYN alifaulu vizuri mtihani wa kidato cha nne na akachaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano
"Old Moshi Secondary school" mwaka 1982 na akamaliza kidato cha sita mwaka 1984.
6.
JYN Ajiunga na JKT
Mwaka 1985,
JYN alijiunga na mafunzo ya lazima ya JKT ya mwaka mmoja kumjenga kuwa Mzalendo.
JYN alipatia mafunzo hayo kwenye kambi za Ruvu JKT na Maramba JKT.
7.
JYN Ajiunga Chuo cha Mweka
Mwaka 1986,
JYN alijiunga na chuo cha Mweka, Moshi kuchukua Diploma ya Usimamizi wa Wanyama Pori.
7.1
JYN Aishi Maisha ya Kifukara
JYN, akiwa chuoni Mweka, alikuwa ni maskini wa kutupwa kiasi kwamba hakuwa na hata nauli ya kurudi kwao, Kongwa wakati wa likizo!. Hii ilikuwa ni fedheha kubwa lakini hakuwa na jinsi kama alivyotiririka bungeni Juni 15, 2020-:
"Mweka tulikuwa wanafunzi toka mataifa mbalimbali. Nilikuwa mwanafunzi maskini sana. Sikuwa na nauli ya kurudi kwetu. Wenzangu walipokuwa wanaondoka chuoni, nilikuwa najificha kwa kuogopa kuulizwa swali hili-"We kwanini huendi kwenu?". Mkuu wa Chuo akawa ananipa vijikazi vya kufyekafyeka, kupanga vitabu stoo, kuwasaidia walimu projects zao, kukusanya data nk".
JYN alisoma hivyohivyo kiugumuugumu hadi akamaliza mafunzo yake.
8.
JYN Afanya Kazi Wizara ya Maliasili
Mwaka 1988,
JYN alifanya kazi kama Muhifadhi wanyama pori, wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.
9.
JYN Ajiunga UDSM
Mwaka 1989,
JYN , kijana aliyekuwa na kiu kubwa ya masomo, alijiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlimani kwenye kozi ya Sayansi ya Hifadhi.
10.
JYN "Atimuliwa" UDSM!
10.1
Wanafunzi Wafanya "Kunji"!
Miezi ya mwanzoni mwa mwaka 1990, ilifanyika
"Kunji ya Karne"( mgomo mkubwa) UDSM kwani wanafunzi walikuwa na madai mbalimbali mf madai ya nyongeza za
"Meal allowance" & "Field Allowance". Kunji hiyo ilikuwa kubwa hadi kuitikisa nchi huku ikipamba kurasa za mbele za magazeti ya
"Daily News" & Uhuru pamoja na kuongelewa sana na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) hususan kwenye kipindi maarufu cha
"Mazungumzo Baada ya Habari" kilichotumika
"kuwanyali" wanafunzi hao.
10.2
Rais MWINYI Atinga UDSM
Mei 7, 1990, Rais wa Awamu ya Pili, Mh. ALI HASSAN MWINYI aliyekuwa Mkuu wa Chuo, alifika chuoni na kuyazungukia maeneo ya chuo yakiwemo mabweni ya wanafunzi na kisha akafanya mikutano kadhaa.
10.3
Wanafunzi Wamtukana Rais MWINYI "Matusi ya Nguoni"!
Wakati
"Kunji" hiyo ikirindima chuoni hapo, baadhi ya wanafunzi wakawa, bila woga, wakimtukana "matusi ya nguoni" Rais MWINYI na Waziri wa Habari, Mh. AHMED HASSAN DIRIA, kwenye mbao za matangazo ya kafeteria za Manzese na Yombo!. Kwa hakika yalikuwa ni matusi mazito sana na wakati mwingine na picha za viongozi hao ziliambatishwa "kunogesha" matusi hayo!.
10.4
Rais MWINYI Awaomba Wanafunzi Warejee Madarasani
Rais MWINYI, kwa unyenyekevu mkubwa, aliwasihi wanafunzi kurejea madarasani. Hata hivyo, wanafunzi hao waliendelea kushikilia msimamo wao bila kutetereka!.
10.5
Wanafunzi wote Watimuliwa Chuo
Kutokana na jitihada za kuwafanya wanafunzi warejee madarasani kushindikana huku mbao za matangazo zikitamalaki matusi, wanafunzi wote walitimuliwa chuoni hapo!.
Wanafunzi hao walitimuliwa Jumamosi ya Mei 12, 1990 ambapo RTD kupitia mtangazaji wake mahiri, AHMED JONGO, iliutangazia umma uamuzi huo kwenye taarifa ya habari ya saa 7 mchana ambapo walitakiwa kuwa wameondoka chuoni hapo kufikia saa 12 jioni. Wanafunzi wote, akiwepo
JYN, wakaondoka mara moja chuoni kwenda makwao kwani FFU walitanda kila mahali chuoni hapo. Katika kipindi cha propaganda cha RTD
"Mazungumzo Baada ya Habari" saa 2.10 usiku wa siku hiyo, ilielezwa kuwa-:
"Wanafunzi hao wamefukuzwa kutokana na kushinikiza kupewa chai ya maziwa, mkate wa siagi na mayai, vitu ambavyo hata kwenye familia zao vijijini walikuwa hawavipati"!.
Kutimuliwa huko kulienda sambamba na adhabu ya kukataza wanafunzi hao kuajiriwa sehemu yoyote! Hii ilikuwa ni adhabu kali sana kwani baadhi ya wanafunzi hao walikuwa na familia zilizokuwa zinawategemea.
10.6
Rais MWINYI Aongea na Wazee wa Dsm
Kutokana na hali kuwa tete, Rais MWINYI aliongea na wazee wa Dsm na kuwaeleza kinagaubaga Watanzania nchi nzima kupitia kwa wazee hao kuhusu mgomo huo. Siku hiyo ndipo Rais MWINYI alipotoa kauli ambayo imekuwa ikirejewa sana na Wanazuoni-:
"Mimi niliwaomba vijana wale warejee madarasani lakini wakakataa na badala yake wakawa wananitukana matusi ya nguoni!. Baadaye wakadai kuwa kauli yangu ilikuwa ni ombi tu hivyo walikuwa na hiari ya kuitekekeza ama kutoitekeleza. Ndugu zangu, niwaambieni ukweli-: Ombi la Rais ni Amri"!.
10.7
Wanafunzi Wasio na Makosa Warejeshwa Chuoni UDSM
Mchujo mkali ulifanyika na wanafunzi wasio na hatia, akiwemo
JYN, wakarudishwa chuoni baada ya mwaka mzima kusota na kunyanyapaliwa na jamii. Hivyo basi,
JYN akamaliza UDSM 1993 badala ya 1992.
11.
JYN Aenda Masomoni Norway
JYN alipenda sana elimu hivyo alipomaliza tu UDSM akaunganisha kwenda chuo cha
"Agricultural University of Norway" mwaka 1994 aliposomea Diploma na akaendelea hadi kupata shahada ya Uzamili mwaka 1996.
12.
JYN Arejea, Awa Mkurugenzi
Baada ya kupata shahada yake ya uzamili,
JYN alirejea nchini na kati ya mwaka 1996 hadi 1998, akawa Mkurugenzi wa Miradi kwenye mbuga ya Serengeti.
13.
JYN Awa Afisa Mtafiti
Mwaka 1998,
JYN aliajiriwa kama Afisa Mtafiti wa Tawiri.
14.
JYN Ajitosa Ubunge 2000
14.1
JYN Ashindana na Maprofesa
Mwaka 2000,
JYN akiwa kijana mdogo wa miaka 40, alijitosa kinyang'anyiro cha ubunge jimboni Kongwa kupitia CCM, akiwa ni mdogo kuliko wagombea wenzie 10 wakiwemo maprofesa na madaktari ambao walikuwa wakimdhihaki.
14.2
JYN Awasambaratisha Maprofesa!
Katika kura za maoni,
JYN aliwatimulia vumbi washindani wake wote baada ya kushinda kwa 90%.
14.3
RC Ashangazwa, Atinga Kongwa!
Uongozi wa CCM Mkoa wa Idodomia pamoja na RC ISIDORY SHIRIMA hawakuamini kuona kijana mdogo asiejulikana akiwaangusha vigogo. Ushindi huo wa kimbunga wa
JYN ulipelekea viongozi hao kwenda Kongwa kujua kilichojiri. Viongozi hao walifanya uchunguzi na kubaini
JYN alishinda kihalali na hakukuwa na
"figisufigisu".
JYN aliposhindana na wagombea wa vyama vingine akawasambaratisha na kutangazwa mshindi wa kiti cha ubunge, Kongwa.
15.
JYN Awa Mjumbe wa Kamati
Mara baada ya kuingia bungeni na kuapishwa,
JYN aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Maliasili huku Mwenyekiti akiwa Bi. ANNE MAKINDA.
16.
JYN Ashinda tena Ubunge
Mwaka 2005,
JYN aligombea tena ubunge jimbo la Kongwa na kushinda kwa kishindo kama kawaida yake.
17.
JYN Awa Mwenyekiti wa Bunge
JYN alipata heshima ya kuwa Mwenyekiti wa Bunge ambapo alikuwa akiendesha Bunge wakati Mh Spika & Naibu wake walipokuwa hawapo.
18.
JYN Ashinda Tena Ubunge
Mwaka 2010,
JYN aligombea tena ubunge na kuibuka kidedea.
19.
JYN Asomea Sheria "OU"
JYN aliamua kujiendeleza zaidi ili apate weledi kwenye utendaji kazi hivyo akasomea na kuhitimu Chuo Kikuu Huria
"Open University " shahada ya Sheria
20.
JYN Awa Mchangiaji Bora
JYN alitajwa kuwa ndiye alikuwa mchangiaji mkubwa bungeni kipindi cha 2005 hadi Agosti 2010 bunge lilipovunjwa.
JYN aliuliza maswali 29, maswali ya nyongeza 60 na michango mingine 289. JYN alifuatiwa na Mh. JENISTER MHAGAMA na Dr. WILBROAD SLAA.
21.
Mh. JYN Awa Naibu Spika
Nyota ya
JYN iliendelea kung'ara ambapo mwaka 2010, alichaguliwa kuwa Naibu Spika kuchukua nafasi ya Bi. ANNE MAKINDA ambaye alikuwa amechaguliwa kuwa Spika.
22.
JYN Agombea Tena Ubunge
Mwaka 2015, kama kawa,
JYN alijitosa kinyang'anyiro cha ubunge jimboni Kongwa.
22.1
JYN Apandwa Munkari, Atembeza Bakora!
JYN sio mtu wa mchezo mchezo! Katika kinyang'anyiro cha kura za maoni mwaka 2015,
JYN alimcharaza bakora mgombea mwenzake wa CCM, Dr. JOSEPH CHILONGANI, na kuzua songombingo kubwa! Wakati wa zoezi la kujinadi,
JYN alikuwa akifanya mambo ya ajabu yasiyoendana na hadhi ya Spika ndipo Dr. CHILONGANI alipoamua kumrekodi, kitu kilichomkasirisha sana
JYN aliyeamua kumtia adabu kwa kutumia fimbo ambayo huwa anatembea nayo wakati wa kampeni.
JYN alimtandika maeneo ya tumboni na kichwani Bw. CHILONGANI ambaye hapohapo akapoteza
"network" kwa muda!.
23.
Mh. JYN Ashinda Tena Ubunge
Katika kinyanganyiro hicho cha ubunge,
JYN alibuka mshindi kwa kuhomola kura 73,165 na kumshinda Bw. NGOBEI FREMONT aliyepata kura 20,335.
24.
Mh. JYN Awa Spika
Nyota ya
JYN iliendelea kung'ara ambapo Novemba 17, 2015 alipochaguliwa kuwa Spika.
JYN alipata kura 233 dhidi ya kura 109 za mpinzani wake, Mh. GOODLUCK OLE MEDEYE wa CHADEMA.
25.
JYN Ashinda Kura za Maoni
JYN alijitosa tena kinyang'anyiro cha ubunge na kushinda kura za maoni jimboni Kongwa, ambapo mwezi Julai 2020, alitangazwa mshindi baada ya kuhomola kura 850. Hii ilimfanya kuwa ni mmoja wa wana CCM walioongoza kwa kupata kura nyingi.
26.
JYN Apita Bila Kupingwa
JYN alipita bila kupingwa na kukabidhiwa hati yake Agosti 27, 2020 kufuatia wagombea wa upinzani kukosa vigezo.
27.
JYN Awa Spika Tena
JYN alichaguliwa kwa kishindo kuwa Spika wa Bunge la 12 baada ya kuhomola kura 344 kati ya 355 ambayo ni sawa na 99.7%.
JYN alikuwa mgombea pekee kwani wapinzani
"hawakutia timu"!
28.
JYN Augua, Alazwa ICU India!
Mwaka 2018 ulikuwa mgumu sana kwa
JYN kwani aliugua sana hadi kupelekwa India akiwa na mkewe.
JYN alimweleza mtangazaji BABY KABAYE wa Clouds FM Juni 2020-:
"Nilikuwa naumwa sana nikapekekwa hospitalini India. Kule nikawekwa chumba cha ICU. Kuna wakati nilikuwa naona kama hakutakucha vile! Mke wangu, Dr. Fatuma, alikuwa akilala kwenye kiti masaa 24 humo ICU kwa siku kadhaa. Alipata shida sana. Huyu ni mke mwema sana".
29.
JYN Hajui ana Watoto Wangapi!
Kuhusu idadi ya watoto alionao,
JYN akihojiwa na
"Star Tv" Julai 29, 2012, alitiririka-:
"Ni vigumu kwa mwanaume kujua una watoto wangapi kwani kuna pitapita nyingi, hivyo unaweza kutaja idadi isiyo sahihi".
Hata hivyo,
JYN akiliaga bunge Juni 15, 2021 alifika bungeni na kuelezea kuhusu familia yake.
JYN alisema ana mke aitwaye Dr. FATUMA RAMADHANI MGANGA na watoto watatu ambapo mmoja mkubwa ni wa kiume.
Dr. FATUMA ni
"Medical Doctor" na DED wa Bahi.
30.
JYN Hakai Nyumba ya Spika!
Mjini Idodomia kuna nyumba nzuri maalum kwa Spika yenye kila kitu ikiwemo
"Swimming pool". Nyumba hiyo ipo eneo la wazito karibu na polisi kwa juu.
JYN alijenga nyumba yake eneo la Kisasa mwishoni mwa miaka ya 2000 na ndiko anakoishi. Hivyobasi, nyumba ya spika inatumiwa na wageni maalum wa bunge wanapokuwa Idodomia.
31.
Maisha ya Umaskini Yanapelekea JYN Kuwa na Munkari!
Kutokana na
JYN kupitia kwenye maisha ya umaskini ukiokithiri, imepelekea awe na hasira; kama anavyotiririka-:
"Kutokana na aina ya maisha ya dhiki niliyopitia, saa zingine Waheshimiwa wabunge mnisanehe ninapohamaki nikutanapo na mtu mjinga"
32.
JYN Mpenzi Kindakindaki wa "MNYAMA"
JYN ni shabiki mkubwa wa mpira wa miguu. Yeye ni mpenzi mkubwa wa SIMBA kama alivyo Waziri Mkuu, Mh. MAJALIWA KASSIM MAJALIWA. Wawili hawa mara kwa mara huonekana wakiwatania na kuwakoga mashabiki wa Yanga hususan aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dr. PHILLIP MPANGO na Waziri wa Fedha, Dr. MWIGULU NCHEMBA.
Akihojiwa na mwandishi BABY KABAYE wa Clouds FM, Juni 15, 2020 kuhusu timu aipendayo Tanzania na nje,
JYN alitiririka-:
"Kwa hapa nyumbani, mimi ni mpenzi mkubwa wa Simba na kwa nje timu ninayoshabikia ni Manchester City".
33.
TAMATI-: JYN Abwaga Manyanga
Januari 6, 2022, ni siku ambayo daima itabaki kwenye kumbukumbu ya JYN kwani aliamuru kujiuzulu uspika. Mh. JYN ameandika barua ya kujiuzulu kwa Katibu wa Bunge akieleza kwamba amechukua uamuzi huo kwa hiari yake binafsi na kwa maslahi mapana zaidi ya Taifa lake.
Desemba 28, 2021, Mh.
JYN akizungumza katika Mkutano mkuu wa pili wa Wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyija Idodomia, alitiririka-:
"Juzi mama ameenda kukopa 1.3 trilioni. Hivi ipi bora, sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubananebanane hapahapa, tujenge wenyeee bila madeni haya makubwamakubwa yasioeleweka? Ni lini sisi tutafanya wenyewe"?.
Mh. Rais Samia Suluhu Hassan alikerwa sana na kauli hiyo ambapo alieleza kwa hisia kali Januari 4, 2022, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa fedha hizo na kuihusisha kauli ya
JYN na homa ya urais 2025. Aidha, Mh. Rais aliihusisha na kauli aliyokuwa akiisikia mjengoni kwa akina KASSIM kuwa Serikali yake ni ya mpito kitu ambacho si cha kweli!
Na Mzee wa Atikali ✍️✍️✍️
Atikaligbm@yahoo.com
0754744557