Dk. Nchimbi ageuka mbogo kujibu shutuma dhidi yake
2008-10-05 14:30:33
Na Simon Mhina
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Dk. Emmanuel Nchimbi, jana aligeuka Mbogo baada ya kuulizwa juu ya shutuma zilizotolewa dhidi yake na Katibu wa umoja huo mkoani Tanga, Mwita Mwaikabe Waitara.
Katibu huyo alikaririwa na vyombo vya habari akilalamika kwamba Dk. Nchimbi, anafanya mikakati na hila za kila aina kuwakwamisha vijana wenye msimamo kama wa Nape Nnauye, katika kuwafichua mafisadi.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana jijini Dar es Salaam, Nchimbi, alisema habari hizo zimemkera na kumnyima raha.
Mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake, alisema yeye hahusiki na shughuli za utawala na utendaji wa kila siku katika UVCCM, hivyo kumuuliza maswali ni kuzidi kumnyima raha na kutomtendea haki.
Alipoulizwa ni vipi anakataa kuzungumzia mambo ya UVCCM wakati yeye ndiye bosi wa umoja huo na Waitara alimtaja waziwazi, Nchimbi alijibu ``Lakini wewe Mwandishi kwa nini unataka kunilazimisha niseme mambo nisiyotaka kusema? Kukaa kimya ni haki yangu naomba usiendelee kuninyima raha.``
Nchimbi alisema yeye akiwa mwenyekiti hashughuliki na mambo `madogo madogo` kama hayo bali anazo shughuli nyingi za kufanya.
``Simjibu Waitara japokuwa mnanitaka ni jibu simjibu, nimekataa sina muda mchafu,`` alisema Nchimbi.
Alipoulizwa madai kwamba alitumia ukabila kumpa nafasi ndugu yake aitwaye Sixtus Mapunda, Nchimbi alisema madai hayo ni ujinga, kisha akakata simu.
Baadaye Nchimbi alituma namba za simu za Katibu wake na kumtaka mwandishi wa habari hizi awasiliana naye kuhusu suala la Waitara.
Katibu huyo Francis Issac, alimbeza Waitara huku akisisitiza kwamba si mwanasiasa bali ni mtumishi tu.
``Waitara si mwanasiasa yule ni mtumishi kama walivyo watumishi wengine sehemu yoyote nimeshangazwa na majigambo yake,`` alisema.
Issac, alisema kama kweli Waitara anataka kibarua chake kiote majani, basi anapaswa kuandika barua rasmi.
``Maneno yale kayasemea nje ya kituo chake cha kazi, yule ni mtumishi tu tuliyemwajiri, sasa kama hataki kazi aandike barua sio kuzungumza kwenye magazeti.
Anazungumza na Magazeti kwani ndiyo yalimuandikia barua ya kumwajiri?� Alihoji na kuongeza ``Yule ni mtumishi anapaswa kujua hilo na sisi ndio waajiri wake.``
Katibu huyo alisema anasubiri kwa hamu barua ya Waitara hivyo aiwasilishe kwake haraka iwezekanavyo.
Kuhusu madai ya upendeleo, Issac alisema si kweli kwamba Mapunda ni ndugu wa Nchimbi.
``Yaani kwa vile wote ni Wangoni, basi ni ndugu? Wewe kama ni Mnyaturu basi Wanyaturu wote wanakuwa ni ndugu zako?`` Alihoji.
Alipoulizwa ikiwa Waitara si mwanasiasa, kwanini aliitwa kwenye kampeni za CCM mjini Tarime, Issac alisema alishiriki kwa vile wanachama wote wanaruhusiwa kukipigia debe chama chao.
SOURCE: Nipashe