Shehena ya mayai feki yakamatwa Dar
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, imekamata shehena ya mayai yakiwa ndani ya lori katika eneo la Kitunda Dar es Salaam ambayo yalikuwa yakisafirishwa bila kibali. Shehena hiyo iliyokuwa na zaidi ya trei 500, ilikamatwa siku chache baada ya vyombo vya habari kuripoti kuingizwa kwa mayai feki kutoka nchini Kenya ambayo yanauzwa kwa bei rahisi hali inayozua shaka kwa walaji.
Tanzania Daima ilishuhudia shehena hiyo ikiwa kwenye lori lenye namba za usajili T 423 BCQ likiwa limeegeshwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Mayai hayo huuzwa kati ya sh 4,000 hadi 5,000 kwa trei moja wakati bei halali sokoni kwa sasa ni kati y ash 6,000 hadi 7,000 kwa trei. Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa wizara hiyo, Dk. Winston Mleche, alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa, walisema mayai hayo ni mali ya kampuni ya Morning Fresh kutoka Mkuranga mkoani Pwani na kwamba wanayazalisha huko.
Kutokana na hali hiyo waziri mwenye dhamana, Dk. David Mathayo, ameagiza maofisa wake kwenda Mkuranga kufanya uchunguzi wa masuala mbalimbali ikiwemo kujua kama mayai hayo yanazalishwa huko au la. Dk. Mleche alikiri kuwa hata ofisa mifugo wa wilaya ya Mkuranga hana taarifa za kampuni hiyo iliyotajwa kuwa mmiliki wa mayai yaliyokamatwa kwani haina uwezo wa kuzalisha kiasi kikubwa kama hicho.Alisema kuwa hata wanapokwenda kwenye eneo la kampuni, maofisa hukataliwa kuingia ndani vinginevyo watimize masharti likiwemo la kufanyiwa uhakiki wa kuoga kabla hawajaingia kiwandani jambo ambalo hupingwa na maofisa hao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri Mathayo alisema hivi sasa kuna taarifa za kuingizwa kwa mayai mengi kutoka nchi jirani hali ambayo husababisha soko la ndani kudorora.Kwa mujibu wa Dk. Mathayo, serikali ilishapiga marufuku uingizwaji wa mayai ya kula kutoka nje ili kudhibiti pia magonjwa na kwamba hata leseni ya aina hiyo hawatoi badala yake imeruhusu kuingizwa nchini mayai ya mbegu pekee.Pamoja na mambo mengine alisema hakuna upungufu wa mayai nchini hivyo hakuna sababu ya kuendelea kulididimiza soko la ndani na kuwanufaisha wengine.
Hivi karibuni kumeripotiwa kuingiliwa kwa soko la mayai hapa nchini kutokana na kuingizwa kwa mayai kutoka Kenya hali inayosababisha wafanyabiashara wa nchini kupata wakati mgumu.Mayai hayo yanaelezwa kuwa siyo makubwa kama yanayopatikana nchini na yanapovunjwa hayana kiini na baadhi maji yake yamechanganyika na vitu mithili ya nyuzi zenye rangi nyekundu. Mayai hayo yanapatikana kwa wingi maeneo ya Kariakoo na Gongo la Mboto na yanauzwa kwa wingi kwa wafanyabiashara wa vyakula jijini Dar es Salaam
Source. Tanzania Daima