Tendwa atabiri viti 100 vya ubunge kwenda upinzani
Tuesday, 31 August 2010 22:25
Na Ramadhan Semtawa
WAKATI joto la uchaguzi likizidi kupanda, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tenda ametabiri kuwa vya vya upinzani vinaweza kupata viti 80 hadi 100 kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kama watacheza karata zao vizuri. Msajili ametoa kauli hiyo wakati upinzani ukionekana kuzidi kukua baada ya wabunge kadhaa wa chama tawala kuhamia vyama vya upinzani kutokana na kutokubaliana na mchakato wa kura za maoni na matokeo yake, huku baadhi ya vyama vikijiimarisha kwenye majimbo kwa kuweka wanachama wenye nguvu, wakiwemo viongozi wao wakuu.
Wanachama wengi walioihama CCM na kuhamia upinzani wamesimamishwa kwenye majimbo waliyokuwa wakiyashikilia zamani kupambana na chama tawala, wakati Chadema na TLP zikisimamisha wenyeviti wao kugombea ubunge.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuhusu mwelekeo wa uchaguzi huo, Tendwa alisema mtazamo wake unatokana na sababu kuu nne ambazo anaamini zitaongeza idadi ya wapinzani bungeni kama wakicheza vizuri karata zao.
"Wapinzani wanaweza kupata viti kati ya 80 hadi 100 kama wataweza kujipanga vema. Temperature (joto) ya kisiasa iko juu sana kwa sasa," alisema msajili huyo.
Tendwa aliitaja sababu ya kwanza kuwa ni mwamko mkubwa ambao ameuona kwa Watanzania katika kushiriki kwenye mchakato wa kuchagua viongozi, hali ambayo alisema imepandisha joto la kisiasa.
"Mwamko wa Watanzania ni mkubwa sana," alifafanua Tendwa.
Mkuu huyo wa ofisi hiyo yenye dhamana ya malezi na kuangalia mwenendo wa vyama vya siasa nchini, alitaja sababu nyingine kuwa ni kuwepo kwa mwamko pia kuanzia ndani ya vyama vyenyewe vya siasa.
Alisema yapo mabadiliko ndani ya vyama ambayo yameongeza joto la kisiasa kutokana na mwamko mpya ambao awali haukuwepo kutokana na mazingira ya mfumo na wakati.
"Unaangalia pia public (umma) inasema nini. Ukiangalia ndani ya vyama kuna watu ambao hawakuwa wametarajiwa kuong'olewa, lakini wameangushwa kwenye kura za maoni wakati wa mchakato wa wabunge," alifafanua.
"Kura za maoni ndani ya vyama zimeonyesha public inasema nini. Kuna mwamko mkubwa kwa wapigakura ambao tumeona si ndani ya chama tawala pekee ambako kuna majina yasiyotarajiwa yaliangushwa, bali hata ndani ya vyama vya upinzani kulikuwa na mwamko mkubwa."
Wabunge wengi vigogo ndani ya CCM, akiwemo mwanasiasa mkongwe John Malecela, waliangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM, sambamba na mawaziri watano.
Visiwani Zanzibar, zaidi ya wawakilishi 10 wanaomaliza muda wao walianguka kwenye kura za maoni za CUF, huku Chadema ikikumbwa na mapambano kwenye baadhi ya majimbo na uchaguzi wa wabunge wa viti maalum kiasi cha uongozi kuamua kusitisha mchakato huo.
"Umeona uchaguzi wa wabunge wa viti maalum wa Chadema umeahirishwa; hii yote ni mwamko kwa wapigakura kuanzia ndani ya vyama," alisema Tendwa.
Tendwa alisema sababu ya tatu ni kuwepo mabadiliko ndani ya chama tawala ambayo yamesababisha baadhi ya makada kwenda vyama vya upinzani kwa wingi.Alieleza kuwa zamani haikuwa rahisi kuona makada kutoka chama hicho tawala wakikihama na kukimbilia upinzani kama ilivyo sasa hivi.
Chanzo:Mwananchi