Siri ya Buzwagi
Wapinzani kuuanika kesho
na Mwandishi Wetu
MKATABA wa uchimbaji wa madini wa Buzwagi uliozusha mabishano makali wakati wa kikao kilichopita cha Bunge hata kusababisha kusimamishwa kwa uwakilishi wa Kabwe Zitto, kwa miezi mitano, umevuja.
Kuvuja kwa mkataba huo uliosainiwa Februari 17 mwaka huu, hatimaye kumeweza kufichuka kwa siri ya kile ambacho kilishindwa kubainika kabla na baada ya Zitto kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kumtuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kwa kulidanganya Bunge, hatua ambayo iligeuka na kumtia matatizoni mbunge huyo mdogo kuliko wote wa kuchaguliwa.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kambi ya upinzani ambayo imeushikia bango mkataba huo zinaeleza kuwa, kuvuja kwa mkataba huo kumewawezesha kubaini mapungufu makubwa yaliyomo ndani ya mkataba huo ambayo kiongozi mmoja wa juu wa upinzani ameyaeleza kuwa hatua muhimu katika kuthibitisha mkweli kati yao na serikali.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari kamati maalumu ya kambi ya upinzani inayohusisha watu wenye taaluma mbalimbali wakiwamo, wachumi na wanasheria, wameishaupitia mkataba huo mzima wenye kurasa 24, uliosainiwa na Waziri Karamagi kwa upande wa serikali na Gareth Taylor wa Pangea Minerals Ltd, ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick Gold Corporation ya Canada.
Katika kufanikisha malengo yao, wapinzani kupitia katika kamati yao hiyo mahususi, imeainisha maeneo kadhaa yenye mapungufu makubwa yaliyo katika maeneo sita, ambayo yanaonyesha namna mkataba huo unavyoliumiza taifa zaidi ya kulinufaisha.
Moja ya mapungufu ya haraka haraka yanayoonekana ni ukweli kwamba, wawekezaji hao katika kipindi chote cha mkataba hawatalazimika kulipa kodi kwa halmashauri na serikali kuu, ambazo zinazidi viwango vya sehemu nyingine nchini na ambazo zimetokana na faida, mauzo au uzalishaji unaotokana na uchimbaji madini.
Pamoja na ukweli kwamba wawekezaji hao watalipa dola za Marekani zisizozidi 200,000 kwa mwaka kwa halmashauri, na serikali kuu hawatalipa kodi zinazotokana na thamani ya ardhi inayotumika kama mgodi, kwa miundombinu ya uchimbaji madini au mitambo.
Miongoni mwa maeneo yaliyoainishwa kuwa yenye mapungufu yasiyozingatia masilahi ya taifa na ambayo yanaonekana kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa taifa ni eneo la kodi ambalo linaonekana kuwa pungufu kuliko ilivyobainishwa na Waziri Karamagi bungeni.
Aidha, eneo jingine lililobainishwa na kamati hiyo mahususi, imebainisha kuwapo kwa upungufu mkubwa katika mkataba huo unaoonyesha kuwa, kiwango cha kodi kimekadiriwa kuwa kitakuwa kisicho na mabadiliko makubwa katika kipindi chote cha mkataba.
Kwa mujibu wa mkataba huo, ambao gazeti hili limefanikiwa kuuona, mafao mengi ambayo Karamagi aliyataja kuwa nchi itajipatia katika maelezo yake bungeni hayaonekani, hali ambayo inatarajiwa kuwa ajenda kuu ya kuishambulia serikali katika mkutano wao kesho.
Wapinzani katika uchambuzi wao huo wamebaini kuwa, vifungu vya mkataba huo vinaonyesha kwamba nje ya malipo ya mrahaba na kodi ya zuio, Serikali ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kahama unakojengwa mgodi huo, itakuwa inalipwa jumla ya dola za Marekani 583,980 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa mkataba huo, baadhi ya kodi zitakazolipwa na Pangea Minerals, ni pamoja na asilimia tatu ya thamani ya madini baada ya kuondoa gharama za uzalishaji kama mrahaba kwa madini yote yatakayochimbwa eneo la Buzwagi isipokuwa almasi, ambayo mrahaba wake utakuwa asilimia tano.
Aidha, kampuni italipa ushuru wa stempu kama ulivyoainishwa na Sheria ya Ushuru wa Stempu Na. 20 ya Mwaka 1972 kuanzia tarehe ya kuanza kwa mkataba wa Buzwagi.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa Pangea Minerals kutolipa hata senti moja kama ushuru wa stempu, kwani kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Ushuru wa Stempu kimetoa angalizo kwamba hakuna ushuru wowote utakaolipwa kutokana na waraka wowote uliosainiwa na, au kwa niaba au kwa taarifa ya Serikali. Ambapo kama kifungu hiki kisingekuwapo, basi Serikali ingekuwa na wajibu wa kulipa ushuru huo kuhusiana na waraka huo.
Pangea italipa pia dola za Marekani 125,000 kwa ajili ya Mfuko wa Uwezeshwaji zitakazolipwa kila tarehe 31 Desemba ya kila mwaka kuanzia mwaka wa uzalishaji.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Mwaka wa Uzalishaji umetafsiriwa kuwa ni kipindi ambapo uzalishaji wa dhahabu safi au isiyosafishwa utafikia kiasi cha wakia 20,000, hivyo Pangea Minerals haiwajibiki kulipa kodi ya Mfuko wa Uwezeshwaji iwapo uzalishaji wa dhahabu hautafikia wakia 20,000 kwa mwaka.
Kwa ujumla, vipengele vya mkataba huo vinaonyesha kuwa kiwango cha jumla ya kodi zote ambazo Pangea Minerals italipa kwa halmashauri za wilaya au serikali za mitaa kwa ujumla hakitazidi dola za Marekani 200,000 kwa mwaka, tofauti na ilivyoelezwa na Karamagi bungeni.
Aidha, kampuni haitalipa kodi za halmashauri na/au serikali za mitaa ambazo zinazidi viwango vya sehemu nyingine za Tanzania na ambazo zimetokana na faida, mauzo au uzalishaji unaotokana na uchimbaji madini au ambazo zimetokana na thamani ya ardhi inayotumika kama mgodi, kwa miundombinu ya uchimbaji madini au mitambo.
Kwa mujibu wa mkataba huo, kampuni hiyo haitawajibika kulipa ushuru, ada au mchango wowote wa lazima zaidi ya vile ilivyoelezwa katika aya ya (iv) ya mkataba huo, isipokuwa kwa kodi, ushuru, ada au michango midogo midogo ambayo kwa pamoja haitazidi dola za Marekani 10,000 kwa mwaka.
Kampuni hiyo pia haitalipa malipo yatozwayo chini ya Sheria ya Madini au kanuni zake yanayozidi dola za Marekani 2,000 kwa kilometa ya mraba kwa mwaka.
Wapinzani wamebaini pia kwamba, Pangea haitalipa kodi ya matumizi ya barabara iliyowekwa na Sheria ya Kodi za Mafuta na Barabara ya mwaka 1985 itakayozidi dola za Marekani 200,000 kwa mwaka na kodi yoyote ya mauzo, matumizi au ongezeko la thamani, isipokuwa kama ilivyowekwa chini ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 1997.
Kama hiyo haitoshi, imebainika pia kwamba, Pangea Minerals italipa kodi ya zuio (withholding tax) kutokana na malipo kwa watu wengine kama inavyotakiwa na sheria husika, isipokuwa kampuni haitawajibika kushikilia kodi kwa kiwango chochote kutokana na malipo ya mkopo au deni la riba inayotakiwa kulipwa kwa fedha za kigeni kwa ajili ya mikopo, ikiwa ni pamoja na mikopo ya washirika wake, iliyokopwa nje ya Tanzania kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini.
Pia mkataba unaonyesha kuwa Pangea Minerals itaruhusiwa kukata asilimia 80 ya mtaji uliotumika kwa mwaka huo, na baada ya hapo itakata asilimia 50 kwa mwaka, isipokuwa tu kwamba Serikali ya Tanzania itatakiwa kufanya marekebisho ya sheria ili kuyafanya makato haya yakubalike chini ya sheria za Tanzania.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo ya sheria, kifungu hiki cha mkataba kina maana kwamba endapo serikali haitafanya marekebisho ya sheria husika, basi Pangea Minerals itaendelea kukata asilimia mia moja ya mtaji uliotumika kwa mwaka wa kwanza.
Kwamba, mradi huo unaweza kuipatia Tanzania mamilioni hayo ya fedha, inatia shaka, kwa sababu kwa mujibu wa maelezo ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Serikali ya Tanzania imepokea dola za Marekani milioni 78 tu kama mrahaba na kodi nyingine kutoka kwa migodi yote sita ya dhahabu ambayo inafanya kazi hadi sasa.
Kwa kiwango hicho, Buzwagi ambao Waziri Karamagi mwenyewe aliuita kama Marginal Mine, yaani Mgodi Mdogo ni wazi kwamba matarajio ya serikali kuhusu manufaa ya Mgodi wa Buzwagi hayana msingi wowote katika hali halisi.
Aidha, mkataba huo una kipengele ambacho kinamlazimisha Waziri Karamagi kutoa leseni Maalumu ya Uchimbaji kwa Pangea Minerals ya muda wa kuanzia, wa miaka ishirini na mitano (25).
Mkataba unataka leseni hiyo kutolewa haraka iwezekanavyo na kwa vyovyote vile ndani ya muda usiozidi siku sitini (60) tangu Pangea Minerals kuwasilisha maombi yao ya Leseni Maalumu ya Uchimbaji.
Aidha, mkataba unaipa uhuru Pangea Minerals kuongeza muda wa leseni hiyo kwa masharti hayo hayo kwa miaka mingine ishirini na mitano (25).
Mkataba huo unairuhusu pia kampuni hiyo kuhamisha rasilimali ya taifa kwenda nje ya nchi (capital flight) kwa muda wote wa uhai wa mkataba.
Kuhusu manunuzi ya bidhaa na huduma, tofauti na alivyosema Karamagi, kifungu cha 7 cha mkataba kinasema: Kampuni itatoa upendeleo wa kununua bidhaa na huduma zilizoko Tanzania, ilimradi bidhaa na huduma hizo zina ubora wa kimataifa, zinapatikana kwa wakati na idadi inayotakiwa na zinauzwa kwa bei ya ushindani zinapofikishwa Tanzania."
Vile vile kampuni kwa kushauriana na waziri itaweka utaratibu wa zabuni utakaowawezesha makandarasi kushindania zabuni hizo kwa kuangalia mazingira ya Tanzania, hakuna chochote katika kifungu hiki cha mkataba kinachoelezea kiasi cha fedha kitakachotumika katika kununua bidhaa na huduma ndani ya nchi na kama bidhaa au huduma zenyewe zitazalishwa Tanzania au zimenunuliwa nje kwa matumizi ya ndani.
Kwa upande mwingine, mkataba huo unaibana serikali kuhakikisha kwamba vifungu vya sheria vinavyohusu manufaa, haki na wajibu wa Kampuni na/au wanahisa wa kampuni hiyo, hazibadilishwi wakati wowote wa uhai wa mkataba.
Mkataba unairuhusu Pangea Minerals kuingiza Tanzania wafanyakazi wa nje, mashine, mitambo, magari ya usafirishaji na vifaa vingine muhimu kwa ajili ya ujenzi wa mgodi na uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini.
Kuhusu sheria itakayotumika, mkataba huo pamoja na kutambua sherisa za Tanzania, una kipengele kinachoongeza; na taratibu za sheria za kimataifa zinazohusika."
Jambo hili limetiliwa nguvu zaidi na kifungu cha 13 cha mkataba kinachoamrisha kwamba mgogoro wowote utatatuliwa kwa upatanishi kufuatana na Kanuni za Upatanishi za Tume ya Umoja wa Mataifa ya Sheria za Kimataifa za Biashara (UNCITRAL)."
Pili, mahakama za Tanzania hazina mamlaka ya kusikiliza na/au kutatua migogoro chini ya mkataba huu, kwani jukumu hilo imepewa Mahakama ya Upatanishi ya Kimataifa ya London, kufuatana na kanuni za upatanishi za UNCITRAL, zitakazokuwa zinatumika wakati wa kusaini mkataba huu.