habari yenyewe hii hapa...
[h=3]MADUDU YA LIGI KUU, MECHI ZINAONYESHWA LIVE TIMU HAZILIPWI. CHAMAZI INAONGOZA KWA DHULUMA[/h]

LIGI Kuu ya soka ya Tanzania Bara inaendelea wikiendi hii katika viwanja tofauti tofauti, lakini kuna jambo moja linalokwenda ndivyo sivyo. Matangazo ya haki za televisheni ya ‘live' yanayoendelea hayaendi inavyotakiwa.
Kama utagundua, mechi kadhaa za Azam FC zimekuwa zikionyeshwa ‘live' kwenye Uwanja wa Chamazi bila kuzingatia baadhi ya mambo muhimu ikiwemo timu pinzani kulipwa haki za matangazo hayo bila kuzingatia uenyeji kama ilivyo kawaida.
Kwa muda mrefu klabu za Simba na Yanga zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mechi zake hazirushwi ‘live' bila kuwepo makubaliano maalum kutoka kwa chombo husika au kampuni yoyote inayotaka kufanya hivyo.
Sasa hali ni toifauti kwani mechi za Azam zinaonyeshwa live kutoka Uwanja wa Chamazi unaomilikiwa na timu hiyo iliyo chini ya makampuni ya S. S Bakhressa, mbaya zaidi bila kufuata haki za matangazo kwa klabu pinzani.
MFANO HAI
Jumatano ya Februari 20, 2013 kwenye Uwanja wa Chamazi, JKT Ruvu ilikuwa mwenyeji dhidi ya Azam na matokeo yakawa Azam mshindi kwa mabao 4-0. Mchezo huu ulionyeshwa live na televisheni ya StarTV.
Inavyotakiwa, kabla ya mchezo huo ni lazima Azam, JKT na Kamati ya Ligi inayosimamia Ligi Kuu ya Bara zikubaliane juu ya uonyeshwaji huo wa moja kwa moja.
Mambo hayo yote yanatakiwa yawemo katika mkataba huru unaowezwa kuona na pande zote muda wowote inapohitajika kufanyika hivyo.
STAR TV INALIPWA NA AZAM
Azam kwa kuzingatia kwamba inahitaji zaidi kutangaza bidhaa zake kupitia timu yake ya soka, imelazimika kuwa inailipa StarTV kiasi cha fedha kisichopungua Sh. 5 milioni ili mechi yake moja iweze kurushwa live na kituo hicho.
"Azam huwa wanatulipa ili tuweze kuonyesha mechi zao moja kwa moja. Kwa kweli mambo yanakwenda vizuri maana kwao inawasaidia kwa kujitangaza zaidi na sisi tunaingiza fedha kupitia matangazo hayo kuwa yamelipiwa na wao siyo sisi kuwalipa wao," kilisema chanzo chetu kutoka StarTV.
Kwa kauli hii, ina maana StarTV haifanyi mazungumzo na klabu inayocheza Chamazi na Azam bali jukumu hilo linabaki kwa Azam wenyewe na klabu husika. Hapa kuna tatizo kwani, Azam haina haki ya 100% ya kurusha live mechi zake zinazochezwa Chamazi hata kama itakuwa mwenyeji.
AZAM YAKIRI KUILIPA STAR TV
Mmoja wa viongozi wa Azam ambaye hakupenda jina lake kutajwa, amesema kila mchezo wao unapokaribia hufanya mawasiliano na StarTV kisha kuwalipa kiasi cha fedha kisichopungua Sh. 5 milioni na mechi zao kuonyeshwa live.
"Sisi tunazungumza na StarsTV kisha tunawalipa gharama za kuonyesha mechi live, ambazo huwa kuanzia Sh. 5 milioni, bada ya hapo mechi inachezwa," alisema kiongozi huyo na alipiulizwa kuhusu malipo ya klabu pinzani, alijibu:
"Hayo ya kuwalipa klabu pinzani mimi siwezi kukujibu lolote kwani hilo ni suala la watu wa timu moja kwa moja. Nadhani kama kungekuwa na tatizo wangetuzuia," alisema kiongozi huyo.
JKT RUVU HAIKULIPWA
Baada ya kujiridhisha na maelezo ya Azam na StarsTV, mtandao huu uliwasiliana na mmoja wa viongozi wa JKT Ruvu ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake kwa sababu maalum, ambaye alisema timu yake haikulipwa haki za mechi kuonyeshwa live Februari 20, 2013 kwenye Uwanja wa Chamazi.
"Ndugu yangu, sikudanganyi mimi sikuona malipo yoyote kutokana na mechi ile kuonyeshwa live. Sijuhi labda kwa viongozi wenzangu yawezekna wao wamelipwa lakini kwa utaratibu wetu hapa, tungekuwa tumewasiliana na fedha kuletwa klabuni. Hivyo fedha hiyo ni kama haikulipwa," alisema kiongozi huyo.
YANGA ILIKATAA MTEGO WA AZAM
Jumamosi Februari 23, 2013, Yanga ilicheza na Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Azam ilitaka mchezo huo uonyeshwe live na kulipa Yanga Sh. 10 milioni, lakini Yanga walikataa.
Katika mchezo huo ulioisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Haruna Niyonzima, mashabiki zaidi ya 36,000 waliingia uwanjani na kuingiza kiasi cha Sh. 250 milioni.
Yanga walikuwa wajanja zaidi kwa kuiona thamani yao na kukataa kiasi kidogo cha Sh. 10 milioni ambacho walitaka kulipwa ili mechi yao irushwe live.
KAMATI YA LIGI HAIJUI
Kwa kawaida, mechi yoyote inayotakiwa kuonyeshwa live, ni lazima makubaliano yake yafikiwe na timu zote mbili na kamati ya ligi. Vyombo vyote hivyo vina mgao wake wa fedha.
Mtandao huu ulipowasiliana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia kuhusu hali hiyo, alisema hayupo ofisini na ndiyo kwanza anarejea jijini Dar es Salaam, hivyo apewe muda wa kuwasiliana na wenzake ili kujua kilichotokea.
Lakini Karia alisema, kimsingi klabu zote mbili zinapaswa kukubaliana juu ya uonyeshwaji wa mechi na pia kamati nayo inapaswa kujua hali hiyo pia kufahamu kaisi cha fedha kitakachoingia kwao.
MGONGANANO WA MASLAHI BINAFSI
Mtandao huu, haukuweza kuzungumza na Mwenyekiti wa Azam ambaye ni pia ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Said Mohamed kwani jambo hili lipo katika mgongano wa maslahi.
Mgongano huo wa maslahi kwa Said Mohamed unakuja kwamba, yeye ndiye anayepaswa kukubaliana kimaslahi kama mtendaji wa Azam na wakati huohuo akiwa kama kiongozi wa kamati ya ligi.
Hata kama kamati ya ligi ina wajumbe wengine, lakini Said Mohamed anachukua nafasi kubwa kama makamu mwenyekiti na pia kiongozi wa Azam, hivyo uaminifu unaweza kuwa mdogo kwa suala hili.
VIONGOZI HAWAJUHI HAKI ZA KLABU ZAO
Mara kadhaa unaweza kwenda uwanjani na kukuta mambo yanatendeka kinyume na matakwa au kanuni zinavyotaka. Mfano halisi ni hili la matangazo ya live.
Klabu inaweza kufika uwanjani na kukuta mechi inaonyeshwa live na wasiwe na wasiwasi wowote bila kujua kama wanapoteza haki yao ya kimsingi siku hiyo. Nayo ni kulipwa kwa kitendo cha wao kuonekana moja kwa moja.
Kote duniani na hata hapa bara, mechi yoyote ya live ni lazima timu zote mbili zilipwe haki zao tena kwa makubaliano maalum. Hapo kila timu itaangalia thamani yake na kukubaliana na fedha wanayotaka kulipwa.
Kwa Ligi Kuu ya Kenya, timu zote hupata kiasi kisichopungua Sh. 150 milioni (kwa thamani ya fedha ya Tanzania) kutokana na kituo cha Supersport kuonyesha mechi zao live. Hicho ni kiasi kikubwa katika kuiendesha klabu na kuweza kushindana kikamilifu.
Kumbuka hata wakati ule GTV ilipokuja nchini na kuingia mkataba wa kuonyesha live beedhi ya mechi za ligi kuu, kila klabu iliambulia kiasi cha fedha kwa kitendo chao cha kuonekana live.
KWA NINI MECHI ZA CHAMAZI TU?
Azam inacheza mechi zake za ligi kuu katika viwanja vingi chini, lakini mpango huu wa kuonyesha mechi zake live unatumika zaidi katika uwanja wa Chamazi, labda kwa sababu zifuatazo;
Kwamba, ni mbali ambako hata watu mbalimbali wadadisi wa mambo hawawezi kubaini tatizo na hata kuwashtua viongozi wa timu nyingine juu ya haki yao ya msingi ya kulipwa fedha hizo. Ukweli ni kwamba, watu wengi huwa hawaendi katika mechi za uwanja huo zinazochezwa katikati ya wiki.
Kitendo cha Azam kuwa mwenyeji wa uwanjani, kinawafanya timu pinzani kutokuwa na ujasiri wa kuuliza mambo mbalimbali ya yanayoendelea uwanjani hapo kwani unaweza kuziona kamera zaidi ya mbili uwanjani na ukadhani labda ni moja kati ya mipango ya Azam ya kurekodi mechi zake.
Ikumbukwe ya kuwa, ufahamu ya kujua kwamba mechi hii inaonyeshwa live au tofauti haupo kwa kila kiongozi wa timu za ligi kuu.
MSIMAMO WA MTANDAO HUU
Tunaipongeza Azam kwa kutaka kuonyesha live mechi zake zote inazocheza kwenye Uwanja wa Chamazi, lakini ni muhimu kwao kufuata kanuni kwa kuzilipa timu inazocheza nazo ili kufuta manung'uniko.
Viongozi wa klabu zote za ligi kuu kuacha kuona kila kitu ni kawaida kutokea kwani kuna wakati wanapoteza haki zao za msingi na kujikuta wakiendelea kulia na ukata wakati mianya ya fedha wanaiacha bila kujielewa.
Tunaiomba kamati ya ligi kufanya kazi kikamilifu kwa kuzingatia haki na kanuni za mambo yote yahusuyo ligi hiyo. Pia ifanye kazi kwa kwenda viwanjani na kusimamia mambo yote ya msingi kama haya ya mechi kuonyeshwa live.
Tuna imani hiki tulichokiandika kitafanyiwa kazi na kila upande uweze kupata haki zake stahiki.
Mwisho