Azam FC yaipiga Stand Utd, Kapombe azidi kufanya kweli
By ppkahemele on March 16, 2016
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imezidi kufanya kweli kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya jioni ya leo kuichapa Stand United bao 1-0 katika mchezo mkali uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.
Alikuwa ni beki wa kulia Shomari Kapombe, aliyeihakikishia pointi tatu muhimu Azam FC baada ya kufunga bao zuri dakika ya 62 akiserereka chini na kupiga shuti lililigonga nyavu za juu akimalizia krosi safi ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Allan Wanga.
Stand United walicheza mchezo huo kwa kulundikana eneo moja kila Azam FC ilipokuwa na mpira kuliwanyima mabingwa hao nafasi ya kuuchezea mpira hasa safu ya ushambuliaji iliyokuwa ikiundwa na Tchetche aliyekuwa akisaidiana na Wanga na hivyo kufanya kipindi cha kwanza kuisha kwa suluhu.
Hadi dakika 90 za mwamuzi Ngole Mwangole kutoka mkoani Mbeya zinamalizika, walikuwa ni Azam FC walioweza kuibuka kifua mbele na kuzoa pointi zote tatu.
Ushindi huo unaifanya Azam FC kuifikia Yanga kwa pointi, wote wakiwa nazo 50 huku akiwa ameachwa kwa pointi nne na kinara Simba iliyojikusanyia jumla ya pointi 54 lakini iko mbele kwa michezo miwili dhidi ya wapinzani wake hao katika mbio za ubingwa.
Kikosi cha Azam FC kiliundwa;
Aishi Manula, Shomari Kapombe, Farid Mussa/Wazir Salum (dk 65), Aggrey Morris, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Jean Mugiraneza, Frank Domayo, Mudarhir Yahya/Michael Bolou (dk 79), Kipre Tchetche, Allan Wanga/John Bocco (C) dk 45.
Source:
Azam FC yaipiga Stand Utd, Kapombe azidi kufanya kweli | The Official Website of Azam Football Club