SoC03 Tiba ya msongo wa mawazo

SoC03 Tiba ya msongo wa mawazo

Stories of Change - 2023 Competition

GoJeVa

Member
Joined
Sep 15, 2021
Posts
41
Reaction score
60
TIBA YA MSONGO WA MAWAZO.

Utangulizi.
Msongo wa mawazo ni hali ya mtu kuzongwa na mawazo hasi ambayo mara nyingi hupelekea matokeo mabaya Kwa muhusika hasa pale asiposaidiwa au asipojisaidia kutoka kwenye changamoto hiyo. Tatizo hili limekuwa ni jambo mtambuka Kwa kizazi chetu, na hii inapelekea kesi nyingi za watu kujidhuru au kudhuru wengine.

Dunia ina changamoto nyingi sana, kama vile magonjwa,ugumu wa maisha na changamoto zinginezo. Ni vigumu kumkuta binadamu asiye na changamoto katika Dunia hii hivyo usidhani changamoto zipo upande wako tuu, jambo la muhimu ni jinsi ya mapokeo ya changamoto hizi na jinsi ya kuzikabili.

".....Chuma ni rahisi kuteketea Kwa kutu, ikumbukwe Chuma hushiriki kutengeneza hiyo kutu. Bila Chuma kuwepo kutu haiwezi kutoke, Vivyo hivyo binadamu hushiriki kutengeneza msongo wa mawazo ndani yake na ikumbukwe bila binadamu msongo wa mawazo hauwezi kuwepo, na huo msongo wa mawazo huweza kumteketeza binadamu..."

Kabla ya kuendelea hebu tupate funzo kutoka katika mkasa wa kweli unaonihusu Mimi hapo chini;
Nakumbuka ilikuwa mwaka 2015 huu ni mwaka niliohitimu shahada yangu. Baada ya kuhitimu nilipitia changamoto nyingi sana ambazo ndio zimefanya niandike andiko hili. Kwanza kabisa sikubahatika kuajiriwa hivyo nilijiari kwa kuwa muuzaji wa viatu vya mtumba pale Ubungo(machinga), baada ya kupata mtaji kidogo nilirudi kijijini kwetu na kwenda kuanza kilimo cha maharage. Bahati mbaya mwaka niliolima mvua hazikunyesha vizuri, mazao yangu yalikauka hivyo nikaambulia hasara.

Hilo lilipopita nikaamua kwenda kuomba ajira kwenye taasisi moja huko wilayani kwetu, kwenye hiyo taasisi waliniambia watakuwa wananilipa laki na nusu(150,000) kutokana na ugumu wa maisha nilikubali na kuanza kazi hapo. Miezi sita ilipopita nilishindwa kuendelea kufanya kazi pale hivyo niliacha, kuanzia hapo msongo wa mawazo ulianza kunisonga na kujikuta nadumbukia kwenye matumizi ya kupindukia ya pombe na bangi nikidhani najiweka sawa kiakili.

Wazazi wangu walipoona nazidi kuharibikiwa walinipa msaada, nakumbuka mama yangu alinikutanisha na mchungaji wa kanisani kwao huyo mchungaji alisaidia sana kunitoa kwenye changamoto yangu ya msongo wa mawazo. Hadi sana nimerudi kwenye hali yangu ya kawaida, japo bado sijaajiriwa lakini nimekuwa mjasilimali na maisha yanaendelea vizuri.

Nakumbuka mchungaji huyo aliyenisaidia alikuwa anapenda kuniambia..."Kijana wangu, jifunze angalau kumshuru Mungu kwani amekufanyia mengi hadi wakati huu, amekupa uhai, amepa ndugu,jamaa na marafiki, amekupa elimu na mengineyo mengi. Hivyo mpe Mungu shukrani atakufungulia na milango mingine.." kauli hii ilikuwa inanijenga sana.

NJIA ZA KUKABILIANA NA MSONGO WA MAWAZO.

Zipo njia nyingi chanya za kukabiliana na msongo wa mawazo katika makala hii nitadadavua njia tatu ambazo ni rahisi na Kwa kiasi kikubwa zinapatika katika mazingira yetu.

1. Kuzungumza tatizo lako Kwa watu wako wa karibu ili upate ushauri. Binadamu huwa tuna kiwango Cha mwisho Cha uvumilivu, ni rahisi kujidhuru pale uvumilivu unapofika mwisho. Ndio maana unashauriwa usipende kukaa na matatizo moyoni kwa kipindi kirefu bila kushirikisha watu wako wa karibu kama vile; ndugu, jamaa na marafiki ambao wanaweza kukutoa kwenye changamoto hiyo.
".... Msongo wa mawazo huondoa hofu ya kifo ndio maana ni rahisi binadamu kujidhuru pale anapokabiliwa na changamoto hiyo. Hivyo unapokuwa kwenye changamoto hii epuka upweke na jitaidi kushirikisha watu wako wa karibu ili kupata msaada...."

2. Kumuona mwanasaikolojia na kumshirikisha changamoto yako. Mwanasaikolojia ni mtaalamu aliyesomea jinsi ya kumuweka sawa mtu anayesumbuliwa na msongo wa mawazo au afya ya akili. Hivyo kupitia wataalamu hawa tatizo lako linaweka kuisha na wewe kubaki salama kabisa.

3. Kwenda nyumba za ibada kama vile msikitini Au kanisani.
Upande wa maandiko tutaangalia namna binadamu atakavyoweza kukabili na kushinda msongo wa mawazo Kwa kutumia moyo wake. Moyo huweza kumaliza kabisa tatizo hili la msongo wa mawazo, binadamu anapozaliwa moyo wake huwa tupu ila anavyoendelea kuishi moyo wake huanza kujazwa mambo mbalimbali. Moyo wa mwanadamu ukijazwa mambo yaliyo mema (mambo ya Kimungu) binadamu huyo atakuwa salama na ataishi kwa Raha katika hii Dunia ila moyo wa mwanadamu ukijazwa mambo yasiyo mema (mambo ya kishetani binadamu huyo ataishia kutaabika na kuteseka katika maisha yake yote. Hivyo Kila mwanadamu inabidi aruhusu mambo mema yaote katika moyo wake, rejea Mithali 4:23, hapa maandiko yanamkumbusha binadamu kulinda moyo wake kwani katika moyo wake ndio uzima hutoka humo. Vivyo hivyo ukiruhusu amani ndani ya moyo hauwezi kupata msongo wa mawazo.

Ukiruhusu mambo mema yaote katika moyo wako vilevile Mungu atakufanyia mema katika maisha yako, wakati ukiruhusu mabaya yaote katika moyo wako vilevile shetani atatawala maisha yako, hapo shetani atatawala moyo wako na kuujaza matatizo mengi ikiwemo msongo wa mawazo Kwa sababu Mungu hawezi kukufanya uteseke na msongo wa mawazo, lakini shetani huweza kufanya hivyo. Rejea maandiko matakatifu, Jeremia 17: 9, hapo maandiko yanatuambia moyo ni mdanganyifu Sana kuliko kitu chochote, hivyo inabidi tuwe makini nao sana kwani usipokuwa na Mungu moyo unaweza kukudanganya Kwa kukujaza msongo wa mawazo na hatimaye kukupelekea umauti.

Moyo wa mwanadamu ni dawa na huweza kumtoa mwanadamu kwenye changamoto yoyote, lakini vilevile moyo huo huo ukimkabidhi shetani unaweza kukupelekea kufanya maovu ambayo ni ya kutisha. Rejea Mithali 17:22, hapo maandiko yanatukumbusha kuwa moyo uliochangamka ni dawa, hivyo basi turuhusu furaha katika mioyo yetu ili tutibike kutoka kwenye changamoto hii ya msongo wa mawazo.

Ukipatwa na msongo wa mawazo usiende kutumia vilevi kama vile pombe, bangi, madawa ya kulevya ukiamini changamoto hiyo itaisha, hapana msongo wa mawazo hauwezi ondoka Kwa vilevi bali utazidi kuingia kwenye kilindi cha matatizo. Kumbuka, Vilevi havijawai kuwa tiba ya msongo wa mawazo toka kuumbwa Kwa Dunia.

Ukiendekeza msongo wa mawazo unakuwa unadidimiza ndoto zako, Kwani ukiwa na changamoto hiyo inapelekea akili yako kushindwa kufanya kazi Kwa ufanisi. Hivyo basi, akikisha unaepuka msongo wa mawazo ili uendelee kukimbilia, kukaribia na kutimiza ndoto zako. AHSANTE.
#Epuka.msongo.wa.mawazo#
 
Upvote 3
Back
Top Bottom