SoC04 Tubadili mfumo wa elimu ili kusaidia jamii

SoC04 Tubadili mfumo wa elimu ili kusaidia jamii

Tanzania Tuitakayo competition threads

bravofau2

Member
Joined
Oct 4, 2023
Posts
47
Reaction score
57
Utangulizi

Salamu kwenu wana jukwaa. Andiko langu kwa Tanzania niitakayo litajikita katika Nyanja ya Elimu ya awali, msingi mpaka sekondari (Kidato cha Nne)

Mfumo wa Elimu yetu bado haujaweza kukidhi matarajio ya wanafunzi wengi pamoja na wale wanaohangaika kuwasomesha.

Wakati wanafanya marekebisho ya mitaala ya Elimu hivi karibuni, binafsi nilijua kuna vitu vya msingi wameviona na kwamba wangekuja na mtaala utakao mfanya mwanafunzi kuwa na mwanga wa nini cha kufanya ikiwa matokeo ya mitihani ya mwisho hayatakuwa mazuri. Binafsi pia sijaona tija ya kupunguzwa darasa moja, sijafatilia pia kujua kama michepuo iliyoongezwa italeta tija au la.

Elimu ni ufunguo wa maisha, Je, ni nini kifanyike ili tuwe na elimu inayoweza kufungua milango ya maisha kwa wahitimu? Mbona tumekuwa na elimu inayomfanya mhitimu kusubiri afunguliwe milango? Jambo hili la mtu kusubiri kufunguliwa mlango na mtu mwingine limekuwa likipelekea hata kuwako na rushwa pindi mtu anapotafuta kazi na hasa kwa mabinti kuombwa hata rushwa ya ngono.

Nawashukuru sana mlio buni uwanja huu, kiuhalisia mtapata mawazo mengi mazuri ambayo ikiwa wenye mamlaka wana nia njema na watanzania na kwamba wanapenda kuona kila mtanzania anapata kilicho bora basi jambo la kufanya mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu haliepukiki, Tanzania tunayoitaka ni ile ambayo itamuandaa mtanzania tangu awali kuweza kufungua mwenyewe mlango wa maisha, hatua za kimageuzi zifuatazo zinaweza kutusaidia kutoka hapa tulipo.

Hatua ya kwanza:- (Elimu ya awali)
Yafanyike mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu yetu, kwamba, Elimu ya awali iende mpaka darasa la tatu na kwa kipindi chote hicho walimu wajikite kwa umakini sana katika kuwafundisha watoto yafuatayo:-

1: Kusoma

2: Kuandika

3: Somo la kiswahili

4: Somo la kingereza

5: Somo la hisabati

6: Michezo

Masomo haya sita, yote yapewe nafasi ya kutosha katika kufundishwa kwa kipindi hiki cha miaka minne ya mwanzo ili kumfanya mwanafunzi awe na uwezo mzuri wa kusoma vizuri kwa uhakika na kwa kujiamini, kadhalika kuandika na kuhesababu, kwa kifupi mtoto atakapomaliza kipengele cha elimu ya awali, walimu wa madarasa yanayofuata wasihangaike tena kumfundisha mtoto namna ya kusoma, kuandika au kuhesabu.

Hatua ya pili:- (Elimu ya Msingi)
Wanapoingia darasa la nne, ambao ni mwaka wa tano tangu mtoto aanze shule, wafuatao waanze kutembelea shule zetu za msingi ili kuanza kupenyeza nadhalia ya fani mbalimbali kwa watoto wetu, Elimu hii ya msingi iwe kwa miaka minne yaani darasa la nne, la tano, la sita na la saba.

Wakufunzi wa vyuo vya ufundi kama; Umeme, ushonaji, fundi ujenzi, fundi mbao, fundi magari, Udereva, uchomeleaji, fundi rangi, fundi bomba, Hotelia, Saloon za kike na kiume, fundi paa, wachoraji, wachongaji na kadhalika.

Taasisi/Kada.
Daktari/Nesi, Maabara, Askari Polisi, Askari Magereza, Askari Jeshi, Dini, Siasa, Sheria, Uhasibu, Ugavi, Sayansi, Ustawi wa jamii, Mazingira, Jorojia, biashara, kilimo, uvuvi na kadhalika.

Watajwa wote hapo juu, na hata ambao sijawataja ambao serikali itaona inafaa, waanze kutembelea shule za msingi, walau kila shule mara mbili kwa wiki kwa kila fani ili kuanza kupenyeza elimu ya ufundi na fani zingine, hii itasaidia sana, kwamba kadiri mtoto anavyokuwa kiumri ndivyo yeye mwenyewe na mzazi/mlezi wanajua uelekeo kwa siku za mbeleni, na kumbe mtoto hatapata shida kwa sababu tayari ana uelewa wa awali wa shughuli anayoweza kuifanya tofauti na utaratibu wa sasa ambapo mtoto huchagua mchepuo afikapo kidato cha pili kwenda cha tatu bila kuzingatia miaka minane au tisa aliyoipitia akisoma bila kujua atafanya kitu gani kama sehemu ya maisha yake, pia utaratibu huu utampa mzazi au mlezi mwanga wa kujua namna ya kumsaidia mtoto wake.

Programu hii ya elimu ya ufundi na fani zingine kwa nadharia iwe ni ya miaka mitatu au minne, hivyo, wanafunzi watakapofika darasa la sita au la saba watatahiniwa ili kupima uelewa wao katika fani aliyokuwa akiifatilia kwa miaka hiyo mitatu au minne, na mzazi/mlezi atapewa matokeo na ushauri wa kumuendeleza mtoto katika fani husika.

Na michepuo yote ianze kuelezewa katika kipindi hiki ili mtoto kwa msaada wa mzazi au mlezi apate muda mwingi wa kuchagua jambo ambalo anaona atalimudu vizuri.

Na kama mtoto akichagua mchepuo wa biashara, basi anapofika kidato cha kwanza ajikite kwenye hilo, na masomo yasiyohusiana na mchepuo wake yasimpotezee muda wa kufatilia yale yanayomuhusu, mtoto kasema angependa kuwa Daktari, kwanini alazimishwe kufundishwa kwa pamoja na masomo yasiyohusiana na udaktari?

Hatua ya tatu:- (Elimu ya sekondari)
Ni matumaini yangu kwamba hizo hatua mbili za kwanza zinaweza kutoa mazao bora sana, hivyo, katika hatua hii ya tatu Serikali iongeze Techinical School na Vyuo vya ufundi ili kuweza kuwapokea na kuwaendeleza wanafunzi wote wanaomaliza elimu ya msingi, shule za sekondari zilizopo zinatosha, hivyo ili kuharakisha mchakato huu, baadhi ya shule za sekondari zibadilishwe na kuwa vyuo vya ufundi na nyingine kuwa technical school.

Mwisho
Jambo hili lina gharama kubwa sana kulianzisha, kwa kuwa litahitaji wakufunzi wengi, kurekebisha au kuaandaa mitaala mipya Pamoja na kununua vifaa vya kufundishia au kujifunzia, lakini ikiwa wadau na serikali kwa ujumla watalichukulia Chanya litakuwa na tija kubwa kwa serikali na taifa kwa ujumla kwa kuwa Taifa litakuwa na wataalamu wengi na wenye sifa za kujiajiri na kuajiriwa tofauti na sasa kwamba baadhi ya watoto wanaofeli darasa la saba au kidato cha nne wengi wao hukosa muelekeo na hapo ndio familia na mtoto huanza kuhangaika na kujikuta wanaingia katika shughuli mbalimbali hatarishi kwa afya na mustakabari wao kwa ujumla.

Mzazi anampeleka mtoto chuo cha ufundi umeme baada ya mtoto kufeli kidato cha nne, bahati mbaya hajui mtoto angependa kufanya nini, kwa hiyo mzazi akikosea kumpeleka mtoto kwenye uelekeo wake, mtoto atakuwa amepoteza tena miaka minne. Na hata akifanikiwa kusoma fani hiyo bado exposure yake sokoni itakuwa ndogo tofauti na kama angeanza mapema maana angekuwa anafatilia fani yake kwa zaidi ya miaka minane.

Asanteni sana Jamii Forum kwa namna mnavyojikita kuisaida jamii yetu.

Mungu atusaidie. Amina.
 
Upvote 2
Nawashukuru sana mlio buni uwanja huu, kiuhalisia mtapata mawazo mengi mazuri ambayo ikiwa wenye mamlaka wana nia njema na watanzania na kwamba wanapenda kuona kila mtanzania anapata kilicho bora basi jambo la kufanya mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu haliepukiki, Tanzania tunayoitaka ni ile ambayo itamuandaa mtanzania tangu awali kuweza kufungua mwenyewe mlango wa maisha, hatua za kimageuzi zifuatazo zinaweza kutusaidia kutoka hapa tulipo.
Hakika.

Programu hii ya elimu ya ufundi na fani zingine kwa nadharia iwe ni ya miaka mitatu au minne, hivyo, wanafunzi watakapofika darasa la sita au la saba watatahiniwa ili kupima uelewa wao katika fani aliyokuwa akiifatilia kwa miaka hiyo mitatu au minne, na mzazi/mlezi atapewa matokeo na ushauri wa kumuendeleza mtoto katika fani husika.
Asee, wazo murua sana hili. Kama wanamazingaombwe waliweza kualikwa na kuwasisimua watoto kuhusu viinimacho. Ni wakati sasa wa kuwaalika wataalamu mbalimbali na wajasiriamali kadri inavyowezekana ili mtoto akirudi nyumbani akaseme vitu kama "Baba leo tulitembelewa na mtu anatengeneza mkaa/sabuni hapohapo unaitumia" au "Tumetembelewa na daktari katuonyesha upasuaji wa midoli, na kutoa huduma ya kwanza". Mwisho wa siku anavutiwa na mmojawapo. Nzuri.

na masomo yasiyohusiana na mchepuo wake yasimpotezee muda wa kufatilia yale yanayomuhusu, mtoto kasema angependa kuwa Daktari, kwanini alazimishwe kufundishwa kwa pamoja na masomo yasiy
Kwa hili ni kuwa makini tusikurupuke ili tusije kumpata daktari asiyejua kuandika insha na barua za kikazi kisa aliruka somo la lugha. Kuna faida kiasi kuwa na uelewa mpana wa mambo yote muhimu bila kuathiri umahiri wa kada mahsusi.
Asanteni sana Jamii Forum kwa namna mnavyojikita kuisaida jamii yetu.

Mungu atusaidie. Amina.
Ubarikiwe pia
 
Back
Top Bottom