Waziri Masha aipe Barrick siku Saba!
Chesi Mpilipili Disemba 24, 2008
Raia Mwema Muungwana ni Vitendo
KUNA suala muhimu linalohusu usalama wa raia wa nchi ambalo mpaka wakati makala hii inaandaliwa lilikuwa halijapewa uzito unaostahili na kuna hatari likaishia juu juu bila kutolewa majibu yanayostahili uzito wake.
Wiki iliyopita kulikuwa na taarifa za kushitua kwenye baadhi ya vyombo vya habari nchini zinazohusu Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ofisi ya Mwanza kuzuia kwa muda shehena ya Kampuni ya Uchimbaji dhahabu ya Barrick kwenye Uwanja wa ndege wa jijini humo.
Mamlaka hiyo ililazimika kuzuia shehena hiyo iliyokuwa na uzito wa tani 1.4 na kulipiwa ushuru wa shilingi milioni 144 kutokana na kilichoelezwa kuwa ni shehena hiyo kubainika kuwa ni pamoja na mabomu ya kutupa kwa mkono, mabomu ya machozi na risasi za moto.
Meneja forodha wa TRA Mkoa wa Mwanza, Leopold Kihumu, amekaririwa na gazeti moja la kila siku la Kiswahili akisema kuwa wameshirikiana na Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ, Usalama wa Taifa na wao TRA.
Akaongeza ya kuwa shehena hiyo ilitumia taratibu zote za kuombewa kibali na ndiyo maana baada ya kujiridhisha na ukaguzi iliruhusiwa kuendelea na safari.
Kuanzia hapa maelezo haya yanaanza kukanganya. Meneja huyu anaposema kuwa 'baada ya kujiridhisha na ukaguzi shehena hiyo iliruhusiwa kuendelea na safari' anapaswa kutufafanulia alikuwa na maana gani.
Kutokana na maneno yake mwenyewe, hapa tunazungumzia shehena iliyoingizwa nchini ambayo imekutwa na mabomu ya kutupa kwa mkono, mabomu ya machozi na risasi za moto.
Je, tuelewe kwamba kwa shehena hiyo kuruhusiwa kuendelea na safari yake kampuni ya Barrick ina kibali cha kuingiza nchini mabomu ya machozi, risasi na mabomu ya kutupa kwa mkono ambayo tunajua kuwa yanatumika kwenye vita?
Je, kwa shehena hiyo kuruhusiwa kuendelea na safari sasa tuamini kwamba sheria za nchi zinaruhusu makampuni ya wawekezaji kuingiza silaha nchini?
Tuamini kwamba Barrick wana kibali kinachowawezesha kuingiza silaha kama hizo na ndiyo maana baada ya 'ukaguzi wa kujiridhisha wa shehena yao' waliruhusiwa kuichukua?
Wakati meneja huyo akithibitisha kuwapo kwa mabomu na risasi kwenye shehena ya Barrick, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Khamis Bhai, amenukuriwa kwenye habari hiyo hiyo akisema kuwa taarifa aliyopewa na Afisa Upelelezi wa Mkoa, Augustine Olomi, ilisema kuwa shehena hiyo ilikuwa ni ya baruti za kulipulia miamba.
Maneno hayo yameungwa mkono pia na meneja uhusiano wa kampuni hiyo Teweli Teweli ambaye amenukuliwa na gazeti lililotoa taarifa hiyo akisema kuwa Barrick haina sababu yoyote ya kusafirisha shehena kama hiyo kwa vile haina matumizi katika shughuli za kampuni hiyo za kuchimba dhahabu.
Ni rai yangu kwamba kauli hizi za kukanganya kutoka kwa wahusika wa suala hili hazipaswi kuachwa zikayeyuka kirahisi rahisi hivi kwa vile zinahusiana na usalama wa umma.
Inashangaza mno kwa maofisa wa idara za serikali ambao mmoja wao anasema walishirikiana kuifanyia uchunguzi shehena hiyo wawe na majibu yanayotofautiana, mmoja akisema ni shehena ya mabomu na risasi huku mwingine anasema ni baruti za kupasulia miamba.
Tungependa kufahamishwa inakuwaje Afisa Upelelezi wa mkoa apeleke ripoti kwa kaimu Kamanda wa Polisi kwamba kilichomo kwenye shehena ilivyokuwa imezuiwa uwanja wa ndege ni baruti za kupasulia miamba huku meneja wa forodha wa TRA anasema kuwa shehena hiyo ina mabomu ya kutupa kwa mkono, mabomu ya machozi na risasi?
Ina maana kuwa baada ya uchunguzi wa shehena hiyo ambayo tunaambiwa kuwa ulishirikisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi JWTZ na Usalama wa Taifa kuliandikwa ripoti mbili tofauti, TRA walioitisha uchunguzi huo wakisema shehena hiyo ilikuwa na mabomu ya kutupa kwa mkono na risasi huku ofisi ya Upelelezi ikisema kuwa shehena hiyo ni baruti za kulipulia miamba?
Ni majuzi tu kampuni hiyo ya Barrick ilikuwa kwenye vichwa vya habari kutokana na wanachi wanaosadikiwa kufikia 400 kuingia kwenye mgodi wa kampuni hiyo, North Mara, ulioko Nyamongo na kufanya uharibifu mkubwa wa mali za kampuni ambapo mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita wananchi 10 walikwisha kukamatwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo.
Tumeelezwa kuwa katika tukio hilo walinzi wa mgodi huo waliokuwa zamu waliamua kukimbia na kuwaacha wanachi hao wakiendelea na uharibifu huo hadi pale Kikosi cha Polisi wa Kutuliza Ghasia walipofika mgodini hapo na kuzima ghasia hizo.
Imeshangaza kidogo kwamba wakati taarifa za kuvamiwa kwa mgodi wa Barrick zikitamba kwenye kurasa za mbele za vyombo vyetu vya habari, hizi za kampuni hiyo kushukiwa kuingiza nchini zana za kivita nchini, iwe kweli ama si kweli, hazikupata 'bahati' hiyo. Tutafakari.
Tunapopata taarifa zinazohuzu kampuni hiyo kuingiza nchini shehena ambayo inajumlisha mabomu ya kutupa kwa mkono yanayotumiwa kwenye vita na yale ya machozi yanayotumiwa kuzima ghasia pamoja na risasi tunapata wasiwasi kuhusu usalama wa umma.
Kama maneno ya Meneja wa Forodha wa TRA Mkoani Mwanza, Leopold Kihumo kwamba shehena hiyo ni ya mabomu ya vita na risasi za moto ni kweli basi tunapaswa kujiuliza kampuni ya Barrack inataka kutumia mabomu hayo na risasi hizo kwa ajili gani wakati zana hizo hazihusiani kwa namna yoyote ile na uchimbaji madini?
Nadhani Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha anapaswa kuwahoji haraka maafisa wa idara zake Mkoani Mwanza na kujua, kisha kutufahamisha, ukweli wa suala hilo na yule atakayebainika kutoa taarifa za kupotosha umma achukuliwe hatua kali zinazostahili.
Hapa nina maana ya yule aliyesema shehena hiyo ina mabomu ya kutupa kwa mkono na risasi na kumbe hakuna kitu kama hicho na kwa maana hiyo kutuweka roho juu bure ama yule aliyesema shehena hiyo ni ya baruti za kupasulia miamba tu na kumbe ina risasi na mabomu na hivyo kuuweka rehani usalama wetu.
Mkanganyiko huu unazidi zaidi pale meneja forodha huyo anaponukuliwa akisema kuwa 'baada ya ukaguzi walipendekeza shehena kama hizo ziwe zinaagizwa na wakala wa serikali wanaojihusisha na silaha na si mwekezaji'.
Maneno haya yanaondoa chembe ya wasiwasi juu ya kuwapo ama kutokuwapo kwa zana hizo kwenye shehena hiyo. Meneja huyo asingeweza kutoa hitimisho kama hilo kama kusingekuwapo na silaha hizo.
Tunadhani kuwa Waziri Masha anapaswa pia kuipa Barrick siku saba za kulitolea maelezo ya kina suala hili ili isije kuwa kwamba kila mwekezaji akawa na kajeshi kake ka kumlinda yeye na mali zake.
Wakati yote hayo yakifanyika, ni vema pia tukaangalia kwa undani kiini cha tatizo la wananchi wetu kuvunja sheria kwa kuvamia mgodi wa muwekezaji uliopo kihalali. Tusingependa hii iwe ni rasha rasha inayoashiria gharika. Ni wazi kuwa yapo mambo mengi ambayo hayawafurahishi wananchi wetu wanaozunguka maeneo ya migodi iliyopewa wawekezaji. Ni jukumu letu kuondoa hali hii inayoashiria upotevu wa amani.
Tuchukue 'ukurasa wa uzoefu' kutoka kwa ndugu zetu wa Nigeria ambako maeneo yao yanayotoa mafuta hayana amani na mara nyingi yamekuwa uwanja wa mapambano na utekaji nyara wa wafanyakazi wa makampuni ya kimataifa ya mafuta yanayochimba mafuta eneo hilo.
Hii ni kutokana na wananchi wa maeneo hayo, hasa wale wa kabila la Ogoni, kuona hawatendewi haki na serikali yao na makampuni hayo yanayopata faida kubwa huku yakiwaacha wao katika umasikini na mazingira yaliyochafuliwa na uchimbaji huo.
Blogu: Chesimpilipili.blogspot.com