Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
TAMKO KULAANI KUVAMIWA KWA MWANDISHI WA HABARI
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unalaani vikali kitendo cha kuvamiwa na kuzuiwa kufanya kazi za uandishi wa habari kinyume na sheria kwa mwandishi wa habari wa Ayo Tv kilichotokea jana Ijumaa Septemba 19, 2024 akiwa anatekeleza majukumu yake katika Kijiji cha Mbuyuni, kata ya Makuyuni, wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
Mwandishi huyo Godfrey Ng'omba alivamiwa na Polisi pamoja na wasaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akiwa anarekodi tukio la wananchi kufunga barabara katika Kijiji cha Mbuyuni kutokana na tukio la watoto kupotea katika mazingira ya kutatanisha na wengine kukutwa wamefariki huku wakiwa wamenyofolewa figo. Wananchi wanahaki ya kutumia vyombo vya habari kuelezea shida zao, kitendo cha kumzuia mwandishi asitoe taarifa ya wananchi waliokuwa na kilio chao kuhusu vifo vya watoto wao ni kinyume na Katiba na misingi ya utawala bora.
Askari Polisi pamoja na wasaidizi wa Mkuu wa Mkoa walimvamia na kumzuia kufanya kazi za uandishi wa habari ikiwemo kutaka kumnyang'anya camera na hatimae walimnyang'anya kadi ya kwenye camera na kuondoka nayo. Mwandishi hakuvunja Sheria yoyote kwakuwa alikwenda kutafuta habari katika matukio yanayotokea katika jamii.
Kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 waandishi wa habari wana haki na uhuru wa kutafuta habari ikiwa ni pamoja na kuuhabarisha umma juu ya habari hizo, hivyo kwa namna yoyote ile ni makosa na ni kinyume cha Katiba na Sheria za nchi kumshambulia mwandishi wa habari akiwa anatekeleza majukumu yake.
Wito wetu
Mtandao unatoa wito kwa askari Polisi na wasaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kurudisha kadi ya mwandishi Godfrey Ng'omba ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kuuhabarisha umma.
Mtandao unatoa wito pia kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuwaelekeza wasaidizi wake kuheshimu kazi za waandishi wa habari na kutokuwashambulia ukizingatia pia ukweli kwamba Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha ni mdau mkubwa wa matumizi ya waandishi na vyombo vya habari
Mtandao unatoa wito kwa wananchi na viongozi wote kuheshimu waandishi wa habari wanapokuwa wanafanya kazi zao.
Imetolewa na,
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Septemba 20, 2024 Dar es Salaam, Tanzania.