SoC01 Tokomeza "UKIMWI"

SoC01 Tokomeza "UKIMWI"

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Oct 6, 2018
Posts
10
Reaction score
45
Pima ➡️ Jitambue ➡️ Ishi

Unaweza kuishi na maambukizi ya VVU lakini usiwe na UKIMWI;

Inawezekanaje?
VVU
ni Virusi Vinavyosababisha UKIMWI.
UKIMWI ni Upungufu wa Kinga Mwilini.

Mtu huambukizwa virusi vya Ukimwi (VVU) na sio UKIMWI, baada ya kupata maambukizi ya VVU asipochukua hatua ndio itapelekea kupata UKIMWI.

Unashauriwa kupima na kujua hali yako ya afya. Endapo kama utabainika kuwa na maambukizi ya VVU utashauriwa njia sahihi zitakazokuwezesha kulinda afya yako na kuzuia kupata UKIMWI.

Fahamu Jinsi VVU Inavyoweza Kushambulia Afya Yako
Mtu anapopata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), hivi virusi vinaanza kushambulia kinga yake ya mwili, kwa kadri atakavyoendelea kuishi na hivi virusi bila kuchukua hatua yoyote virusi vitaendelea kuzaliana kwenye mwili wake, kinga yake ya mwili itaendelea kushambuliwa na kuanza kupungua. Kinga ya mwili itakapopungua kabisa mwilini basi huyu mtu atapata Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI).
Baada ya kupata UKIMWI (Upungufu wa Kinga Mwilini), mwili wake utakua hauna kinga ya kutosha kujikinga na magonjwa nyemelezi na hivyo itapelekea aanze kupata Homa za mara kwa mara, Magonjwa ya mfumo wa hewa ikiwemo Kikohozi kikali, Kifua kikuu (TB), Kupungua uzito, Kuharisha, Magonjwa ya ngozi na Kuvimba Tezi.
Hivyo afya yake kiujumla itadhoofika.

Jinsi Unavyoweza Kuambukizwa VVU.
VVU inaambukizwa kwa kujamiiana na mtu mwenye maambukizi bila kutumia kinga, kuchangia vitu vyenye ncha kali na mtu mwenye maambukizi na pia maambukizi ya kutoka kwa mama mjamzito mwenye maambukizi kwenda kwa mtoto kipindi akiwa tumboni au wakati wa kujifungua au wakati wa kunyonyesha.

Kuwa na Afya Nzuri Hata Baada ya Kupata Maambukizi ya VVU;
Anza ARV Mapema
Dawa za ARV zinasaidia kufubaza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kuzuia virusi visiendelee kuzaliana kwenye mwili wako, hivyo huzuia kinga yako ya mwili isiendelee kushambuliwa.

Tumia ARV Kwa Usahihi
Unapotumia dawa za ARV kwa usahihi virusi vya ukimwi (VVU) vitafubaa, virusi vya ukimwi (VVU) vikifubaa uwezekano wa kumuambukiza mwenzi wako unakua mgumu hivyo mnaweza kukutana kimwili bila kumuambukiza na pia mnaweza kuzaa watoto wasiokuwa na maambukizi na pia kinga yako ya mwili itaendelea kuimarika.

Hakikisha Mwenzi Wako Anapima
Unapogundulika una maambukizi ya VVU ni vyema kumtaarifu mwenzi/wenzi wako ili nao wapime na kujitambua.
Mwenzi/wenzi wako wanaweza kuishi na maambukizi ya VVU bila kuonesha dalili, iwapo mwenzi/wenzi wako watabainika kuwa na maambukizi ya VVU wataanzishiwa ARV mapema na kupunguza uwezekano wa kuambukiza wengine.
Unapokutana na mwenzi wako kimwili hakikisha mnatumia kinga mpaka pale itakapothibitishwa kuwa virusi vyako vimefubaa.

Pima Wingi wa VVU Mwilini
Kupima wingi wa VVU mwilini kunakuwezesha kujua kiwango cha VVU kilichopo mwilini na kutambua mwenendo wa tiba yako.

Unaweza kuishi na maambukizi ya VVU na bado ukawa na afya nzuri na ukaendelea kufanya shughuli zako za maisha kawaida na hautafikia kwenye UKIMWI kama utazingatia matumizi sahihi ya ARV.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom