Hii lugha ya kuwa eti deni letu la taifa bado ni himilivu, na kuanza kujisifu kuwa bado tunakopesheka na bado pia tutaendelea kukopa, ina ukakasi mwingi sana. Hii ndiyo sababu kubwa inayopelekea viongozi wetu kutokutilia maanani kuongeza vyanzo na kupanua wigo wa kuongeza mapato ya nchi.
Mikopo ambayo baadhi yetu wanaishangilia, hivi sijui hata kama wanadadisi kuhusu masharti yanayoambatana nayo. Serikali ifikie wakati sasa ifanye "down sizing".
Ipunguze nafasi nyingi za watendaji wenye kofia za kisiasa tu ndani yake ili "government expenditure" zishuke angalau kwa 50%. Serikali imejaza watumishi wengi mno ambao wengi wao hata hawajui wanafanya nini, achilia mbali suala la uzalishaji wao kuwa wenye tija.
Badala ya kukopa, ni vyema serikali ikafikiria vitu vifuatavyo;
1. Iendeshe baadhi ya shughuli ama mashirika yaliyo chini yake kwa njia ya PPP.
2. Nafasi ya RC ama DC ziwe zinatokana na mmoja wapo wa wabunge waliochaguliwa katika majimbo yaliyopo ndani ya mkoa husika.
3. Idadi za wabunge zipunguzwe ili iendane na idadi ya wilaya
4. Ifute nafasi za wabunge wanawake wa viti maalum bungeni, kwa sababu huo umaalum wao wala haupo.
5. Iwakopeshe magari watendaji wa serikali ili wawajibike wao wenyewe katika kuyagharimia katika matengezo yake na kuajiri madereva.
6. Kupunguza marupurupu ya kufuru kwa viongozi wakisiasa wastaafu ili nao wawe kama wazee na wastaafu wengine.
7. Posho za vikao kwa wabunge ziondolewe, kwani kazi ya uwakilishi bungeni ni kazi, kwa hiyo wanapaswa kulipwa mishahara, "transport allowances" na "per diems" tu pale wanapoenda kuhudhuria vikao vya kamati za bunge ama vingine vya Bunge.