Lengo la makala haya ni kuonesha kwamba kuendekeza ushirikina au uchawi na waganga wa kienyeji (wapiga ramli) kunaathiri maendeleo ya jamii. Tuachane na hiyo imani maana badala ya kutusaidia kusonga mbele, tunajenga chuki, uadui na moyo wa kulipiza kisasi kwa kuwadhania wengine ndio vyanzo vya matatizo yetu.
Makala hayaongelei tiba asilia (tiba mbadala) au waganga wa tiba asilia wanaofanya kazi nzuri ya kutibu wagonjwa wenye maradhi mbalimbali kwenye jamii.
Miaka ya hapo nyuma mauaji ya ndugu zetu albino na wazee yalishika kasi sana, kiasi cha kuchafua sifa nzuri ya taifa letu. Wateja wa viungo vya albino na wahusika wa mauaji hayo waliamini viungo vya albino ni dawa ya kujipatia utajiri wa haraka, hasa kwa shughuli za uchimbaji madini migodini na uvuvi Kanda ya Ziwa na maeneo mengine nchini. Tamaa ya pesa iliwekwa mbele zaidi ya hadhi ya utu na kugeuza viungo vya binadamu wenzetu kuwa bidhaa za kuuzwa na kujipatia pesa.
Kulingana na bei ya kiungo kimoja kuwa kubwa sana (angalia Kipindi maalum cha tatu kuhusu Siku ya Albino ya Kimataifa--Hatma yetu sio ndoto - china radio international au Kiungo kimoja cha albino shilingi milioni 600), ni dhahiri wateja wa viungo vya albino hawakuwa watu wadogo, bali watu wakubwa na wenye pesa. Ili biashara zao zifanikiwe zaidi waliona ni heri wajipatie mali au utajiri kwa njia hii haramu, ambayo imelifanya taifa letu lionekane la ajabu, lisilo la kistaarabu machoni pa mataifa mengine duniani.
Ni uchungu ulioje kwa ndugu na jamaa kuwapoteza wapendwa wao kwa sababu tu ya kuamini kwamba viungo vyao vinaleta utajiri! Ni uchungu ulioje kuwafanya baadhi ya ndugu zetu albino waishi wakiwa wamepoteza baadhi ya viungo vyao na ni hofu iliyoje kuishi katika jamii ambayo baadhi ya wanajamii wanaamini viungo vya albino ni dawa ya kujipatia mali! Ni uchungu ulioje pia kwa familia zao zilizoachwa katika hali ya hofu na dhiki? Ni kweli taifa limepoteza sehemu ya nguvu kazi yake katika mazingira ambayo haikutakiwa iwe hivyo.
Leo hii mauji ya albino na wazee yamepungua kwa sababu ya kukamatwa kwa wahusika na wauaji waliokuwa wakitekeleza huo unyama kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria. Inawezekana nia ya kuendelea na biashara hiyo kwa baadhi ya watu bado ipo, lakini siyo kama ilivyokuwa hapo nyuma, ambapo karibu kila baada ya siku kadhaa vyombo vya habari viliripoti matukio ya mauaji ya albino au albino kukatwa baadhi ya viungo vyao na wakataji kuondoka navyo.
Kuna baadhi ya maeneo vyombo vya habari viliripoti pia mauaji ya wazee wenye vipara na akina mama wanaonyonyesha kwa imani kwamba kichwa cha mzee mwenye upara au titi la mama anayenyonyesha ni mali. Matokeo yake, alibino, wazee wenye upara na akina mama wanaonyonyesha waliwindwa kama wanyama ili wakatwe viungo vyao.
Kwa upande mwingine, baadhi ya watu waliuliwa na kuacha wajane na mayatima, baadhi ya nyumba zao zilichomwa moto na wengine wameachwa wakiwa na majeraha ya kudumu kwa tuhuma za ushirikina au uchawi. Watuhumiwa mara nyingi ni bibi vizee au wazee, ambao macho yao kwa sababu ya kuwa na umri mkubwa ni mekundu na ngozi yao imekauka na ni ngumu na pia kwa sababu ya shida ya kutosikia vizuri wakisalimiwa hawaitikii, huku wakidhaniwa kuwa na kiburi na hawawatakii watu wengine mema.
Katika baadhi ya matukio yaliyoripotiwa na vyombo vya habari baadhi ya wazee waliuawa kwa kuchomewa ndani ya nyumba zao wakiwa wamelala usiku, baadhi walivamiwa na kukatwa mapanga hadi kufa au kufukiwa kwenye shimo wakiwa hai. Wengine wanaoadhibiwa kikatili ni wale wanaodhaniwa kuanguka kutoka kwenye ungo wakati wakisafiri kichawi angani baada ya kuzidiwa “nguvu za giza” na wachawi wenzao.
Hali hii imekuwa ikiwafanya wazee wajione hawafai kuishi au waishi kwa hofu, wakiwaona vijana kama maadui wao. Vijana nao wanawaona hao wazee kama maadui wao. Watuhumiwa wa kesho wa uchawi ni vijana ambao leo wao kwa sababu ya nguvu walizonazo na hawajazeeka wanawatuhumu wazee kwa sababu ya kuzeeka. Lakini je, ni nani anayezaliwa na kukua na hawezi kuzeeka?
Kwa hiyo, ushirikina au uchawi umeathiri sana maendeleo ya jamii katika baadhi ya maeneo. Kisiwa cha Ukerewe, Mwanza, ni moja ya maeneo hayo. Kitu ambacho kimeanza kuleta mabadiliko kwa vijana ni kuona kwamba wengi wa wale waliokuwa wakituhumiwa kuwa ni wachawi wameshafariki dunia. Zamani watu waliogopa kuvaa vizuri au kujenga nyumba bora, wakihofia kurogwa. Lakini kwa sasa vijana wameanza kuwa na ushindani wa kujenga nyumba bora, ingawa tuhuma za uchawi zimetoka kwa wazee na kuhamia kwa ndugu wa karibu kwa sababu ya ndugu kukosa kuelewana au kuwa na mgogoro wa ardhi.
Katika baadhi ya familia, mtu akiugua, akipata ajali, akipigwa na radi au akifariki dunia, tuhuma zinaenda kwa ndugu: kaka au dada mtu, baba mdogo au mkubwa, mjomba au shangazi, babu au bibi, baba mkwe au mama mkwe. Lakini zamani ilikuwa: “Mchawi ni yule bibi kizee au mzee mwenye macho mekundu, ngozi kavu na ngumu.”
Mawakala wa ushirikina au uchawi ni waganga wa kienyeji ambao wanawaaminisha wateja wao kuwa hawafanikiwi kwa sababu ya ndugu au jirani yao, mfanyakazi au mfanyabiashara mwenzao. Yote haya yanasababisha watu kutoaminiana na kuwadhania wengine vibaya. Matokeo yake ni kupandikiza hofu na chuki kwa watu na moyo wa kupenda kulipiza kisasi.
Kukulia katika mazingira ya kuwaona wengine kama maadui wenye lengo la kutumaliza, kunaathiri maendeleo ya familia, ukoo, kijiji, mtaa na jamii kwa jumla kwa kuwaona wengine kama chanzo cha matatizo au majangwa yanayotokea katika jamii. Kwa baadhi ya watu, watoto wake wasipofaulu shuleni, mke wake mjamzito akishindwa kujifungua vizuri au akijifungua watoto wa kike au wa kiume peke yake au kama ni mgumba au amezaa watoto njiti, watoto waliodumaa au waliokufa au mtu akishindwa kupata kazi, kupandishwa cheo au mshahara, mtoto akifukuzwa shuleni au yeye mwenyewe akifukuzwa kazini kwa sababu ya utovu wa nidhamu, chanzo cha hayo yote ni ndugu, jirani, bibi kizee au mzee fulani kijijini au mtaani mwetu.
Kutaka mafanikio kwa njia ya mkato au kupata majibu rahisi kwa maswali magumu umekuwa ndio utamaduni mpya kwa baadhi ya watu. Watu wengi wanaenda kwa waganga wa kienyeji ili kujua nyota yao ikoje, adui wao ni nani au nani amesababisha maradhi yao au ya ndugu yao, kifo cha ndugu yao, ajali ya majini au barabarani iliyompata ndugu yao, radi, mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na mafuriko katika kijiji chao, nani amesababisha mke wake kufariki wakati wa kujifungua au ndugu yao kufungwa gerezani na kadhalika. Kuendekeza imani au fikira za aina hii hakutusaidii kutatua matatizo yetu, bali kunayasukuma mbele zaidi na kufanya hivyo ni kuchelewesha majibu ya maswali yetu, utatuzi wa migogoro yetu na maendeleo ya jamii.
Matangazo ya waganga wa kienyeji tunayoyaona yamebandikwa maeneo mbalimbali au ujumbe mfupi wa simu tunaopokea ukitutaka kama tunataka pesa za majini au kutajirika tuwasiliane na fulani kwa namba za simu zinazotolewa kwa ajili ya mawasiliano zaidi ni ishara wazi kwamba kuna mahitaji.
Dawa zinazotangazwa mara nyingi ni kama vile dawa ya mvuto kimapenzi, kuongeza mbegu za kiume na kurejesha heshima ya ndoa, kunenepesha au kurefusha sehemu za siri (kwa wanaume), kupandishwa cheo au mshahara kazini, kumwita mtu wa mbali, kuondoa mkosi, kupata kazi, kupata watoto kwa wale wenye matatizo ya uzazi, kufaulu mitihani au usaili, kurudisha ndoa iliyovunjika na zinginezo.
Hivyo, watu wengi sana katika jamii wanaamini kuna watu wana uwezo fulani (wenye “nguvu za giza”) wa kusababisha matatizo ya wenzao na wengine wana uwezo pia wa kuwatambua hao watu wabaya ni akina nani na wanaweza kuwadhibiti kwa kutumia dawa fulani, ikiwa ni pamoja na kuvaa hirizi, kuzindika shamba, nyumba au biashara.
Kwa vile tunazaliwa na kukua tukiwa kwenye jamii ambayo masimulizi ya matukio ya ushirikina au uchawi ni ya kawaida, ni rahisi kuyapokea kama yalivyo na kuyaamini bila kuyathibitisha. Bw Mitchell Robert kwenye kitabu chake African Primal Religions (1977) ukurasa wa 71 anaeleza kwa nini imani ya ushirikina au uchawi ni ya kawaida kwa jamii za Kiafrika.
Anataja vipengele vinne. Kwanza, maradhi na vifo ni vitu vya kawaida katika jamii za Kiafrika. Pili, watu wengi hawana ufahamu mzuri wa kisayansi wa vyanzo vya maradhi na vifo vinavyotokea. Hivyo, ni rahisi sana kuhusisha hayo maradhi na vifo na imani ya ushirikina au uchawi. Tatu, watu wanazaliwa na kukua katika jamii wakisikia mara kwa mara matukio ya ushirikina au uchawi. Katika mazingira kama haya, ni rahisi kuamini yale wengine wanayoyaamini. Nne, watu wanaishi pia kwenye mazingira ambayo ni rahisi kumhisi mtu mwingine vibaya, kumwonea wivu au kumchukia kwa sababu yoyote ile. Hivyo, kwenye jamii ambayo vipengele vyote hivi vinne ni vya kawaida, ni rahisi sana kuwa na imani ya ushirikina au uchawi kwa sababu inasaidia kutoa majibu ya matatizo ambayo jamii ingehitaji majibu yake, lakini hayapatikani.
Kwa hiyo, kama jamii tuna changamoto kubwa ya kutafuta majibu sahihi ya maswali yetu na ufumbuzi sahihi wa matatizo yetu kuliko kukubali majibu rahisi au ufumbuzi usio sahihi wa matatizo yetu. Tuchague njia sahihi itakayotuletea maendeleo kuliko kupoteza muda kwa kufikiria watu wengine ndio vyanzo vya matatizo yetu. Tuachane na ushirikina au uchawi tupate maendeleo.

Upvote
2