Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Kanda ya Ziwa imewakamata wafanyabiashara wawili mjini Bariadi, mkoani Simiyu, kwa tuhuma za kuuza mbolea za ruzuku kwa bei tofauti na ile iliyoelekezwa na Serikali, hatua inayolenga kudhibiti vitendo vinavyowaumiza wakulima na kulinda lengo la ruzuku.
Akizungumza ofisini kwake, Meneja wa TFRA Kanda ya Ziwa, Michael Sanga, amesema wafanyabiashara hao walikamatwa baada ya maafisa wa mamlaka hiyo kufanya operesheni maalumu ya mtego iliyofanikisha kuwabaini wakiuza mbolea hizo kwa bei isiyo rasmi.
Aidha, amewatahadharisha wafanyabiashara wote wa pembejeo za kilimo kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia biashara ya mbolea, huku akiwahimiza wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini ukiukwaji wa bei elekezi au changamoto nyingine zinazohusu upatikanaji wa mbolea za ruzuku.
TFRA imesisitiza kuwa haitamvumilia mfanyabiashara yeyote atakayekiuka utaratibu wa uuzaji wa mbolea za ruzuku, ikieleza kuwa ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa utasaidia kuhakikisha ruzuku ya Serikali inanufaisha wakulima waliokusudiwa na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.