Msajili wa vyama vya siasa John Tendwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu ofisi yake kupokea rasmi malalamiko ya chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema yanayodai mgombea urais kupitia CCM kukiuka sheria ya ghalama za uchaguzi . Picha na Said Powa
Na Ramadhan Semtawa
WAKATI joto la uchaguzi likizidi kupanda, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tenda ametabiri kuwa vya vya upinzani vinaweza kupata viti 80 hadi 100 kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kama watacheza karata zao vizuri. Msajili ametoa kauli hiyo wakati upinzani ukionekana kuzidi kukua baada ya wabunge kadhaa wa chama tawala kuhamia vyama vya upinzani kutokana na kutokubaliana na mchakato wa kura za maoni na matokeo yake, huku baadhi ya vyama vikijiimarisha kwenye majimbo kwa kuweka wanachama wenye nguvu, wakiwemo viongozi wao wakuu.
Wanachama wengi walioihama CCM na kuhamia upinzani wamesimamishwa kwenye majimbo waliyokuwa wakiyashikilia zamani kupambana na chama tawala, wakati Chadema na TLP zikisimamisha wenyeviti wao kugombea ubunge.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuhusu mwelekeo wa uchaguzi huo, Tendwa alisema mtazamo wake unatokana na sababu kuu nne ambazo anaamini zitaongeza idadi ya wapinzani bungeni kama wakicheza vizuri karata zao.
"Wapinzani wanaweza kupata viti kati ya 80 hadi 100 kama wataweza kujipanga vema. Temperature (joto) ya kisiasa iko juu sana kwa sasa," alisema msajili huyo.
Tendwa aliitaja sababu ya kwanza kuwa ni mwamko mkubwa ambao ameuona kwa Watanzania katika kushiriki kwenye mchakato wa kuchagua viongozi, hali ambayo alisema imepandisha joto la kisiasa.
"Mwamko wa Watanzania ni mkubwa sana," alifafanua Tendwa.
Mkuu huyo wa ofisi hiyo yenye dhamana ya malezi na kuangalia mwenendo wa vyama vya siasa nchini, alitaja sababu nyingine kuwa ni kuwepo kwa mwamko pia kuanzia ndani ya vyama vyenyewe vya siasa.
Alisema yapo mabadiliko ndani ya vyama ambayo yameongeza joto la kisiasa kutokana na mwamko mpya ambao awali haukuwepo kutokana na mazingira ya mfumo na wakati."Unaangalia pia public (umma) inasema nini. Ukiangalia ndani ya vyama kuna watu ambao hawakuwa wametarajiwa kuong'olewa, lakini wameangushwa kwenye kura za maoni wakati wa mchakato wa wabunge," alifafanua.
"Kura za maoni ndani ya vyama zimeonyesha public inasema nini. Kuna mwamko mkubwa kwa wapigakura ambao tumeona si ndani ya chama tawala pekee ambako kuna majina yasiyotarajiwa yaliangushwa, bali hata ndani ya vyama vya upinzani kulikuwa na mwamko mkubwa."
Wabunge wengi vigogo ndani ya CCM, akiwemo mwanasiasa mkongwe John Malecela, waliangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM, sambamba na mawaziri watano.
Visiwani Zanzibar, zaidi ya wawakilishi 10 wanaomaliza muda wao walianguka kwenye kura za maoni za CUF, huku Chadema ikikumbwa na mapambano kwenye baadhi ya majimbo na uchaguzi wa wabunge wa viti maalum kiasi cha uongozi kuamua kusitisha mchakato huo.
"Umeona uchaguzi wa wabunge wa viti maalum wa Chadema umeahirishwa; hii yote ni mwamko kwa wapigakura kuanzia ndani ya vyama," alisema Tendwa.
Tendwa alisema sababu ya tatu ni kuwepo mabadiliko ndani ya chama tawala ambayo yamesababisha baadhi ya makada kwenda vyama vya upinzani kwa wingi.Alieleza kuwa zamani haikuwa rahisi kuona makada kutoka chama hicho tawala wakikihama na kukimbilia upinzani kama ilivyo sasa hivi.
"Hiki si kitu ambacho ni cha kawaida sana. Hivi sasa kuna makada wa CCM wanaamua kwenda upinzani. Zamani hii haikuwa rahisi sana au kwa kiasi kama cha safari hii," alisema.
Waziri wa zamani, Arcado Ntagazwa, mbunge wa siku nyingi wa Maswa, John Shibuda, mbunge wa kwanza wa Jimbo la Njombe Magharibi, Thomas Nyimbo na mbunge wa zamani wa Mlalo, Charles Kagonji ni miongoni mwa vigogo waliohamia Chadema baada ya kumalizika kwa kura za maoni wakifuatwa na wanachama wanaowaunga mkono.
Mbunge wa zamani wa Kishapu, Fred Mpendazoe aliihama CCM kabla ya Mkutano wa Tisa wa Bunge kumalizika na kujiunga na chama kipya cha CCJ kabla ya kutua Chadema.
Wengine ni Sijapata Nkayamba na Omary Likwelilo maarufu kama Dunia ambao wamehamia CUF pia wakiwa na wanachama wengine wanaowaunga mkono.
"Hayo yote ni changamoto na ishara kwamba kunaweza kuwepo na mabadiliko makubwa katika ukuaji wa demokrasia. Hilo linaonyesha kuwa wananchi wana uhuru na haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa," alisema.
Tendwa alitaja sababu ya nne kuwa ni kuwepo mazingira huru ya kidemokrasi ambayo yanafanya vyama vya upinzani na tawala kufanya kampeni zao kwa uhuru, haki na usawa.
Alidai kuwa hakuna ukandamizaji wowote wa haki za vyama kwa kuwa viko huru kunadi sera zao, bila kuingiliwa wala kusumbuliwa na upande wowote uwe wa chama tawala au upande wa vyombo vya dola.
"Nchi ina mazingira mazuri mno ya kidemokrasia; hakuna chama kinazuiwa kunadi sera zake. Vyama vina uhuru mpana kunadi sera zao kwa wapigakura na hakuna mtu anaweza kuwasumbua."
Aliongeza kwamba mwaka 2005 alitabiri kuwa upinzani ungepata viti vingi, lakini hilo halikuwezekana kwa sababu muda wa kampeni uliongezeka baada ya kufariki kwa mgombea mwenza wa Chadema.
Akiwa Hoteli ya Hill Top mkoani Kigoma, Tendwa aliitisha mkutano na waandishi baada ya ziara yake katika maeneo mbalimbali nchini na kueleza kuwa upinzani ungeweza kupata viti hadi 60 lakini uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na kifo mgombea huyo.
Viti vya majimbo vinatarajiwa kufikia 245 wakati vya viti maalum na uteuzi vikifanya jumla ya wabunge wote kufikia 315.
Source.
Tendwa atabiri viti 100 vya ubunge kwenda upinzani