ALICHOFANYA NAZIR MUSTAFA KARAMAGI KATIKA MKATABA WA BUZWAGI
Nazir Mustafa Karamagi ni Waziri wa sasa wa Nishati na Madini. Aliingia kwa mara ya kwanza katika Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete kama Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko. Lakini kufuatia Kashfa ya Umeme wa Richmond iliyomwondoa Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo Dr. Ibrahim Msabaha na Naibu wake Lau Masha, Mheshimiwa Karamagi alihamishiwa Wizara ya Nishati na Madini. Katika kipindi cha karibu mwaka mmoja ambao Mheshimiwa Karamagi ameshikilia madaraka yake ya sasa amehujumu taifa la Tanzania kwa kusaini mkataba wa ujenzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga na kampuni ya Pangea Minerals Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick Gold Corporation ya Canada. Mkataba huo ulisainiwa Churchill Hotel, London, Uingereza tarehe 17 Februari 2007. Kwa vile kusainiwa kwa Mkataba huo ndio ulikuwa chimbuko la hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge iliyopelekea Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mheshimiwa Zitto Z. Kabwe kusimamishwa kufanya shughuli za Bunge kwa miezi mitano, ni vema madhara na/au manufaa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya Mkataba huo kwa Tanzania yachunguzwe kwa makini kama ifuatavyo:
I. MUDA WA MKATABA
(i) Kwamba Waziri Karamagi atatoa Leseni Maalum ya Uchimbaji kwa Pangea Minerals ya muda wa kuanzia wa miaka ishirini na tano (25). Leseni hiyo itatolewa haraka iwezekanavyo na kwa vyovyote vile ndani ya muda usiozidi siku sitini (60) tangu Pangea Minerals kuwasilisha maombi yao ya Leseni Maalum ys Uchimbaji. Aidha, Pangea Minerals
watakuwa na uhuru wa kuongeza muda wa Leseni hiyo kwa masharti hayo hayo kwa miaka mingine ishirini na tano (25). Na endapo muda huo wa nyongeza ukiisha na Pangea Minerals wakaomba kuongezewa muda zaidi,
basi iwapo Waziri ataona ni kwa maslahi ya taifa kuwaongezea muda kama walivyoomba atawaongezea muda wa ziada atakaoona unafaa. Kwa masharti haya ya mkataba, Pangea Minerals wana haki ya kuendelea kuchimba dhahabu kwa miaka hamsini au zaidi kufuatana na mahitaji yao na matakwa ya Waziri wa Nishati na Madini na kwa masharti yale yale yaliyowekwa siku ya kusaini mkataba;
II. MAPATO YA SERIKALI
Mkataba wa Buzwagi unadai kwamba Kampuni inachukulia suala la kutobadilika badilika kwa kodi na sheria za fedha za Tanzania kama sharti la msingi katika uwekezaji wake kwenye Mgodi na kwamba Kampuni itakuwa na uhakika kwamba kodi na utaratibu wa kifedha ulivyo wakati wa kusaini Mkataba utaendelea kuwa hivyo kwa Kampuni wakati wote wa uhai wa Mradi wa Buzwagi. Katika kuhakikisha suala hili, Mkataba huu umeweka masharti yafuatayo kuhusiana na masuala ya kodi na/au ya kifedha:
(i) Kwamba Pangea Minerals watalipa kwa Serikali kodi zifuatazo:
(a) Asilimia 3 (3%) thamani ya madini baada ya kuondoa gharama za uzalishaji kama mrahaba kwa madini yote yatakayochimbwa eneo la Buzwagi isipokuwa almasi ambayo mrahaba wake utakuwa asilimia 5 (5%) ya thamani ya almasi hiyo baada ya kuondoa gharama za uzalishaji;
(b) Ushuru wa stempu (stamp duty) kama ulivyoainishwa na Sheria ya Ushuru wa Stempu Na. 20 ya Mwaka 1972 kuanzia tarehe ya kuanza kwa mkataba wa Buzwagi. Hata hivyo, kuna uwezekano wa Pangea Minerals kutolipa hata senti moja kama ushuru wa stempu kwani kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Ushuru wa Stempu kimetoa angalizo kwamba hakuna ushuru wowote utakaolipwa kutokana na waraka (instrument) wowote uliosainiwa na, au kwa niaba au kwa taarifa ya Serikali ambapo kama kifungu hiki kisingekuwapo, basi Serikali ingekuwa na wajibu wa kulipa ushuru huo kuhusiana na waraka huo. Neno instrument limetafsiriwa kuwa linajumuisha kila nyaraka ambayo kwayo haki au deni/wajibu l/imetengenezwa au imedaiwa kutengenezwa au kuhamishwa, kupunguzwa, kuongezwa, kufutwa au kurekodiwa. Kwa tafsiri hii, ni wazi kwamba Mkataba wa Buzwagi ni waraka (instrument) ambao kwayo haki na wajibu wa Serikali na Pangea Minerals imetengenezwa, kuhamishwa na/au kurekodiwa;
(c) Dola za Marekani laki moja na ishirini na tano elfu (US$ 125,000) kwa ajili ya Mfuko wa Uwezeshwaji (Empowerment Fund) zitakazolipwa kila tarehe 31 Desemba ya kila mwaka kuanzia mwaka wa uzalishaji. Ni muhimu kuelewa hapa kwamba Mwaka wa Uzalishaji umetafsiriwa katika mkataba huu kuwa ni kipindi ambapo uzalishaji wa dhahabu safi au isiyosafishwa utafikia kiasi cha wakia 20,000. Kwa maana nyingine Pangea Minerals hawawajibiki kulipa kodi ya Mfuko wa Uwezeshwaji iwapo uzalishaji wa dhahabu hautafikia wakia 20,000 kwa mwaka;
(ii) Kwamba kodi yoyote, ushuru wowote, ada yoyote au malipo mengine ambayo Kampuni, wenye hisa wake, washirika au wadeni wake watatakiwa kulipa kutokana na mapato, ikiwa ni pamoja na mapato ya gawio, yatokanayo na uchimbaji madini unaofanyika chini ya Leseni Maalum ya Uchimbaji vitalipwa kuanzia tarehe ya mkataba kufuatana na matakwa ya Sheria ya Kodi y Mapato ya mwaka 2004 na Sheria ya Ushuru wa Forodha ya mwaka 1976. Ni muhimu kuelewa hapa kwamba Sheria hizo mbili zilifanyiwa marekebisho makubwa na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria za Fedha Na. 27 ya mwaka 1997. Chini ya marekebisho hayo kodi, ushuru au ada zinazozungumziwa katika kifungu hiki cha Mkataba ziliondolewa au kupunguzwa kwa kiasi kikubwa au kufanywa kuwa tegemezi wa wakati makampuni ya madini yatakapoanza kupata na/au kutangaza faida. Kwa maana nyingine, Serikali inaweza isipate fedha yoyote kutokana na kifungu hiki cha Mkataba wa Buzwagi;
(iii) Kwamba kiwango cha jumla ya kodi zote ambazo Pangea Minerals italipa kwa halmashauri za wilaya au serikali za mitaa kwa ujumla hakitazidi Dola za Marekani laki mbili US$ 200,000) kwa mwaka. Aidha Kampuni haitalipa kodi za halmashauri na/au serikali za mitaa:
(a) ambazo zinazidi viwango vya sehemu nyingine za Tanzania;
(b) ambazo zimetokana na faida, mauzo au uzalishaji unaotokana na uchimbaji madini; au
(c) ambazo zimetokana na thamani ya ardhi inayotumika kama mgodi, kwa miundombinu ya uchimbaji madini au mitambo;
(iv) Kwamba Pangea Minerals haitawajibika kulipa kodi zifuatazo kutokana na shughuli zake za uchimbaji madini:
(a) Ushuru, ada au mchango wowote wa lazima zaidi ya vile ilivyoelezwa katika aya ya (iv) isipokuwa kwa kodi, ushuru, ada au michango midogo midogo ambayo kwa pamoja haitazidi Dola za Marekani elfu kumi (US$ 10,000) kwa mwaka;
(b) Malipo yatozwayo chini ya Sheria ya Madini au kanuni zake yanayozidi Dola za Marekani elfu mbili (US$ 2,000) kwa kilometa ya mraba kwa mwaka. Kwa maana hiyo, kodi ya kiwanja inayotakiwa kulipwa kwa eneo lote la Mkataba wa Buzwagi lenye ukubwa wa kilometa za 24.49 ni Dola za Marekani elfu arobaini na nane mia tisa na themanini (US$ 48,980) kwa mwaka;
(c) Kodi ya matumizi ya barabara iliyowekwa na Sheria ya Kodi za Mafuta na Barabara ya mwaka 1985 itakayozidi Dola za Marekani laki mbili (US$ 200,000) kwa mwaka;
(d) Kodi yoyote ya mauzo, matumizi au ongezeko la thamani isipokuwa kama ilivyowekwa chini ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 1997. Hapa vile vile ni muhimu kuelewa kwamba Sheria Na. 27 ya mwaka iliyofanya marekebisho ya sheria mbali mbali za fedha iliondoa kabisa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa mauzo ya madini yote yanayouzwa nje ya Tanzania kama dhahabu au almasi, n.k. Ndio maana kifungu hiki cha Mkataba wa Buzwagi kimesema wazi kwamba Pangea Minerals ina haki ya kunufaika na nafuu za VAT zilizopo katika Nyongeza ya Tatu ya Sheria ya VAT kuanzia tarehe ya Mkataba;
(v) Kwamba Pangea Minerals italipa kodi ya zuio (withholding tax) kutokana na malipo kwa watu wengine kama inavyotakiwa na sheria husika, isipokuwa Kampuni haitawajibika kushikilia kodi:
(a) Kwa kiwango chochote kutokana na malipo ya mkopo au deni la riba inayotakiwa kulipwa kwa fedha za kigeni kwa ajili ya mikopo, ikiwa ni pamoja na mikopo ya washirika wake, iliyokopwa nje ya Tanzania kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini. Kwa maana nyingine, malipo ya mikopo mikubwa ambayo makampuni ya madini yamekuwa yanadai kulipa kwa wadeni wao wa nje na kwa hiyo kushindwa kupata faida ya kulipa kodi ya mapato kwa Serikali ya Tanzania nayo haitalipiwa kodi ya zuio;
(b) Kwa kiwango chochote kinachozidi asilimia 5 ya malipo ya jumla kuhusiana na huduma za kiutaalamu au ada za menejimenti;
(vi) Pale ambapo asilimia 5 ya malipo ya jumla kwa ajili ya huduma za kiutaalamu au ada ya menejimenti inashikiliwa na Pangea Minerals imezuiliwa, kodi hiyo ya zuio itahesabika kuwa ni sawa na malipo yote ya kodi ya mapato inayotakiwa kulipwa na mtu anayetoa huduma za kiutaalamu au menejimenti. Maana ya kifungu hiki ni kuwawezesha watoa huduma za kiutaalamu au menejimenti kutolipa kodi ya mapato ambayo kisheria ni asilimia 30 ya mapato yao;
(vii) Kwamba Pangea Minerals itaruhusiwa kukata asilimia 80 ya mtaji uliotumika kwa mwaka uliotumika mtaji huo na baada ya hapo itakata asilimia 50 kwa mwaka isipokuwa tu kwamba Serikali ya Tanzania itatakiwa kufanya marekebisho ya sheria ili kuyafanya makato haya yakubalike chini ya sheria za Tanzania. Kifungu hiki cha Mkataba kina maana kwamba endapo Serikali haitafanya marekebisho ya Sheria husika, basi Pangea Minerals itaendelea kukata asilimia mia moja ya mtaji uliotumika kwa mwaka wa kwanza!
(viii) Kwamba mnunuzi wa madini yoyote yaliyochimbwa katika eneo la Mkataba hatalazimika kuzuia kiasi chochote kutoka katika bei ya mauzo.
Itakumbukwa kwamba wakati akijibu hoja ya Mheshimiwa Zitto Kabwe juu ya kuundwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza tuhuma zake dhidi ya kusainiwa kwa Mkataba wa Buzwagi, Waziri Karamagi aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano juu ya faida zifuatazo zinazotarajiwa kutokana na kusainiwa kwa Mkataba wa Buzwagi:
(a) Malipo ya mrahaba na kodi nyingine za kiasi cha Dola za Marekani milioni 198.9;
(b) Makato ya kodi ya mishahara ya wafanyakazi (pay as you earn) ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 50.3;
(c) Ujenzi wa laini na matumizi ya umeme ya Mgodi na maeneo yanayouzunguka ya Dola za Marekani milioni 30;
(d) Manunuzi ya huduma mbali mbali wakati wa kujenga miundo mbinu, mitambo na wakati wa uzalishaji ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 568.4;
(e) Jumla ya mapato yote yatakayoingia kwenye uchumi wa taifa katika kipindi cha uhai wa mgodi ni takriban Dola za Marekani milioni 818.3;
(f) Ajira 630 kwa Watanzania; kuongezeka kwa pato la taifa la fedha za kigeni; miundo mbinu ya kiuchumi na kijamii, n.k.
Hata hivyo, vifungu vilivyotajwa hapo juu vinaonyesha kwamba nje ya malipo ya mrahaba na kodi ya zuio, sana sana Serikali ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, itakuwa inalipwa jumla ya Dola za Marekani 583,980 kwa mwaka. Na kwa kuzingatia taarifa ya Waziri Karamagi kwamba Mgodi wa Buzwagi unatazamiwa kuwa na uhai wa miaka kumi, Serikali italipwa Dola za Marekani 5,839,800 nje ya mrahaba na kodi ya zuio kutokana na utajiri wa madini yote yaliyoko eneo la Buzwagi. Ukweli ni kwamba kiasi hicho kinaweza kupungua zaidi kwa kuangalia maelezo ya aya za ii(c), iv na v(a), (b) na (c) katika Waraka huu. Kuhusiana na madai ya Waziri Karamagi juu ya malipo ya mrahaba na kodi nyinginezo ya Dola za Marekani milioni 198.9, taarifa aliyoitoa Naibu wake William Ngeleja inaonyesha kwamba katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Serikali ya Tanzania imepokea Dola za Marekani milioni 78 tu kama mrahaba na kodi nyingine kutoka kwa migodi yote 6 ya dhahabu ambayo inafanya kazi hadi sasa. Kwa kiwango hicho, Buzwagi ambao Waziri Karamagi mwenyewe aliuita kama Marginal Mine, yaani Mgodi Mdogo ni wazi kwamba matarajio ya Serikali kuhusu manufaa ya Mgodi wa Buzwagi hayana msingi wowote katika hali halisi.
III. UHAMISHAJI WA RASILMALI YA TAIFA
Mkataba wa Buzwagi pia utakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa taifa kwa sababu utapelekea kuhamishwa kwa rasilmali ya taifa letu kwenda nje ya nchi (capital flight). Kwa muda wote wa uhai wa Mkataba, Pangea Minerals
ina haki na itaendelea kuwa na haki ya:
(a) Kubakisha nje ya nchi fedha za mauzo ya madini yanayomilikiwa na Kampuni na, ilimradi tu inatimiza wajibu wake wa kufanya malipo ndani ya Tanzania, Kampuni itakuwa na haki ya kuhamisha na/au kupeleka fedha hizo za mauzo ya madini popote inapotaka na kwa namna yoyote inayotaka;
(b) Kuingia katika makubaliano ya mikopo nje ya Tanzania inayohusu shughuli za uchimbaji na kubakisha nje ya nchi fedha zinazotokana na malipo ya mikopo hiyo;
(c) Kufungua na kuendesha akaunti za fedha za Tanzania au za kigeni endapo akaunti hizo zinatumika kwa ajili ya fedha zinazotokana na/au zinazohusu shughuli za uchimbaji madini;
(d) Kufungua na kuendesha akaunti za fedha za kigeni nje ya Tanzania zinazoweza kuingiziwa fedha bila kizuizi chochote na kuhamisha fedha hizo kwa uhuru na bila kizuizi na bila masharti ya kuzibadilisha fedha hizo kwa fedha za Tanzania na/au kurudisha Tanzania sehemu yoyote ya fedha hizo ilimradi tu Kampuni inaweza kutoa taarifa kwa Benki Kuu ya Tanzania juu matumizi ya akaunti hizo kuhusiana na shughuli za uchimbaji madini kama itakavyotakiwa na Benki Kuu;
(e) Kusafirisha na kuuza kwa wanunuzi wa nje madini yoyote na mazao yanayohusiana nayo yatakayochimbwa na/au kupatikana katika eneo la Mkataba.
Masharti yaliyotajwa katika (a), (b) na (d) yanahitaji vibali vya Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, kifungu cha 5.2 cha Mkataba kinailazimu Serikali ya Tanzania kumfanya Gavana wa Benki Kuu kuiandikia Kampuni barua itakayotoa vibali vyote vinavyotakiwa chini ya Mkataba huu ndani ya siku thelathini (30) kutoka tarehe ya kusainiwa kwa Mkataba. Na endapo vibali hivyo havitatolewa kitendo hicho hakitaathiri au kuzuia Kampuni kutumia haki zake au kufaidika na manufaa yaliyoko kwenye Mkataba huu! Vile vile Serikali na Waziri Karamagi wanatakiwa kuchukua hatua zote kuruhusu kitendo au kitu chochote cha kuhakikisha kwamba Kampuni inakuwa na haki na manufaa yaliyotolewa na Mkataba huu. Aidha taarifa zozote zinazotakiwa kuchapishwa ili kuhalalisha haki na manufaa ya Kampuni chini ya Mkataba huu zitachapishwa lakini kutochapishwa kwa taarifa hizo
hakutaizuia Kampuni kufaidika na manufaa yoyote yanayotarajiwa chini ya Mkataba huu. Kwa masharti yaliyotajwa katika sehemu hii, ni vigumu kuelewa na/au kukubali kauli ya Waziri Karamagi Bungeni kwamba Mgodi wa Buzwagi utaingiza mapato ya takriban Dola za Marekani milioni 818.3 kwenye uchumi wa taifa katika kipindi cha uhai wa mgodi huo!
IV. MANUNUZI YA BIDHAA NA HUDUMA
Katika hotuba yake Bungeni Waziri Karamagi alidai kwamba moja ya faida zitakazopatikana kwa kusainiwa Mkataba wa Buzwagi ni kununua huduma mbali mbali za wakati wa kujenga miundombinu mingine kwenda mgodini, ujenzi wa mitambo na wakati wa uzalishaji ambao unatarajiwa kugharimu takriban USD 568.4 milioni. Ushahidi wa Mkataba wenyewe unapingana na hoja ya Waziri Karamagi. Kwanza, kifungu cha 7 kinasema yafuatayo: Kampuni itatoa upendeleo wa kununua bidhaa na huduma zilizoko Tanzania ilimradi bidhaa na huduma hizo zina ubora wa kimataifa, zinapatikana kwa wakati na idadi inayotakiwa na zinauzwa kwa bei ya ushindani zinapofikishwa Tanzania. Vile vile Kampuni kwa kushauriana na Waziri itaweka utaratibu wa zabuni utakaowawezesha wakandarasi kushindania zabuni hizo kwa kuangalia mazingira ya Tanzania. Hakuna chochote katika kifungu hiki cha Mkataba kinachoelezea kiasi cha fedha kitakachotumika katika kununua bidhaa na huduma ndani ya nchi na kama bidhaa au huduma zenyewe zitazalishwa Tanzania au zimenunuliwa nje kwa matumizi ya ndani.
Pili, kifungu cha 8 cha Mkataba pia kinaitaka Kampuni na makandarasi wake kutumia bidhaa, vifaa na ugavi vilivyozalishwa ndani ya nchi kadri inavyowezekana wakati wa ujenzi na uendeshaji wa Mgodi na miundombinu yake. Hata hivyo, kifungu hiki kinatahadharisha, Kampuni na makandarasi wake watakuwa na haki ya kuagiza, bila kizuizi, vitu vyote vinavyohitajika kwa usanifu, ujenzi, kuweka mitambo na uendeshaji wa Mradi, ikiwa ni pamoja na mafuta, spea na sehemu za spea
ilimradi tu ushuru wowote unaohusu uingizaji mafuta, ikiwa ni pamoja na mchango wa ushuru wa barabara hautazidi Dola za Marekani 200,000. Aidha, ushuru wowote wa forodha utakaotozwa kwa bidhaa na/au vifaa vilivyoagizwa nje utakufuatana na matakwa ya Sheria ya Ushuru wa Forodha Na. 12 ya mwaka 1976 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Fedha Na. 27 ya mwaka 1997. Kama tulivyoonyesha, Sheria Na. 27 ilifuta masharti mbali mbali ya ulipaji wa ushuru wa forodha kwa ajili ya bidhaa na/au vifaa vinavyotumika au kuhusika na uchimbaji madini. Kifungu hiki pia kinapingana na hoja ya Waziri Karamagi juu ya manufaa yatakayotokana na manunuzi ya bidhaa na/au huduma.
V. UTAKATIFU WA MKATABA
Mkataba wa Buzwagi unaitaka Serikali kuhakikisha kwamba vifungu vya sheria vinavyohusu manufaa, haki na wajibu wa Kampuni na/au wanahisa wake hazibadilishwi wakati wowote wa uhai wa Mkataba:
(a) Muda wa Leseni Maalumu ya Uchimbaji au matumizi ya ardhi ya eneo la Mkataba ikiwa ni pamoja na matumizi ya ardhi yoyote iliyoko nje ya eneo la Mkataba kwa miundombinu, utunzaji au usafirishaji wa bidhaa zake;
(b) Kuingiza Tanzania wafanyakazi wa nje, mashine, mitambo, magari ya usafirishaji na vifaa vingine muhimu kwa ajili ya ujenzi wa Mgodi na uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini;
(c) Misamaha ya kodi, ushuru, ada na michango ya aina yoyote;
(d) Ulinzi wa kuhamisha mtaji, faida na gawio na ulinzi dhidi ya utaifishaji ;
(e) Upangaji wa bei au mauzo ya dhahabu;
(f) Kubakisha na kuhamisha nje ya nchi fedha za kigeni;
(g) Wajibu wa kulipa mrahaba, kodi ya mapato na namna ya kuzihesabu kodi hizo;
(h) Jambo lolote ambalo ni la msingi kwa hali ya kiuchumi ya Kampuni.
Mkataba unatamka kwamba vifungu hivyo vya Mkataba ni vya msingi na vitakatifu na kwamba endapo vitabadilishwa na
kuiweka Kampuni katika hali mbaya ya kiuchumi kuliko ilivyokuwa wakati wa kusaini Mkataba, basi Serikali kwa mashauriano na Kampuni itachukua hatua za lazima kuhakikisha kwamba haki au maslahi ya Kampuni hayaporomoshwi au kupunguzwa kimsingi!
VI. UTATUZI WA MIGOGORO
Kufuatiwa hoja ya Mheshimiwa Zitto Kabwe juu ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mazingira ya kusainiwa kwa Mkataba wa Buzwagi, kumejitokeza mjadala mkali juu ya utashi wa kimaadili na/au madhara ya kisheria ya Mkataba huu kusainiwa London nchini Uingereza. Tumezungumzia kwa kirefu viwango vya maadili na/au utashi unaotakiwa kwa viongozi wa umma chini ya Sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma na hatuna haja ya kurudia mjadala huo. Mjadala unaohusu madhara ya kisheria ni wa muhimu vile vile. Mahali unaposainiwa mkataba (locus contractus) ni muhimu sana kisheria kwa sababu endapo mkataba wenyewe uko kimya juu ya utaratibu wa kutatua migogoro inayoweza kutokana na utekelezaji wa mkataba wake basi sheria za mahali uliposainiwa ndio zinazotumika.
Mkataba wa Buzwagi umefafanua juu ya utaratibu wa kutatua migogoro inayoweza kutokea kutokana na utekelezaji wa Mkataba huu. Kama alivyosema Waziri Karamagi Bungeni, Mkataba wa Buzwagi unataja kuwa sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo itaongoza mkataba huo. Kauli hii ya Waziri Karamagi ni sehemu tu ya ukweli wa jambo hili kwani kuna ukweli mwingine ambao Waziri Karamagi hakuutaja. Kwanza, Mkataba huu utatawaliwa na sheria za Tanzania na taratibu za sheria za kimataifa zinazohusika. Jambo hili limetiliwa nguvu zaidi na kifungu cha 13 cha Mkataba kinachoamrisha kwamba mgogoro wowote utatatuliwa kwa upatanishi kufuatana na Kanuni za Upatanishi za Tume ya Umoja wa Mataifa ya Sheria za Kimataifa za Biashara (UNCITRAL).
Pili, mahakama za Tanzania hazina mamlaka ya kusikiliza na/au kutatua migogoro chini ya Mkataba huu kwani jukumu hilo imepewa Mahakama ya Upatanishi wa Kimaifa ya London kufuatana na Kanuni za Upatanishi za UNCITRAL zitakazokuwa zinatumika wakati wa kusaini Mkataba huu. Chini ya utaratibu wa Mkataba huu, kila upande unapaswa kuteua mpatanishi mmoja na wapatanishi hao wawili watachagua mpatanishi wa tatu ambaye ndiye atakuwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Upatanishi. Aidha, kesi ya upatanishi huo itafanyika London na lugha itakayotumika ni Kiingereza. Vile vile hukumu yoyote itakayotolewa na Mahakama ya Upatanishi itazifunga pande zote na Serikali inafuta haki zake za kudai ulinzi dhidi ya mashtaka kwa nchi huru (sovereign immunity) na inafuta madai yoyote ya ulinzi huo kuhusu mashauri ya kukaza hukumu hiyo
na ulinzi kuhusu ukazaji wa hukumu dhidi ya mali yoyote ya Serikali inayotumika kwa ajili ya shughuli za biashara.
Tatu, ni muhimu kuelewa kwamba ingawa Mkataba wa Buzwagi unasema kwamba utaongozwa na sheria za Tanzania, sheria zenyewe hazilindi uhuru wa taifa letu na mamlaka ya kikatiba ya taasisi zetu za kutatua migogoro. Kwa mfano, Sheria ya Madini Na. 5 ya mwaka 1998 - ambayo ndiyo sheria itakayoongoza Mkataba huu inatamka kwamba migogoro yoyote kati ya mmiliki wa Leseni Maalumu ya Uchimbaji na serikali utatatuliwa kwa kufuata kanuni au taratibu za Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID). Kituo hiki ni moja ya taasisi za Benki ya Dunia na kina makao yake makuu New York, Marekani.