SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF) na
Shirikisho la Soka nchini (TFF), limeitaka
Yanga kulipa fidia ya gharama za mchezo
wake na TP Mazembe Sh milioni 530.
CAF na TFF imefikia hatua hiyo baada ya
Yanga kufuta kiingilio katika mchezo wao
huo wa makundi wa Kombe la Shirikisho
Afrika unaotarajiwa kuchezwa leo kwenye
Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na sasa
mashabiki wataingia bure.
Katika kikao chao cha jana kilichofanyika
kwenye hoteli ya Coral Beach jijini na
kukutanisha maofisa wa CAF, uongozi wa
TFF, Polisi, Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo na viongozi wa Yanga
wakiongozwa na Katibu mkuu wa klabu
hiyo, Baraka Deusdetit wametakiwa kulipa
kiasi hicho cha fedha kama gharama za
mchezo.
Makato katika mchezo huo wa hatua ya
makundi Kombe la Shirikisho asilimia 15
ya fedha hizo zitaenda CAF, asilimia 15
nyingine gharama ya uwanja, TFF asilimia
tano, Baraza la Michezo la Taifa (BMT),
asilimia 10, na Chama cha soka Dar es
Salaam (DRFA) asilimia tano.
Tayari Yanga ilikuwa imechapisha tiketi
31,000 ambazo zingeuzwa kwa Sh7,000
ambazo zingeingiza Sh 217,000,000 huku
zile za Sh 25,000 zilikuwa zimechapishwa
tiketi 8,200 zingeingiza Sh milioni 205
huku VIP zilikuwa tiketi 5,000 ambazo
zingeingiza Sh milioni 150 jumla ya fedha
zote ambazo zingepatikana katika
mchezo huo ni Sh milioni 572.
Pia Yanga wametakiwa kuingiza
mashabiki wasiozidi 40,000 wakizidi
kiwango hicho mchezo huo utafutwa na
Yanga watalazimika kuwajibishwa.