DHANA YA UBEBAJI MIZIGO KWA MUJIBU WA SHERIA ZA TANZANIA Je, sheria inasemaje kuhusu kubeba mizigo? Je, ni kosa kutumia gari langu kubeba mizigo? Kuna sheria mbili tutakazoziangalia hapa, nazo ni Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 ya sheria za Tanzania, na kanuni za SUMATRA za usafirishaji mizigo za mwaka 2012 KANUNI ZA SUMATRA [TRANSPORT LICENSING (GOODS CARRYING VEHICLE) REGULATIONS 2012 Kifungu cha 2 cha kanuni kinatafsiri gari gari la kubebea mizigo (Goods carrying vehicle) kama gari ambalo limetengenezwa au kufanyiwa mabadiliko kwaajili ya kubebea bidhaa au lililotengenezwa au kurekebishwa kwaajili hiyo. Kanuni hazisemi nini maana ya mzigo.
Nadhani hii inaweza kuwa inatokana na dhana kwamba kila mtu anajua mzigo ni nini. Kwa mujbu wa kanuni ya 3 mtu yeyote mwenye gari ya mizigo kwaajili ya kufanya shughuli ya kubeba mizigo ni sharti awe na leseni ya kubebea mizigo. Kwa mujibu wa kanuni ya 4 leseni hiyo ataipata baada ya kuiomba kutoka SUMATRA.
Kanuni ya 4(2) inataja mahitaji ya vitu ambayo mwomba leseni anatakiwa kwenda navyo SUMATRA ili kupata leseni. Vitu hivyo ni pamoja na kadi ya gari,bima,ripoti ya ukaguzi, majina ya nakala za leseni ya madereva wa magari hayo,picha za mwenye gari, nakala ya mkataba wa dereva. Kwa mujibu wa kanuni ya 7 iwapo mamlaka itaridhika na nyaraka zilizowasilishwa basi itampa leseni mwomba leseni ya kusafirisha mizigo. Muda wa leseni ni mwaka mmoja na inaweza kuhuishwa (renewal) Kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 26, Mamlaka itatoa cheti cha ruhusa ya kuendesha gari kwa dereva atakayeendesha gari hilo.
Cheti hicho kitataja namba ya leseni ya dereva,TIN,tarehe ya kuzaliwa,picha ya dereva,jina na anwani ya dereva, jina la shule ya udereva aliyosomea. Masharti kwa dereva na matendo yaliyokatazwa Kwa mujibu wa kanuni ya 27 dereva atazingatia yafuatayo: (a) Kuendesha kwa spidi iliyokubaliwa; (b) Kutobeba abiria kwenye gari la mizigo; (c) Kutozidisha mizigo kinyume na uzito wa gari husika Kwa mujibu wa kanuni ya 28, dereva anakatazwa:
a) Kutumia lugha mbaya au za matusi kwa wateja (b) Kuwazuia wengine barabarani (c) Kuendesha akiwa na kilevi (d) Kuendesha kwa pupa na kutojali kinyume na sheria ya usalama barabarani (e) Kuegesha gari mahali pasiporuhusiwa (f) Kuendesha gari katika barabara ambazo uzito unaoruhusiwa ni wa chini kuliko ule wa gari (g) Kuwanyanyasa wateja (h) Kutumia simu wakati anaendesha Kushindwa kutekeleza masharti ya kanuni ya 27 na 28 kunaweza kupelekea dereva kupigwa faini ya shilingi laki moja au kifungo cha miezi mitano jela au vyote kwa pamoja.
Hitimisho Kwa ufupi sheria hii inawahusu Zaidi wale wanaomiliki magari kwaajili ya kufanya biashara au shughuli za ubebaji mizigo kwa kutumia magari yaliyotengenezwa maalumu kwaajili ya kubebea mizigo. Na hasa hasa wale wanaofanya bishara kwa kutumia magari hayo. Japokuwa sheria hapa imeweka masharti ya jumla bila kujali kwamba mwenye gari la mizigo anafanyia bishara au la. Kwa mujibu wa kanuni ya 35(1) polisi na maafisa wa SUMATRA wamepewa mamlaka ya kusimamisha magari haya ya mizigo na kukagua iwapo yanatimiza masharti ya kanuni hizi au kukagua leseni ama nyaraka nyingine inayotakiwa kuwemo kwenye gari.
Je, sheria hii inaelekeza lolote kuhusu namna ya kubeba mizigo au aina gani ya mizigo ibebwe? Je, sheria hii inakataza gari fulani kubeba mizigo? Jibu la maswali yote haya mawili ni hapana, sheria hii inajikita kwenye utoaji wa leseni tu au vibali kwaajili ya magari yanayobeba mizigo, na kwamba magari haya yanatakiwa kuzingatia sheria nyingine wakati wa kufanya kazi ya kubeba mizigo, mathalani sheria ya usalama barabarani, sheria ya ubebaji kemikali, nk. SHERIA YA USALAMA BARABARANI, SURA YA 168 (RTA,1973) Hii ndiyo sheria mama ya usalama barabarani.
Kwa mujibu wa kifungu cha 2 cha sheria hii tafsiri ya nini maana ya gari ya mizigo inafanana sana na ile iliyotolewa kwenye kanuni za SUMATRA za magari ya mizigo,2012. Kama zilivyo kanuini za SUMATRA sheria hii haitoa maana ya neno “mizigo au bidhaa” wala hakuna popote, kuanzia kifungu cha 1 hadi cha 118 inapokataza magari ya aina fulani kubeba mizigo.
Je, nini kinachokatazwa au kuelekezwa na sheria hii? [MAMBO AMBAYO DEREVA ALIYEBEBA MZIGO ANATAKIWA KUZINGATIA KWA MUJIBU WA SHERIA] 1. Sheria hii inataka gari lolote, likiwemo la mizigo au tela lake liwe zima, yaani linafaa kwa matumizi ya barabarani kwa mujibu wa kifungu cha 39(1) na (2) ili lisihatarishe maisha ya walimo kwenye gari na watumiaji wengine wa barabara. Kipimo cha ubovu wa gari kwa mujibu wa kifungu cha 39 ni sentensi hii “…not likely to be a danger to the persons travelling on the motor vehicle or trailer or to other users of the road.”
Yaani uendeshaji wa gari husika katika hali liliyopo usiweze kuwa hatari kwa watu wanaosafiri na gari hilo au watumiaji wengine wa barabara.” 2. Kifungu cha 39(3) kinapiga marufuku gari lolote au trela lake kutumika barabarani ikiwa mgawanyo, ufungaji, na urekebishaji wa mzigo uliobebwa unafana gari hilo kuwa hatari kwa watu wanaosafiri na gari hilo au watumiaji wengine wa barabara. [(3) No motor vehicle or trailer shall be used on a road if the distribution, packing and adjustment of the load carried is such as to make it a danger to persons travelling on the motor vehicle or trailer or to other users of the road.] 3. Kifungu cha 39(4) kinaeleza kwamba, kwa minajili ya kifungu kidogo cha 2 na cha 3 cha kifungu cha 39, watu wanaosafiri kwenye gari ni sehemu ya mzigo.
[travelling on a motor vehicle or trailer shall be deemed to be part of the load:] 4. Kifungu cha 39(2) kinapiga marufuku gari kubeba mzigo mkubwa zaidi ya uzito uliowekwa na mtengenezaji wa chesisi ya gari au kuzidisha uzito Zaidi ya ule uliotengenezwa kwa gari husika. Kifungu cha 39A(2), kinataka mzigo wowote uliopakiwa kwenye gari uwe umepangwa na kuzingirwa (secured) vizuri ili kuuzuia mzigo huo: (a) Kuwadhuru watu au kusababisha madhara kwa mali binafsi au ya umma na kuanguka au kuburuzika barabarani; (b) Kuzuia uoni wa dereva au kuathiri uwiano wa gari linapoendeshwa; (c) Kusababisha kelele, vumbi, au kusababisha kadhia nyingine zinazoweza kuepukwa (d) Kufunika taa,indiketa, viakisi mwanga(reflectors), sahani za namba, na alama za nchi ya usajili wa gari, au kuzuia kuonekana kwa alama yoyote inayotolewa kwa mkono.
5. Kifungu cha 39A(3) kila dereva atahakikisha kuwa viunganisha vyote kama vile minyororo,Kamba, waya, na bati zilizotumika kufunga au kuzingira mzigo zimefungwa thabiti kuweza kuushikilia mzigo. 6. Kifungu cha 39A(4) iwapo mzigo uliobebwa umetokeza nyuma au mbele kiasi cha kutoonekana na madereva wengine, dereva atahakikisha eneo hilo lililojitokeza linawekewa alama itakayofanya uonekane. [ hii ndio sababu watu huweka kitambaa chekundu au taa inayowaka na kuzima] 7. Kifungu cha 39A(5), dereva ambaye gari lake limetengenezwa mahsusi kwajili ya kubeba mizigo, anaweza katika mazingira fulani maalumu yaliyoelezwa na sheria hii, kubeba abiria kwenye nafasi iliyowekwa maalumu kwaajili ya mizigo.
[ Hata hivyo katika sheria mama mazingira hayo hayatajwi kinaganaga] Kwa maelezo haya, je gari ndogo za chini ya tani 3.5 ambazo hazikutengenezwa kwaajili ya kubeba mizigo mikubwa, kama vile, saloon, station wagon, nk, haziruhusiwi kubeba mizigo? JIBU ni hapana, hakuna popote kwenye sheria panapokataa gari hizo kubeba mizigo, ili mradi tu dereva atakuwa amezingatia msharti ya kifungu cha 39 na 39A cha sheria ya usalama barabarani.
Kwa mantiki hiyo madereva wanaopigwa faini kwa kubeba mizigo ndani ya siti za abiria wa gari ndogo, mfano umebeba boxi mbili zenye laptop kwenye saloon car seat za nyuma, je utakuwa umetenda kosa? Jibu ni hapana utakuwa hujatenda kosa, ili mradi tu mzigo huo umekaa salama kwenye siti husika kiasi kwamba hauwezi kusababisha uione mbele au nyuma kwa kutumia side mirror au driving mirror au windscreen.
Kwa hiyo hataukipigwa faini kosa pale sio kubeba mizigo kwenye gari isiyo ya mizigo bali kubeba mizigo kwa njia ya hatari. Na hatari yenye ni kule kubeba mzigo kiasi kwamba huwezi kuona kwa kutumia vioo vyako, au namba zimefichwa au taa zako zimefichwa au mzigo husika haujafungwa vizuri.
Hitimisho Kwa hiyo hakuna gari inayokatazwa kubeba mzigo ili mradi tu usalama umezingatiwa, kinachokatazwa ni KUBEBA MZIGO KWA NJA YA HATARI au kwa lugha nyingine KUHATARISHA WALIOMO KWENYE GARI AU WATUMIAJI WENGINE WA BARABARA. Ndio maana hizi gari ndogo zina buti au nafasi nyingine kwaajili ya kubebea mizigo. Zipo gari hazina buti ila kwa ndani sehemu ya siti imetengenzwa vizuri kiasi siti zinaweza kukunjwa ikapatikana nafasi ya kuweka mizigo