Karamagi angolewa TICTS
na Irene Mark
KAMPUNI ya kimataifa ya kupakua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam (TICTS), ambayo iko hatarini kufutiwa mkataba wake wa miaka 15, imemuondoa katika uenyekiti wa bodi yake, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.
Karamagi anakutwa na zahama hiyo ikiwa ni miezi miwili tangu alipolazimishwa kujiuzulu uwaziri huo, akihusishwa na kashfa ya ufisadi kwenye mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa Richmond.
Habari zaidi kutoka ndani ya TICTS zinaeleza kwamba, kuondolewa kwa Karamagi kumechukuliwa kama hatua mahususi ya kurejesha uhusiano imara kati ya kampuni hiyo na serikali.
Kwa mujibu wa habari hizo, mbali ya kuondolewa katika nafasi hiyo, tayari mazungumzo yameshaanza ndani ya TICTS ili kuangalia uwezekano wa kununua hisa zote za Karamagi ndani ya kampuni hiyo.
Baada ya kuondolewa kwake, nafasi hiyo ya Karamagi sasa imechukuliwa na Mkurugenzi wa Kundi la Hutchson Port Holdings (HPH), ambalo ni kampuni mama ya TICTS, John Meredith, tangu Mei 8, mwaka huu.
Katika mazungumzo ya Mwakilishi wa HPH kutoka Hongkong, Neville Bissett na waandishi wa habari yaliyofanyika Dar es Salaam jana, ilielezwa kwamba kuondolewa kwa Karamagi, kutatoa nafasi nzuri kwa uongozi mpya wa kampuni hiyo, inayolalamikiwa kwa ufanisi hafifu, kuzungumzia utata wa mkataba wa TICTS.
Kampuni iliona ili iweze kuwasiliana vyema na serikali, hasa kuhusu utata uliojitokeza, ni bora haya mabadiliko (kuondolewa kwa Karamagi), yangekuwepo, alisema Bissett baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi wa nyongeza ya miaka 15 ya mkataba kati ya kampuni yake na serikali, ulioibua mzozo ndani na nje ya Bunge, hivi karibuni.
Mwakilishi huyo alisema, tayari TICTS imewekeza dola za Marekani milioni 21 tangu kuanza kwa mkataba wake, kiasi ambacho ni zaidi ya mipango ya uwekezaji iliyomo katika mkataba wa ukodishwaji wa kitengo hicho.
Tangu kuongezwa kwa muda wa mkataba mwishoni mwa mwaka 2005, TICTS imejitahidi kukabiliana na uhaba wa nafasi bandarini hapo kwa kubomoa maghala na kuingiza vitu muhimu kwa kazi ya upakuaji na upakiaji wa makontena kwa viwango vikubwa kazi ambayo isingeweza kufanyika bila kuongezewa mkataba, alisema.
Hata hivyo, Bissette alibainisha kwamba, kiasi cha dola milioni 60 za Marekani zitawekezwa kwenye vifaa na upanuzi wa miundombinu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mwakilishi huyo alisema, Mwenyekiti mpya wa TICTS amefurahishwa kwa kuwa serikali imeunga mkono uongezwaji wa mkataba wake hadi mwaka 2025 kwa sababu ni muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu.
Meredith alitazama mustakabali wa kazi hii, akaonekana kufurahishwa na jinsi serikali ilivyounga mkono uongezwaji wa mkataba wake hadi mwaka 2025, kwa sababu ni muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu ya bandari husika.
TICTS imedhamiria kuleta maendeleo ya kitengo cha makontena jitihada zikilenga kuifanya Tanzania iwe bandari yenye ufanisi zaidi Afrika Mashariki, alisema mwakilishi huyo kwa niaba ya mwenyekiti mpya ambaye hakuwepo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Hivi karibuni, suala la kuongezwa kwa mkataba huo lilizua mtafaruku kiasi cha wabunge kuikalia kooni serikali na kusababisha Karamagi ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), kutakiwa kutoa maelezo kwa Spika wa Bunge kuhusu kauli zake ndani ya Bunge alipokuwa akitetea ongezeko la mkataba huo.
source: TanzaniaDaima