Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri vipindi vya mvua katika baadhi ya maeneo ya mikoa 25 nchini katika siku 10 zijazo, huku maeneo mengine yakitarajiwa kuendelea kuwa makavu.
TMA imesema katika kipindi hicho, mifumo ya shinikizo la juu la hewa iliyopo kaskazini mwa dunia, ikiwamo Azores na Siberia, inatarajiwa kuendelea kuimarika, huku mifumo iliyopo kusini mwa dunia, ikiwamo St Helena na Mascarene, ikitarajiwa kudhoofika kidogo.
Vilevile, joto la bahari katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi, linalojumuisha pwani ya Afrika Mashariki, linatarajiwa kuwa juu ya wastani ikilinganishwa na eneo la mashariki mwa bahari hiyo, linalojumuisha pwani ya Indonesia.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA ya leo, Alhamisi, Oktoba mosi, 2026, hali hiyo inatarajiwa kuimarisha upepo wenye unyevunyevu kutoka baharini kuelekea maeneo ya ukanda wa Pwani ya Tanzania na maeneo jirani, hivyo kuchochea mifumo ya hali ya hewa inayosababisha mvua katika maeneo hayo.
Soma Pia: TMA: October kuna mvua za El Nino zinakuja
“Aidha, mifumo ya hali ya hewa iliyopo katika ukanda wa Ziwa Victoria inatarajiwa kuimarisha kwa vipindi vichache mifumo inayosababisha mvua katika maeneo hayo,” imesema TMA.