Caster Semenya Kushoto alikuwa akivaa suruali siku zote wakati alipokuwa shuleni tofauti na wanafunzi wenzake wa kike Monday, August 24, 2009 4:08 AM
Zengwe la utata wa jinsia ya mwanariadha wa kike wa Afrika Kusini, Caster Semenya limezidi kufukuta na kupelekea baraza la michezo la Afrika Kusini kuamua kulifikisha suala hilo umoja wa mataifa. Mwenyeketi wa baraza la michezo la bunge la Afrika Kusini, Butana Komphela ambaye pia ni mbunge wa chama tawala cha ANC amesema kwamba baraza lake liko njiani kupeleka malalamiko umoja wa mataifa dhidi ya shirikisho la kimataifa la riadha duniani (IAAF) kwa kumfanyia unyanyasaji mwanariadha wao wa kike Caster Semenya na kuvunja haki zake za msingi.
"Kwakuwa Semanya ni mweusi na amewaacha mbali wapinzani wake toka ulaya ndio ameanzishiwa zengwe hili la kufanyiwa vipimo vya jinsia yake" alisema Komphela.
"Kuna wanariadha wengi wa kike wazungu ambao walishiriki kwenye mashindano haya ambao wanaonekana kama wanaume lakini hakuna chochote kilichosemwa, hawawezi kuwafanyia hivyo wanariadha wao" alisema Komphela.
Siku ya ijumaa Leonard Chuene, mwenyekiti wa shirikisho la riadha nchini Afrika Kusini aliliambia gazeti la Saturday Star la Afrika Kusini kwamba anaachia ngazi nafasi yake ya uwakilishi kwenye IAAF ili aweze kupambana nao vizuri juu ya uamuzi wa kuchunguza jinsia ya Semenya.
"Watoto hawachukuliwi na kupelekwa maabara ili kujua jinsia zao. Huwa tunaangalia sehemu moja tu ya mwili na huwa tunajua jinsia yake, kwanini afanyiwe hivi?".
"Hii ni kuiaibisha nchi yetu, je tutaruhusu watu wafanye maamuzi wanayotaka kwa waafrika kwasababu tupo kwenye nchi zao za ulaya? nasema hapana. Hakuna vipimo zaidi atakavyofanyiwa mtoto huyu. Hakuna mtu atakayemgusa mpaka atakaporudi nyumbani".
Hata hivyo msemaji wa IAAF, Nick Davies, alisema kwamba shirikisho la riadha halisemi kwamba Semanya ameongopa kuhusiana na jinsia yake bali uchunguzi unafanyika ili kuthibitisha jinsia yake. Anaweza akaendelea kukimbia wakati tunasubiria majibu ya vipimo" alisema Chuene.
Semenya aliingia kwenye zengwe la kujadiliwa jinsia yake baada ya kunyakua medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 800 za wanawake kwa kuwaacha kwa mbali sana washiriki wenzake. Aliweka rekodi ya muda bora mwaka huu.
Misuli yake iliyojengeka, sauti nzito na vinyweleo vyake vya usoni vilitumiwa kama vielelezo vya kutia shaka jinsia yake.
Semenya ambaye hakuwahi kuvaa sketi alipokuwa shuleni kama wanafunzi wenzake wa kike, hupendelea kuvaa na kujiweka kama mwanaume na alikua akicheza michezo yote ya kiume kama vile soka, mieleka, ndondi, karate n.k.
Semenya alikataa kwenda kchukua medali yake ya dhahabu baada ya kushinda mbio hizo kufuatia maneno mengi juu ya jinsia yake lakini viongozi wa Afrika Kusini walimsihi sana aende kuchukua medali yake ndipo alipokubali.
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kumwandalia mapokezi ya nguvu Semenya atakaporudi Afrika Kusini wiki hii.
http://www.nifahamishe.com/NewsDetails.aspx?NewsId=2896822&&Cat=2