Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,108
- 10,191
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mwenendo wa hali ya hewa kwa Mikoa ya Kaskazini inayopakana na nchi ya Kenya, ikieleza kuwa kiwango hafifu cha upepo hakiwezi kuhamisha nzige kutoka nchi hiyo kuingia Tanzania.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Februari 11, 2020 na meneja wa kituo kikuu cha utabiri cha TMA, Samweli Mbuyaa katika mkutano wa wadau wa hali ya hewa uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mbuya amesema upepo unaovuma sasa ni wa kasi ya kilomita 20 hadi 25 kwa saa na ili nzige wahame unatakiwa kufika kilomita 28 kwa saa.
"Upepo ukitulia nzige huweka makao kwa hiyo kwa sasa kuna kiwango kidogo cha upepo kuja Tanzania na hii ni hali inayotarajiwa kwa siku kumi zijazo yaani kuanzia Februari 11 hadi 21,2020," amesema Mbuya.
Amewataka wataalamu wa sekta husika kufuatilia taarifa ya hali ya hewa ili kuweza kukabiliana na nzige.
Mkurugenzi wa TMA, Agness Kijazi amesema utabiri huo haumaanishi nzige hao wapo nchini Tanzania.
Amesema unalenga mamlaka husika kuchukua tahadhali japo kwa muda huo wa siku kumi za utabiri, kwamba upepo unaweza kuhama usiwe na mwelekeo wa kuja nchini.
"Hawa wadudu ili waruke lazima kuwe na mazingira ya kuruka kwa hiyo taarifa hii inalenga kujiandaa," anasema Mbuya.
Chanzo: Mwananchi