Habari wana JF
Mwenzenu nimeoa (mke mfanyakazi) miaka mitatu iliyopita na kujaaliwa ka baby boy mmoja tu.
Tatizo langu ni, mke wangu kamwachia majukumu yooote msichana wa kazi! Kwa mfano, usafi wa nguo zangu, maandalizi ya chakula na kazi zote za nyumbani.
Hilo mimi sijali lakini najiuliza kuhusu hili, ninaporudi nyumbani na kifurushi mkononi hata kama mke wangu amekaa tu hana kazi yoyote atamwita msichana wa kazi na kumuamuru anipokee. Anaponipokea anasema, shikamoo baba......, pole........., karibu............., tena kwa unyenyekevu wa hali ya juu. Mke wangu desturi hiyo hanaa!!
Atakapoandaa chakula house girl huyu huyu ataninawisha mikono na kunikaribisha chakula kwa unyenyekevu mkubwa akisema `karibu chakula baba`. Wife wala habari hana, na siku akiandaa msosi wife atasema `Baba nanii....chakula tayari`.
Asubuhi chai napo ni vivyo hivyo, atapewa house girl viatu asafishe (kubrash) then atanirudishia na kunambia kwa utulivu, viatu tayari baba!!
Mbaya zaidi juzi nikamkuta chumbani kwetu kwenye bafu (master) anafulia huko huku wife akiwa amekaa barazani na wenzie wanapiga story. Nikamuuliza unafanya nini huku na kwa ruhusa ya nani, alinijibu kuwa mama kamwambia afulie nguo zetu kule (za mimi na wife) then afanye na usafi wa kule msalani na chumba kizima, pia nahisi alitakiwa afue hata nguo za ndani coz nilikuta zimelowekwa pale pale.
Kiukweli nilichukia sana na akili ilinituma nimchape kitu yule binti (ku-mdo) but ni busara tuu iliyoniepusha.
Nimejaribu kumrekebisha mara kadhaa ananisikia na kunielewa but anaonekana ni mvivu kutimiza wajibu wake. Wife ni msikivu sana but sielewi tatizo nini jamani.
Swali langu ni kwamba, wanaume wenzangu mnayarekebisha vipi mambo kama haya coz kikawaida hisia zinaweza kuhamia kwa binti kwa jinsi alivyoachwa kuwa karibu nami na hasa wife alivyojiweka mbali ili nisije zua balaa.
Asanteni sana
Kwa kuoana hamchukuani mke na mume, Bali mnauchukua ulimwengu wenu mzima. Kuanzia hapo mpaka maisha yenu yote mke/mume wako atakuwa mwenzio, mwandani wako, na rafiki yako mpenzi.
Mwanamume na mwanamke wanapofunga ndoa inawapasa wote watambue desturi, mwendo mwema na adabu katika maisha hayo ya mke na mume ili ndoa yao iwe katika mipaka ya sharia ya imani yao.
Mimi binafsi sikubaliano na mitazamo ya baadhi ya waafidhina, wenye kung'ang'ania kuwa ni lazima mke afanye kazi za nyumbani, kama vile kufua, kupika au kufanyakazi za usafi...! Hizo kazi zitakuwa ni wajibu wake tu, kama mtakubaliana wewe na yeye katika kuwajibika. Kama mume ni mfanyakazi aliye ajiriwa na mke ni mama wa nyumbani basi hapo mtakubaliana kuwa mke awe anafanyakazi za nyumbani kama hizo nilizo zitaja hapo juu na mume atakwenda kibaruani.
Kinyume chake kama mke na mume wote ni wafanyakazi na wana uwezo wa kuweka msaidizi wa kazi, basi mimi sioni kwanini mke afanyekazi za nyumbani na ofisini kwani naye ni binadamu kama alivyo mume, maana wote mnarudi nyumbani mkiwa mmechoka kwa kuwajibika uko makazini kwenu. Sikatahi kuwa mke kumtengea mume chakula na kumfulia nguo za ndani kunaongeza mapenzi, lakini hata mume pia ni wajibu wake kufanyakazi za ndani kama kufua, kupika na usafi wa nyumba. Hapa kidogo inabidi unielewe, mimi siamini wala si mtetezi wa ile dhana ya kijinga ya ukombozi wa mwanamke hapa nina maanisha ile dhana ya jinsia sawa? Naamini kuwa kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake ndani ya nyumba, tena kwa makubaliano na uwezo mliokuwa nao wa kiutendaji. Kwani katika jamii nyingi haswa za Kiafrika bado mwanamke anatarajiwa kuwa, mama kwa maana ya kulea watoto, mke bora, kwa maana ya mfanyakazi mzuri wa nyumbani.
Katika maelewano ya watu wawili kukipatikana aina yoyote ya ushindani na mvutano, basi kunakuwa na matatizo ambayo yataleta mtetereko katika mahusiano hayo kwa jinsi ambayo jambo dogo tu linapofanyika kutapatikana na utesi ulio mkubwa sana. Wanaume wengi wanapenda sana wake zao wawayenyekee na kuwatii, sikatahi ilo maana sisi wanaume wengi tunapenda kuonyesha utawala ndani ya himaya zetu, lakini kumbuka kuwa wewe ukiwa ni mfalme ndani ya nyumba basi mkeo ni malkia naye ana haki ya kuzungumzishwa kwa njia ya kumnasihi na katika kufanikisha hilo tafuta wakati ambao ni munasibu na uzungumze naye kwa kumpa mawaidha mazuri na kwa upole.
Suhala la kutembea na mfanyakazi wa ndani kwa kuwa tu ndiye anaye kuhudumia kwa unyenyekevu na heshima icho si kisingizio cha wewe kuingia kwenye aibu ya zinaa na kumdhalilisha mkeo.
Je ingekuwa mnamiliki shamba, na mmemuweka shamba boy, ambaye anafanyakazi zote za shurba uko shambani, na ikaja kutokea kuwa mkeo amemtamani ili azini naye kwa kuwa tu shamba boy anaonekana shupavu na mwenye mwili uliojengeka kwa kazi za shamba. Wewe kama mume ukija sikia utachukuwa uwamuzi gani? Tusiwe na fikra za ngono kwa kufikiria kuwa ndio suluhisho za hasira zetu.
Basi nimalizie kwa kushauri jambo moja, ikiwa maisha yenu, yameelemea kwenye mila na desturi zenu za kikabila, na jitihada zako za kumfahamisha nini wewe unapenda kushindikana, basi itisha kikao baina yako wewe, mkeo na wazazi wake na wako ili kuzungumzia suala hilo ambalo wewe unahisi linaharibu utulivu wa nyumba yako. Mazungumzo yawe ya upole na ulaini na huenda akafahamu makosa na akajirekebisha. Msisitizo katika kufanikisha hilo ni kila mmoja awe muwazi katika kikao hicho.
Lakini ukumbuke kuwa mume na mke wanapaswa waishi katika mawimbi ya hisia kila mmoja ajaribu kumzidi mwingine kihisia za kumjali mwenza, hapa maisha ya ndoa yatakuwa ya furaha kwelikweli na ndoa hiyo, InshaAllah, itadumu na kama itavunjika basi ni kwa sababu za msingi za kibinadamu.
Ni jambo la kuzingatia mno kuwa ndoa ni mkataba lakini mkataba huu hauna uhai wa kujitegemea, uhai wa mkataba huu si wa cheti cha ndoa wala pete ya ndoa na si wa sherehe za harusi bali umo katika nyoyo za wale waliofunga ndoa, na wakaishi kwa mapenzi na kusaidia katika kila jambo linalowezekana kusaidiana...!
Nakutakia kila la kheri katika maisha ndoa yako wewe na mkeo, pia nasisitiza kuwa achana na mawazo ya kutaka kutembea na mfanyakazi wa ndani kwani heshima yako itakuja kupotea bure na kuhatarisha ndoa yako.