Timbulo aja na Sina Makosa
Timbulo aja na Sina Makosa
na Elizabeth John
MKALI wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ally Timbulo ‘Timbulo' anatarajia hivi karibuni kuachia kibao chake kipya, ‘Sina Makosa'.
Licha ya kutaka kutoka na kibao hicho, Timbulo alishawahi kutamba na kibao chake cha ‘Samson na Delila', ambacho kilifanya vizuri zaidi katika vituo mbalimbali vya redio.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Timbulo alisema yupo katika hatua za mwisho za uandaaji wa kibao hicho, ambacho anatarajia kukiachia baada ya Sikukuu ya Pasaka.
"Namshukuru Mungu baadhi ya kazi zangu zimepokelewa vizuri na mashabiki, naomba mashabiki wangu wakae mkao wa kula kwa ajili ya kazi nyingine ambazo zinafuata," alisema Timbulo.
Alisema kazi hiyo ina ujumbe mzito na kwamba inafundisha na kuelimisha jamii bila kujali umri wa msikilizaji au shabiki wa kazi zake.
Timbulo alisema kibao hicho atakitoa pamoja na video yake kwa lengo la kuwapa burudani iliyokamilika mashabiki wake.