CUF Habari
JF-Expert Member
- Dec 12, 2019
- 239
- 234
TUACHE UJINGA, TANZANIA SIYO UINGEREZA!
Mwaka 1997 aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza, John Major alishindwa uchaguzi na kupoteza nafasi yake ya kuendelea kuwa waziri mkuu.
Inadawia kwamba tangu mwaka 1832 hakuna waziri mkuu wa Uingereza ambaye alishindwa uchaguzi kwa kishindo kama John Major.
Kushindwa kwa John major kulishangaza kwa sababu inadaiwa kuwa kati ya mawaziri wakuu wote wa Uingereza, alikuwa anashikilia rekodi ya kuipa Uingereza mafanikio makubwa ya kiuchumi!
Baada ya uchaguzi na kushindwa kwa John Major watafiti walitaka kujua ni kwa nini wapiga kura walimkataa John Major pamoja na kwamba alikuwa ameipa Uingereza mafanikio makubwa ya kiuchumi.
Waingereza wengi walitoa jibu la kijinga kabisa pale walipoulizwa ni kwa nini hawakumchagua.
''HATUPENDI TU SURA YAKE!''. Hilo ndilo lililokuwa jibu lao.
Ukweli ni kwamba Waingereza wanaweza kumudu anasa hiyo ya kuchagua kiongozi kwa kuangalia sura yake. Hii ni kwa sababu Waingereza wote wanapata huduma zote za msingi - elimu, afya, chakula, malazi bila kujali kama wameajiriwa au hawajaajiriwa.
Kwa upande wake Tanzania ni nchi ambayo huduma za msingi bado ni tatizo kubwa kwa wale walioajiriwa, achilia mbali jeshi kubwa lililopo la watu ambao hawana ajira.
Katika mazingira haya ni jambo la kushangaza sana kwamba unakutana na Mtanzania ambaye anakuambia kwamba fulani hafai kuchaguliwa kwa sababu eti 'hana sura ya urais!'
Kwa nchi kama Tanzania kigezo chetu kikubwa cha kupiga kura hivi sasa kinatakiwa kiwe uwezo wa mgombea kututoa hapa tulipo na siyo vinginevyo. Kwani tuko wapi?
TUKO NCHI YA HUZUNI!
Taarifa ya hali ya furaha duniani inaonyesha kuwa Tanzania ni ya nne duniani kwa nchi zinazoongoza kwa huzuni! Tanzania imeshindwa tu na Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya kati na Syria. Cha kushangaza ni kwamba hizi nchi zote zinazoshindana na Tanzania zina vita! Ni wazi kabisa kuwa wananchi hawawezi kuwa na furaha iwapo wanaishi katika mazingira ya vita. Tanzania kulikoni, ilhali watawala kila siku wanajipiga vifua kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani?
KWA NINI HATUNA FURAHA?
Sababu bila ya shaka ziko nyingi, miongoni mwake zikiwa ni hizi zifuatazo:
1. Hali za wananchi kiuchumi ni mbaya sana. Mzunguko wa fedha umepungua sana kiasi kwamba biashara nyingi na shughuli zingine za kiuchumi zimeathirika kwa kiwango kikubwa.
2. Hali ya usalama wa wananchi ni mbaya sana. Watu wote wanaishi kwa hofu kubwa kutokana na madhara yanayowakuta wale wanaoonekana kuupinga mfumo. Watu kubambikiwa kesi, kupotezwa, kushikiliwa kinyume na sheria vimekuwa ni vitu vya kawaida hivi sasa kwenye jamii yetu.
3. Gharama kubwa za huduma za afya zinapelekea wananchi wengi kuugulia nyumbani. Kwa mfano, kuna ushahidi kwamba Kina mama wengi wanaoharibikiwa na mimba wanatembea na uchafu tumboni kwa sababu hawawezi kumudu gharama za kusafishwa. Hali ni hiyo hiyo kwa wale wenye uvimbe kwenye viungo vyao vya uzazi, nakadhalika.
4. Elimu duni imepelekea kuwepo na jeshi kubwa la wahitimu wa sekondari na vyuo ambao hawaajiriki. Wengi wako chini sana ya viwango.
5. Kumekuwa na matatizo makubwa ya ajira kwa vijana wa kada zote - bila kujali iwapo wamesoma au au hawakusoma.
Hatuoni jitihada zozote za kutatua tatizo hili zaidi ya kupiga blah blah za kisiasa.
Tunataka kiongozi ajaye atutoe hapa tulipo. Bila ya shaka siyo Magufuli.Siyo Magufuli kwa sababu yeye ni miongoni mwa waundaji wakubwa wa matatizo tuliyonayo. Moja ya sifa kubwa za Magufuli ni kutoweza kupima faida na hasara ya baadhi ya vitendo vyake. Leo uchumi wa wananchi uko hoi kwa sababu hiyo.
Vipi kuhusu Lisu? Kama alivyo Magufuli, Lisu naye ni kiongozi ambaye hawezi kupima faida na hasara za vitendo vyake. Lisu ni kiongozi mwenye jeuri, kibri na mjuaji.
Kwa hapa tulipofika tunahitaji kiongozi mnyenyekevu na msikivu. Tunahitaji kiongozi ambaye ana subira ukizingatia kwamba ataongoza taifa la watu wenye uelewa mdogo sana na maskini pia.
Ujinga na umasikini ni vitu viwili ambavyo vikichanganyika vinaweza kuwa na madhara makubwa.
Kiongozi pekee katika wagombea urais waliopo hivi sasa ambaye amebeba sifa zote za kuweza kututoa hapa tulipo ni Profesa Lipumba.
Lipumba ni mchumi bobezi, ni mpole na ni myenyekevu. Ni mtu mwenye subira ya hali ya juu pia.
Profesa Lipumba atalirejeshea hili Taifa matumani baada ya miaka mitano ya purukushani na unyanyasaji mkubwa kwa wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara na baadhi ya viongozi wa dini.
Bila ya shaka wafanyakazi watapenda kupata rais ambaye atawalipa mshahara na marupurupu yanayoendana na kupanda kwa gharama za maisha, na siyo kila siku kupewa ahadi ambazo hazitekelezwi, huku kila siku wakiishi kwa hofu ya kufukuzwa kazi bila ya kusikilizwa.
Bila ya shaka wakulima watapenda kupata rais ambaye atasikiliza matatizo yao na kuyafanyia kazi, na sio kuamka asubuhi na kuambiwa kuwa haki ya kuuza mazao yao kwa mnunuzi wanayemtaka imepokwa!
Bila ya shaka wafanyabiashara watapenda kupata rais ambaye atajenga mfumo wa kodi unaotabirika na ambaye anawapa msaada wa kukuza biashara zao na sio kutoa vitisho kila kukicha.
Bila shaka Watanzania wenye dini watapenda kuona kuwa rais ajaye atasimamia kuhakikisha kwamba dini zote zinapewa hadhi sawa na mamia ya wafungwa wa kiimani wanaachiliwa huru na kuungana na familia zao.
TUSISAHAU, OKTOBA 28 KURA ZOTE KWA LIPUMBA!