Tishio la Muswada wa Marekani, Kunyimwa misaada; Je, Tanzania inafuata njia ya Zimbabwe?

Tishio la Muswada wa Marekani, Kunyimwa misaada; Je, Tanzania inafuata njia ya Zimbabwe?

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014
91d46b11-2085-493e-b23f-0600e706f3b4.jpg

Wakati uhusiano kati ya Tanzania na Marekani ukiingia katika kipindi nyeti zaidi katika miaka ya karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amefanya ziara muhimu nchini Marekani inayobeba uzito mkubwa wa kidiplomasia kuliko inavyoonekana juu juu.

Rasmi, ziara hiyo imelenga kuwasilisha ujumbe maalumu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, mazingira ambayo ziara hiyo imefanyika yanaifanya ionekane pia kama sehemu ya juhudi kubwa za kidiplomasia za kuzuia kuzorota kwa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.

Ziara hiyo imekuja wakati Seneti ya Marekani ikianza kupitia Muswada wa S.4577, unaojulikana kama Reassessing the United States-Tanzania Bilateral Relationship Act, uliowasilishwa na maseneta wawili wenye ushawishi mkubwa kutoka vyama viwili vikuu vya siasa nchini humo, Jeanne Shaheen wa Democratic Party na Ted Cruz wa Republican Party.

Ted_Cruz_official_116th_portrait_(3x4_cropped).jpg


Muswada huo ni matokeo ya wasiwasi uliojitokeza Washington kufuatia uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025, ambao baadhi ya wadau wa kimataifa walidai uliambatana na ukiukwaji wa haki za binadamu, ukandamizaji wa upinzani na vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza.

Hii inakuwa ziara ya pili ndani ya kipindi kifupi, baada ya ziara iliyofanyika Desemba 2025, jambo linaloashiria kuwa Serikali ya Tanzania imeanza kuona umuhimu wa kuwekeza nguvu zaidi katika diplomasia ya moja kwa moja na watunga sera wa Marekani wakati mjadala kuhusu Tanzania ukizidi kushika kasi ndani ya Bunge la Marekani.

Kwa kawaida, mawaziri wa mambo ya nje hufanya ziara nyingi za kikazi katika nchi mbalimbali, lakini kurudi Marekani kwa mara ya pili katika mazingira ambayo Muswada wa S.4577 umeanza kupata uungwaji mkono kutoka pande zote mbili za siasa za Marekani kunaonyesha kiwango cha wasiwasi kilichopo Dodoma kuhusu mwelekeo wa uhusiano wa nchi hizo mbili.

Tanzania Yachagua Diplomasia ya Mashambulizi ya Kimya​

Katika siku zake za kwanza nchini Marekani, Kombo amekutana na viongozi kadhaa waandamizi wa serikali ya Marekani pamoja na wabunge wenye ushawishi katika masuala ya Afrika.

Miongoni mwa mikutano hiyo ni pamoja na mazungumzo yake na Allison Hooker, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa, ambapo pande hizo zilijadili maendeleo ya uhusiano wa Tanzania na Marekani, uhuru wa dini, uhuru wa kujieleza na fursa za biashara.

Aidha, Kombo amekutana na wabunge Jonathan L. Jackson na Dkt. Ronny L. Jackson, ambao wote wameonyesha nia ya kutembelea Tanzania katika siku zijazo. Pia amefanya mazungumzo na Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani (U.S. Chamber of Commerce) pamoja na wawekezaji wa Marekani waliopo Tanzania.

Serikali ya Tanzania inaonekana kutaka kuonyesha kwamba licha ya tofauti zilizojitokeza baada ya uchaguzi wa 2025, bado ni mshirika muhimu wa Marekani katika biashara, uwekezaji na usalama wa Afrika Mashariki.

Hatari ya Muswada Muswada​


Senetor.png

Changamoto kubwa kwa Tanzania ni kwamba muswada huu hauishii katika kutoa maoni ya kisiasa pekee.
Iwapo utapitishwa, unaweza kuielekeza Serikali ya Marekani kufanya tathmini mpya ya uhusiano wake na Tanzania, kusitisha baadhi ya misaada ya maendeleo na usalama, kuzuia ushirikiano kupitia Millennium Challenge Corporation (MCC), na hata kuweka vikwazo dhidi ya viongozi binafsi watakaohusishwa na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Muswada huo pia unataka tathmini ya ushawishi wa China nchini Tanzania na athari zake kwa maslahi ya Marekani katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mtazamo wa kisiasa wa Marekani, kazi hiyo si rahisi.

Kwanza, muswada huo unaungwa mkono na maseneta kutoka vyama vyote viwili vikuu. Marekani inapofikia hatua ya kuwa na makubaliano ya Democrat na Republican kuhusu suala la sera ya nje, uwezekano wa kulizuia hupungua kwa kiasi kikubwa.

Pili, muswada wenyewe unaweka masharti ya matokeo, si ahadi. Unataka Marekani kujiridhisha kwamba Tanzania imefanya mageuzi yanayoonekana katika masuala ya demokrasia, haki za binadamu na uhuru wa kisiasa kabla ya kurejesha kikamilifu baadhi ya aina za ushirikiano.

Hii ina maana kwamba hata kama Kombo atafanikiwa kuwashawishi baadhi ya wabunge au maafisa wa Marekani kuwa Tanzania ina nia njema, bado hoja kuu itabaki kuwa hatua zinazochukuliwa ndani ya Tanzania.

Tatu, suala la China linaifanya hoja kuwa pana zaidi kuliko siasa za ndani za Tanzania pekee. Marekani kwa sasa inaangalia kwa karibu ushawishi wa China katika Afrika, hususan katika nchi zenye umuhimu wa kimkakati kama Tanzania kutokana na nafasi yake ya kijiografia, bandari zake na utajiri wa madini muhimu kama nikeli na grafaiti.

Tanzania Bado Ina Kadi Muhimu​

Licha ya tofauti zilizopo, Marekani bado ina maslahi makubwa nchini Tanzania. Biashara kati ya nchi hizo mbili imefikia zaidi ya dola bilioni moja kwa mwaka. Tanzania pia ni mshirika muhimu katika usalama wa bahari ya Hindi, mapambano dhidi ya ugaidi katika Afrika Mashariki na usambazaji wa madini mkakati yanayohitajika katika teknolojia za kisasa.

Kwa sababu hiyo, wachambuzi wengi wanaamini kuwa lengo la Washington si kuvunja uhusiano na Tanzania bali kuushinikiza ufanyiwe marekebisho kulingana na matarajio ya Marekani kuhusu demokrasia na utawala bora.

Ndiyo maana ziara ya Kombo inaweza kusaidia kupunguza mvutano, kufungua njia za mazungumzo na kuzuia hatua kali zaidi dhidi ya Tanzania.

Wapinzani Nao Wapo Washington​

HKDzgOQXcAAzBwL.jpg
HKDzgOqXkAAPx48.jpg

Wakati Waziri Mahmoud Kombo akijaribu kuwasilisha taswira chanya ya Tanzania kwa viongozi wa Marekani, wanaharakati wa kisiasa na watetezi wa demokrasia kutoka Tanzania nao wamekuwa wakikutana na wabunge, maafisa wa serikali na taasisi za kutunga sera nchini Marekani wakitaka shinikizo zaidi dhidi ya Serikali ya Tanzania kufuatia uchaguzi wa 2025.

Tukio la hivi karibuni la Augustine Lissu, mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, akiwa pamoja na mlimbwende na mwanaharakati Tausi Likokola na makada wa chama hicho, Liberatus Mwang'ombe na Emanuel Katili, walifika mjini Washington, D.C. na kufanya mazungumzo katika ofisi ya Congressman Joe Wilson.

Hii ni kwa sababu wabunge wa Marekani hupata simulizi mbili tofauti; upande wa serikali unaosisitiza utulivu, maendeleo na ushirikiano wa kimkakati, na upande wa wanaharakati unaosisitiza ukiukwaji wa haki na ukosefu wa uwajibikaji.

Iwapo wanaharakati hao wataendelea kupata usikivu kutoka kwa maseneta na wajumbe wa kamati zinazoshughulikia sera za nje, wanaweza kuimarisha hoja zinazotumiwa na waandaaji wa Muswada wa S.4577. Hali hiyo inaweza kufanya iwe vigumu zaidi kwa watunga sera wa Marekani kupuuza madai yanayotolewa dhidi ya Tanzania.

Hata hivyo, ushawishi wao peke yake hauwezi kuamua hatima ya muswada huo. Marekani huangalia pia maslahi mapana ya taifa lake, ikiwemo biashara, usalama wa kikanda, ushindani wake na China pamoja na nafasi ya Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Pamoja na juhudi zote za pande mbili, ukweli unabaki kuwa wabunge wa Marekani wataangalia zaidi hali halisi inayojitokeza ndani ya Tanzania. Ikiwa kutakuwa na ishara za kuimarika kwa mazingira ya kisiasa, kuheshimiwa kwa haki za kiraia na kufunguka kwa nafasi za kisiasa, hoja za kutaka vikwazo zinaweza kupungua nguvu.

Kibano cha Bunge la Ulaya kwa Tanzania

cb82b8e6fcf239818f481689d0c6d5f8.webp

Bunge la Ulaya limepitisha azimio linalolitaka Tume ya Ulaya kuondoa mpango wake wa kutoa ufadhili kwa Tanzania kwa mwaka 2026, likieleza kuwa wasiwasi wake kuhusu hali ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria nchini haujapatiwa ufumbuzi.

Katika taarifa iliyotolewa Juni 18, 2026, wabunge wa Bunge la Ulaya (MEPs) walikubaliana kwa kura ya kuonyesha mikono kupinga rasimu ya uamuzi wa Tume ya Ulaya kuhusu ufadhili wa mpango wa utekelezaji wa mwaka 2026 kwa Tanzania.

Bunge hilo limesema tayari lilikuwa limepinga pendekezo hilo tangu Novemba 2025, lakini linaona kuwa Tume ya Ulaya imeendelea na maandalizi ya ufadhili huo bila kushughulikia hoja zilizotolewa na wabunge wake.

Kwa mujibu wa azimio hilo, wabunge hao wameeleza wasiwasi wao kuhusu uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025, ambao wameudai kuwa ulikumbwa na dosari kubwa, pamoja na hatua za Serikali za kukabiliana na maandamano yaliyofuatia uchaguzi huo. Wamedai kuwa matukio hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 400 na mamia ya watu kukamatwa kwa tuhuma za uhaini.

Aidha, Bunge la Ulaya limeeleza kutoridhishwa na hatua ya Serikali ya Tanzania kuahirisha mara kwa mara ziara ya ujumbe wa Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu ya Bunge hilo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziara hiyo iliahirishwa mwezi Februari na tena Mei 2026, jambo ambalo wabunge wamelitafsiri kama kukataliwa kwa ziara iliyolenga kujadili masuala ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria.

Tanzania inafuata njia ya Zimbabwe?

Yanayotokea Tanzania sio mageni, kwani yameshatokea kwingine. Mfano ni Zimbabwe ambayo mwanzoni mwa miaka ya 2000, ZANU-PF ilionekana kuchokwa na wananchi na hapo ndipo Rais Robert Mugabe akaanzisha Sera ya Mabadiliko ya Ardhi ili kuwabembeleza wananchi waliochoshwa na hali ngumu ya maisha.

Sera hiyo iliyotekelezwa kati ya 2001–2002 ililazimisha kuwanyang’anya Wazungu mashamba waliyokuwa wakiyamiliki kwa muda mrefu na kuwapa wazawa. Suala hilo lililalamikiwa na nchi za Magharibi zikidai kuwa haki haki haikutendeka kwa Wazungu.

Pia Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) zilidai kuwa kulikuwa na ukandamizaji wa wapinzani, uhuru wa vyombo vya habari na mashirika ya kiraia, huku Waangalizi wa kimataifa wakieleza kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki kutokana na vitisho na vurugu za kisiasa.

Vilevile wachambuzi wengi wanaamini kuwa pamoja na vikwazo, sera za ndani za serikali ya Rais Robert Mugabe pia zilikuwa sababu kubwa ya mdororo mkubwa wa uchumi uliotokea miaka ya 2000.

Vikwazo

Mwaka 2001 Marekani ilipitisha sheria ya ZDERA (Zimbabwe Democracy and Economic Recovery Act), iliyozuia Marekani kuunga mkono mikopo na misaada mipya ya taasisi za fedha za kimataifa kwa serikali ya Zimbabwe.

Mwaka 2002: Umoja wa Ulaya uliweka marufuku za kusafiri, kufungia mali za viongozi wa serikali na kuanzisha marufuku ya silaha.

Vilevile mwaka 2003–2008: Marekani ilipanua orodha ya watu binafsi na taasisi zilizowekewa vikwazo.

Matokeo yake

Matokeo yake uchumi wa Zimbabwe uliporomoka katika kipindi cha 2000–2008, ikiwamo kushuka kwa uzalishaji wa kilimo, uhaba wa chakula, mafuta na dawa, mfumuko mkubwa wa bei (hyperinflation) uliofikia viwango vya mamilioni ya asilimia na ukosefu mkubwa wa ajira.

Pia Zimbabwe ilipoteza upatikanaji rahisi wa mikopo kutoka taasisi za kimataifa kama IMF na Benki ya Dunia, jambo lililozidisha matatizo ya kifedha ya serikali.

Suluhisho

Baada ya Zimbabwe kuona uhusiano wake na mataifa ya Magharibi umezorota, ndipo ilianza kuimarisha ushirikiano na China, Urusi na mataifa mengine ya Asia. Hii ilijulikana kama sera ya "Look East". Hata hivyo, haikusaidia kuurejesha uchumi kwenye hali yake.

Tangu kuingia madarakani kwa Rais Emmerson Mnangagwa mwaka 2017, sehemu kubwa ya vikwazo vya EU imeondolewa, huku Marekani ikibadilisha baadhi ya hatua zake za zamani na kuendelea kulenga watu na taasisi zinazohusishwa na rushwa au ukiukwaji wa haki za binadamu. Serikali ya Zimbabwe imekuwa ikifanya juhudi za kurekebisha uhusiano wake na nchi za Magharibi na taasisi za fedha za kimataifa.
 
Mambo Mengine Hutakiwi hata kwenda Marekani mkuu.
Labda kama Unaenda kuuza Raslimali za watanganyika.

Hao Jamaa wameorodhesha Mambo yote yanayotunyima Msaada, Ila na mimi nitawaka yangu ambazo ndio sababu kuu.

1. Utekaji.
2. Mauaji.
3. Kupotezwa kwa watu.
4.Uchaguzi Haramu.
5. Kubaka Demokrasia.
6. Uhuru wa Vyombo vya Habari.
7. Rushwa.
8. Ufisadi.
9. Maonevu kwa akina Lissu.
10. Upumbavu wa samoya.

Wazungu mabalozi wao wamejaa hapa kwetu wanasema yote yanayo Endelea.

Mungu wabariki wazungu
 
Natamani mh Samia awe na ziara kwenye mataifa ya Magharibi ikiwemo Marekani
 
Leo ndio nimemuona hadi Makombo kwa mara ya kwanza mtandao wa X kwenye account ya ubalozi wa Italy ambayo bado anaitumia bila kubadili handle, ameamua aitumie kujibu post za senators na kurepost habari za ubalozi.
 
Natamani mh Samia awe na ziara kwenye mataifa ya Magharibi ikiwemo Marekani
Teh teh aende na hotuba alizo andikiwa na Kabudi akishirikiana na yule maarufu kama 'Mzee wa hovyo' Chindi Chonde.
 
Ni nani aliwaambia CCM kuna wana ushawishi wa kubadilisha sera ya nje ya Marekani.
Ni yule kiheremswede bw.Kombolela.Anadhani kulegeza ulimi wakati wa kuongea ndiyo sifa ya ushawishi na "loop hole" ya udanganyifu kwa watu werevu na wenye taarifa.Badala ya kutubu na kurekebisha maovu yao,wao wanaenda kuchochea moto zaidi.
 
Back
Top Bottom