Mchezaji wa zamani wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Alan Shearer amesema kocha wa Manchester United, Erik ten Hag ana michezo miwili pekee ya kuokoa kibarua chake.Man United ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 14, katika mechi tatu za mwanzo za EPL imeshinda moja na kupoteza mbili.
Kutokana na kuanza vibaya, wachambuzi na mashabiki wengi wamekuwa wakimshambulia Ten Hag wakiamini yeye ndio tatizo kwani timu imetumia zaidi ya Pauni 200 milioni kwa ajili ya kufanya maboresho mbalimbali ikiwa pamoja na kuwasajili Joshua Zirkzee, Leny Yoro, Manuel Ugarte na Matthijs De Ligt.
Ripoti zinadai Ten Hag yupo kwenye presha kubwa ya kufutwa kazi ingawa baadhi ya viongozi wa juu wa timu hiyo bado wanataka aendelee na wana imani naye.
Kwa upande wake Shearer anaamini kocha huyo ana michezo miwili tu inayofuata kuamua juu ya hatma yake ikiwa atabakia au laa.