Hiza, Akwilombe watumika kummaliza Zitto
Na Patrick Mabula, Kahama
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewatumia wanasiasa waliojiunga kutoka Upinzani kuzima hoja za mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, kuhusu mgodi wa Buzwagi wilayani hapa, kuhusu mkataba wa madini kusainiwa Uingereza.
Wakihutubia mkutano wa hadhara juzi wanasiasa hao Bw. Tambwe Hiza aliyetoka CUF na Bw. Shaibu Akwilombe aliyetoka CHADEMA, walisema Bw.Zitto alitunga uongo na anatafuta umaarufu wa kisiasa.
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusufu Makamba, aliyeanza kuhutubia, aliwaeleza wananchi wa hapa kuwa madai ya Bw. Zitto ni ya uongo yenye lengo la kukwamisha uwekezaji na maendeleo ya wananchi wilayani hapa.
Alisema wananchi wanapaswa kumpuuza, kwani ana lengo la kukwamisha ajira ya vijana wapatao 600 watakaoajiriwa na mwekezaji wa Kampuni ya Barrick wakati mgodi wa Buzwagi utakapoanza kazi.
Bw. Makamba alisema anashangazwa na baadhi ya wananchi wa Kanda ya Ziwa kumpokea Bw. Zitto kama shujaa wakati hoja zake zilikuwa si za kweli na kuwataka watu wa hapa, atakapokuja wasimpokee kwa namna hiyo wakati wa ziara yake.
Bw. Akwilombe alisema yeye anamfahamu vizuri Bw. Zitto kuliko watu wa hapa, na kwamba hoja zake zilikuwa za kutunga ili kutafuta umaarufu, kwa kuwa hakuna sheria yoyote inayozuia mkataba kusainiwa nje ya nchi.
Alidai yeye akiwa CHADEMA walipanga mbinu za kutengeneza uongo ili wapate umaarufu na kuongeza kuwa hata mkataba wa Reli yaTAZARA ulisainiwa China, lakini reli ilijengwa nchini, hivyo akawataka wananchi wampuuze Bw. Zitto.
Bw. Akwilombe alisema akija kuhutubia masuala ya mgodi wa Buzwagi, kama anavyohutubia sehemu zingine za Kanda ya Ziwa na kupokewa kishujaa wampuuze.
Naye Bw. Hiza alisema CHADEMA wanatumia kigezo cha mgogoro wa mkataba wa Buzwagi kuzunguka nchi nzima kutafuta umaarufu na kujipatia wanachama.
Alisema lengo kuu la Bw. Zitto kuzusha hoja hiyo bungeni ni kutaka iundwe tume ya kuchunguza utiwaji saini mkataba huo ili yeye awe Mwenyekiti wa Tume hiyo ili ajipatie posho wakati wa uchunguzi.
Alisema mbunge anapoanzisha hoja ikifanikiwa kuundiwa tume yeye anakuwa ndiye Mwenyekiti, hivyo mgogoro wa Buzwagi lengo lake lilikuwa kutafuta fedha za Tume hiyo ambayo ingefanya uchunguzi hadi Uingereza ulikofungiwa mkataba.
Bw. Hiza alisema kama Tume ya Malima ilitumia sh. milioni 100 uchunguzi wa uwekaji mkataba wa Buzwagi ungegharimu zaidi ya kiasi cha pesa, kutokana na uchunguzi wake kufika Uingereza.
Alisema mkataba uliowekwa ni halali na taratibu zote zilifuata sheria za nchi na kuwataka wananchi wasiyumbishwe na hoja za wapinzani ambao alidai yeye anawafahamu.