SoC01 Tujifunze kutoka Rwanda viwanda vya kuunganisha magari

SoC01 Tujifunze kutoka Rwanda viwanda vya kuunganisha magari

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Jul 15, 2021
Posts
16
Reaction score
61
Nikiwa seminari tuliwahi kufundishwa kilatini ijapokuwa ntakuwa nimesahau maneno mengi bado nakumbuka msemo wa muhimu sana wa kilatini unaosema kama wengine wameweza kwanini mimi? Kwa kilatini Si isti et istae cur non ego? Msemo huu utatuongoza kwenye makala yetu ya leo tukitafakari hatua walizofikia Rwanda kuanzisha viwanda vya kuonganisha magari (vehicle assembling plants).

Rwanda ni taifa lenye watu takibribani milioni 12 na lina pato la taifa (GDP) linalokadiriwa kuwa dola za Kimarekani bilioni 10.3 kwa takwimu za mwaka 2021. Wamiliki wa magari binafsi waliosajiliwa kuanzia mwaka 1997 mpaka mwaka 2018 wanakadiriwa kuwa watu 200,000.

Mwaka 2018, Rwanda kwa kushirikia na kampuni ya magari ya Volkswagen kutoka Ujerumani walifungua kiwanda cha kuonganisha magari chenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 20 sawa na bilioni 46 za Kitanzania.

Kiwanda hichi tangu kimeanza uzalishaji wa magari haya kimeshazalisha magari 700 na zaidi huku matarajio ya kiwanda hicho ni kuzalisha magari 5,000 kwenye awamu ya kwanza ya mradi huo. Kiwanda hicho kinazalisha takribani aina saba za magari ya Volkswagen kama vile Polo, Passat, Tiguan, Amarok na Teramont huku zingine mbili zikiongezwa mwaka huu.

Malighafi za kuunganisha magari haya ya aina ya Volkswagen inatoka Afrika ya Kusini na kufikia bandari ya Dar es Salaam na kisha kuyasafirisha kwa barabara mpaka Rwanda. Kiwanda hichi kinatarajia kutengeneza ajira zipatazo 1,000 nchini Rwanda.

Kiwanda hichi pia kitaongeza pato la uchumi kwa Rwanda kwa kuongeza wamiliki wa magari ndani ya nchi na kuuza nchi jirani huku ikipunguza gharama ya kuagiza magari yaliyotumika kutoka Japan.

Swali la kujiuliza kama Rwanda wameweza kuanzisha kiwanda cha kuonganisha magari je, Tanzania tunashindwa wapi?

Tanzania kwa upande mwingine ina watu wanaokadiriwa kuwa milioni 60 huku pato la taifa (GDP) likikadiriwa kuwa dola za kimarekani bilioni 62.2 kwa takwimu za mwaka 2012. Tanzania ni muagizaji mkubwa wa magari yaliyotumika kutoka Japan huku ikikadiriwa kuagiza magari 2,000 mpaka 3,000 kwa mwaka. Uagizwaji wa magari haya kutoka Japan na kwingineko kwa mwaka kunakadiriwa kuwa dola za kimarekani milioni 15 sawa na bilioni 34.5 za kitanzania kwa mwaka.

Ukilinganisha Tanzania na Rwanda, ni dhahiri utaona nchi hizi mbili zinautofauti mkubwa takribani kwenye kila kitu japo utofauti wa msingi unakuja kwenye utayari wa kujaribu mambo mengi. Sisemi kuwa Tanzania haijafanya mengi la hasha! ila kwa ukubwa wa nchi yetu na rasilimali tulizonazo tunapaswa kutenda makubwa zaidi kuboresha uchumi wa nchi yetu kwa hali na mali.

Natambua fika vipaumbele vya nchi yetu kama vile kilimo, afya, elimu, maji, umeme, utalii na mengine ya muhimu vinaweza kufanya tukaweka pembeni viwanda vya kuunganisha magari kwa kuwa haiwagusi wananchi wengi. Ila, ukweli unabaki kuwa, sekta ya uagizaji nchi inatumia sehemu kubwa ya pesa na kuzifaidisha nchi zingine kwa kuwa hatuzalishi vitu vingi ndani ya nchi yetu. Gharama hii kubwa ya kuagiza vitu kutoka nje ya nchi itapungua endapo vitu vingine tutazalisha wenyewe ndani ya nchi yetu.

Kutokana na wingi wa watu waliopo Tanzania, ni wazi tutakuwa soko la magari kutoka Rwanda na kuishia kukuza uchumi wao ili hali Tanzania ikibaki kuagiza magari kutoka nje. Nadhani kila jambo linahitaji tathimini nzuri, utayari na kuanza kidogo kidogo. Kwenye hili swala la magari, nadhani ni muda muafaka sasa tukakaribisha wamiliki wa viwanda vikubwa vya magari kutoka sehemu zote ulimwenguni na kuingia ubia na serikali kuanzisha viwanda vya kuonganisha magari Tanzania ambavyo mwisho wa siku vitapunguza kupelekea pesa nyingi nje ya nchi, vitaleta ajira za kutosha, vitatumia rasilimali zilizopo kama chuma cha Liganga na Mchuchuma, madini mbalimbali na mengine mengi.

Kwa kuwa magari yote tunaagiza kutoka nje ya nchi, tunashindwa kufikia sekta muhimu za huduma mbalimbali kama vile afya, elimu, kilimo, usafirishaji kwa kuwa gharama ya kuagiza magari ni kubwa sana kutoka nje ya nchi hivyo kufanya taasisi nyingi za binafsi na serikali kushindwa kuwa na magari ya kusaidia wagonjwa na kutoa huduma kwenye jamii. Endapo tutaweza kuanzisha viwanda vya kuonganisha magari nchini hapa ni dhahiri tutaweza kusaidia jamii yetu kupata huduma bora na muhimu na kuongeza pato la taifa pia.

Viwanda vya magari vinavyoweza kuanza, ni vile viwanda vya kimkakati kwa maana ya magari yanayohitajika sana kama vile ambulance, matrekta, mabasi, magari ya utalii, malori na mengine ambayo hutumika kutoa huduma hivyo kupunguza gharama kubwa ya kuagiza magari ambayo yangepatikana kwa gharama nafuu endapo yangekuwa yanapatikana hapa nchini. Sambamba na hili, tatizo la ajira litapungua kwa kiasi kikubwa kwani viwanda hivi vikubwa vitatoa ajira nyingi sana kwenye mnyonyoro wote huu wa thamani wa magari.

Wizara ya viwanda ni muda sasa wakafanya tathimini hii kwa kujifunza kutoka Afrika ya Kusini na Rwanda ambao tayari wameanza kuonganisha magari nchini kwao na kuona jinsi ya kuanzisha viwanda hivi hapa Tanzania. Wizara pia inahitaji kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji watakaokuwa tayari kuja kuwekeza kwenye viwanda vya magari nchini Tanzania.

Sekta ya usafirishaji inakuwa kwa kasi sana nchini Tanzania na namna pekee ya kuiboresha na kuwapa ahueni wawekezaji kwenye sekta hii ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kuonganisha magari ambavyo vitafanya sekta hii kuwa nafuu na yenye kuingiza mapato makubwa. Hili ni eneo linguine litakaloweza kuongeza kodi kwa kiwango kikubwa kuanzia kwenye ajira, viwanda, vipuri, uingizwaji wa vifaa vya kuonganisha magari na mengine mengi.

Uanzishwaji wa viwanda vya kunganisha magari nchini Tanzania unapaswa kutathiminiwa upya ili kuongeza pato la uchumi wa nchi yetu. Ni muda sasa wataalamu wetu wakalifanyia tathimini eneo hili na kuja na dira yenye maana kisha kupeleka maandiko kwa wamiliki wa viwanda kuona tija ya kuja kuwekeza hapa nchini.
 
Upvote 6
Mkuu hongera sana na kura yangu umepata ya 2. Kanch kadgo kana tushinda sio poa
 
Back
Top Bottom