Moto wa akina Qares wazidi kuichoma CCM
MAKAMBA ANUKUHU BIBLIA, QU'RAAN KUMTETEA KIKWETE
Salim Said
MOTO uliowashwa kwenye kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere dhidi ya Rais Jakaya Kikwete umezidi kuiumiza CCM kiasi cha katibu mkuu wa chama hicho tawala kulazimika kuitisha mkutano mwingine na waandishi kutolea kujibu baadhi ya makombora.
Katika kongamano hilo, wachangiaji walimlaumu Rais Kikwete kwa kusita kufanya maamuzi magumu, huku waziri katika serikali ya awamu ya tatu, Matheo Qares akitaka CCM imtose iwapo atashindwa kufumba macho na kuwashughulikia watuhumiwa wa ufisadi kabla ya mwakani na waziri wa serikali ya awamu ya pili, Musa Nkangaa akieleza bayana kwamba chama kimepoteza mwelekeo.
Katibu huyo, Yusuf Makamba juzi alijibu tuhuma za mawaziri hao wawili akisema kuwa wanaotaka Kikwete atoswe na CCM kwenye urais mwaka 2010 ni wehu, lakini jana akaitisha mkutano na waandishi wa habari na kumtetea mwenyekiti wake akitumia maandiko ya vitabu vitakatifu vya Msaafu na Biblia.
Makamba aliwaambia waandishi wa habari jana akisema: "Kama ilivyoandikwa na Warumi 13:1 'Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu na wao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu; pia katika Korani, Mwenyezi Mungu anasema 'mtiini Mungu na Mtume wake (S.A.W) na wale wenye mamlaka miongoni mwenu.'
Rais Kikwete ana mamlaka miongoni mwetu, kwa nini tunamvunjia heshima?"Nkangaa na Qares walikuwa wakuu wa mikoa na mimi pia nilikuwa mkuu wa mkoa, tunajuana vizuri.
"Wameyasema haya kwa sababu walikuwa na watu wao katika uchaguzi wa 2005, lakini hawakupita ndio maana wanakuja na madai haya. Hapa hatoswi mtu, watajiju."
Alisisitiza kuwa makada hao ni wehu na kwamba CCM haiwezi kukaa na kuwajadili ili kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa kuwa inatambua kuwa ni wehu.
"Tunajuana Qares aligombea ubunge Singida Mjini, lakini akakataliwa, amepauka kama shati na ndio mana labda ana chuki kwa sababu alishindwa na Mohammed Dewji,"alisema Makamba.
"Afadhali wale wehu wa barabarani, maana utamwona mwehu barabarani anatembea bila ya nguo, lakini akiiona CCM au msafara wa rais Kikwete husema 'CCM oyee…..JK oyeee," alisisitiza Makamba.
Makamba alisema CCM haiwezi kumtosa Rais Kikwete kama makada hao wanavyotaka kwa kuwa ni mtaji wake kisiasa.
"Kwa nini nasema ni mtaji wa CCM; moja ni kwamba Redet ilifanya utafiti Novemba 2008 na ikasema umaarufu wa Rais Kikwete ulikuwa asilimia 78.5, Sinovet Tanzania nao walifanya utafiti Julai 2009, walibaini pia kuwa umaarufu wa Rais Kikwete ni asilimia 86," alisema Makamba.
"Redet ikasema umaarufu wa CCM ni asilimia 72.8 wakati Sinovet Tanzania ikabaini asilimia 62.9 umaarufu wa CCM, kwa hiyo hapa tukiangalia Rais Kikwete amekizidi hata chama chake kwa umaarufu, hivyo huu ndio mtaji wetu," aliongeza.
Makamba alisisitiza kuwa "kutokana na hali hiyo, anayetaka JK atoswe 2010, huyo ni mwehu, asiyeitakia mema CCM na hawezi kusikilizwa ndani ya chama".
"Nani kama Kikwete ndani ya CCM? Hamna kwa sasa, yeye ndiye daraja letu tunamtegemea ili atuvushe 2010."
Alifafanua kuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, CCM ilishinda kwa asilimia 93 kazi ambayo haikuwa ya katibu mkuu wake Yusuf Makamba wala mweka hazina wake, (Amosi) Makalla, bali ilikuwa kazi ya Rais Kikwete kutokana na kukubalika kwake.
Kuhusu madai kwamba rais hajachukua maamuzi mazito, Makamba alihoji: "Ni maamuzi gani hayo mazito wanayotaka rais achukue zaidi ya haya aliyochukua?
"Unamchukua rafiki yako, kiongozi mwenzako, uliyekuwa naye katika vikao vya baraza la mawaziri na bunge, unampeleka mahakamani, hayo hayajawa maamuzi mazito? Je, ni maamuzi gani mazito wanayoyataka?
"Lakini hata hao ambao wanatuhumiwa ni hadi uchunguzi ufanyike. Hivi kwa mfano ukisikia Makamba amefumaniwa utaandika tu, si mpaka ufanye uchunguzi?
"Pengine alikuwa na bukta yake anatoka mazoezi watu wanafukuza mwizi wakamwona yeye wakasema ametoka kwa mke wa mtu, hiyo haitakuwa haki hadi uchunguzi ufanyike. Kwa hiyo hawa watuhumiwa ni binadamu nao tuwatendee haki, tuwaonee huruma."
Moja ya mambo ambayo Kikwete amekuwa akilaumiwa kuwa anasita kuchukua hatua ni suala la kuwawajibisha watumishi walio chini ya mamlaka yake ambao Bunge liliazimia wachukuliwe hatua, akiwemo mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah kutokana na kutowajibika ipasavyo katika kashfa ya Richmond.
Alisema CCM iliunda chombo cha maadili ambacho kazi yake kubwa ni kuchunguza tuhuma za wanachama na kuchukua hatua kwa sababu haina utamaduni wa kutimuana kwa tuhuma.
Kuhusu madai kuwa chama hicho kimetekwa na matajiri na kwamba viongozi wanashindana kujilimbikizia mali, Makamba alisema CCM si chama cha matajiri, bali ina wanachama matajiri hivyo kitendo cha watu kusema ni chama cha matajiri sio sahihi.
"Philemon Ndesamburo ni tajiri ndani ya Chadema, lakini hiyo haimaanishi kuwa Chadema ni chama cha matajiri. Kwa hiyo wanapaswa wajue kuwa CCM, NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema si vyama vya matajiri bali vina wanachama matajiri ambao ni waaminifu kwa vyama vyao," alisema Makamba.
"Hawa wehu wanapiga kelele CCM chama cha matajiri, CCM chama cha mafisadi baadhi yao wanachukua posho na mishahara yao hukohuko kwa matajiri," aliongeza.
Alisema yuko tayari kutetea kauli na msimamo huo popote hata ikibidi kufungwa au kufa akimtetea Rais Kikwete.
"Kwanza wakishtaki huyo hakimu mwenyewe atashangaa. Watu wanamvunjia heshima rais halafu anatokea mtu anawaita wehu wanaenda kushtaki, hata huyo hakimu atacheka," alisema Makamba.
Kuhusu hoja kwamba CCM imepoteza mwelekeo, Makamba alisema kabla ya uhuru wakati chama cha Tanganyika African National Union (Tanu) kinaundwa, lengo lilikuwa ni kuwaandaa Watanganyika kujitawala, lakini sasa kila chama cha siasa lengo lake ni kushinda uchaguzi na kushika dola.
Alisema kukubalika kwa chama kunaonekana katika matokeo ya tafiti na chaguzi mbalimbali zinazofanyika mara kwa mara nchini.
“Tumeshinda Tunduru, Kiteto, Busanda, Mbeya Vijijini, Magogoni Zanzibar na tumekomboa jimbo letu la Biharamulo, lakini pia tumeshinda kwa asilimia 93 serikali za mitaa," alisema Makamba.
Alisema kuwa chama bado hakijapata maazimio ya kongamano la taasisi hiyo hawajayapata, lakini watakapoyapata watayajadili katika vikao vya juu vya CCM