Tukibaki Hai, Tutasimulia

Tukibaki Hai, Tutasimulia

TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA -- 37

Na Steve B.S.M



Pennyslavia, Marekani. Majira ya saa nane mchana.

AFISA Michael Summer alivua miwani yake ya jua akaiweka juu ya ‘dashboard’, alifanya hivyo baada ya kuzima gari lake kwani sasa hakuhitaji miwani hiyo maana ameshatoka juani na safari yake imekomea hapo, akafungua mlango na kutoka ndani kisha akaunyoosha mgongo wake, mgongo ukalia ka-ka-kaa! Akashusha pumzi ndefu ya uchovu kisha akalijongea jengo moja lililopo mbele yake, jengo lenye bango kubwa linalosomeka: THE SMITHS. Jengo hilo lilikuwa linahusika na mauzo ya vipuri vya magari, mlango na kuta ya jengo hilo kwa mbele ilikuwa ni ya kioo kitupu.

Akiwa anasogelea mlango, amebakiza kama hatua nne hivi, mara bwana mmoja aliyevalia ‘overall’ ya bluu na kapelo nyeusi alitoka ndani ya jengo hilo akiwa anatembea kwa upesi. Bwana huyo alikuwa anatazama chini akitembea, kidogo akampisha bwana Michael lakini kabla hajaenda popote alihamaki mkono wake wa kushoto umedakwa, kutazama akaona uso wa Michael ukimwangazia na kwenye mkono wa kushoto bwana huyo ameshikilia ‘beji’ ya polisi aliyokuwa anamwonyeshea.

Michael akasema, “bila shaka wewe ni Anthony Sandlers,” kabla bwana yule hajajibu, akaongezea: “mimi ni mpelelezi, nina maongezi kidogo na wewe.”

Maneno hayo yakamshtua bwana yule ndani ya overall. Alimtazama afisa Michael kwa macho ya shaka kisha akatikisa kichwa kuridhia alichoambiwa lakini ajabu ni kwamba punde mkono wa bwana huyo ulipoachiwa, alitimka mbio kama mwendawazimu!

Alitupa miguu yake kadiri alivyoweza akielekea mashariki mwa jengo lile, bwana Michael naye asiwe nyuma, akatimka kumfukuzia. Mbio mbio mbio! Bwana yule alivuka barabara akiyakwepa magari, naye Michael akafanya hivyo! Bwana yule aliwavuka watu na kuwasukuma huku na kule, naye Michael akafanya hivyo! Walikimbizana kwa kama dakika tano pasipo yoyote kufanikiwa.

Ni kama bahati, pikipiki moja ilitokea kusikojulikana ikamsukumia mbali bwana yule mwenye overall. Aliruka juu kiasi chake kisha akabamiza kwenye moja ya kuta ya duka, alipoanguka hapo akawa hana tena jipya, alitulia chini kuugulia maumivu. Bwana Michael Summer, akiwa anahema juu juu, akamsogelea bwana huyo huku akiwa ameshikilia kiuno chake. Alipomfikia akachuchumaa na kumtazama bwana huyo na mbio zake za sakafuni, akamwambia:

“Sasa naona tunaweza kuongea.”

Baada ya muda mchache watu hao wawili wakawa wamo ndani ya gari la Afisa Michael Summer, bwana yule wa overall, Anthony Sandlers kwa jina, akiwa yu kifungoni kwa pingu mikono yake ipo nyuma ya mgongo.

“Kama haufahamu kitu kwanini ulikuwa unakimbia?” Michael alifoka akimtazama Anthony. Macho yake yalikuwa makali, uso wake haukuwa na lepe la utani. “Nakuuliza wewe. Kwanini ulinikimbia?”

“Kwasababu niliogopa!” Anthony akafoka kwa ‘panick’. “Nilikimbia kwasababu niliogopa!” akarudia tena jibu lake. Afisa Michael akaingia mfukoni mwake na kutoa simu, aliifungua akamwonyesha bwana Anthony. Katika simu hiyo kulikuwa na picha kadhaa zinazoonyesha tukio la mauaji ya Travis. Picha ya mwisho ilikuwa ni ile iloandikwa kwa maandishi ya damu ya Travis ‘SUITS AND TIE’.

Anthony akasema kwa mkazo, “van uliyoitoa yard siku hiyo, ndo’ limehusika na mauaji ya afisa huyu wa polisi. Wewe ulikuwa zamu, nataka kujua nani alichukua usafiri huo.”

Kabla Anthony hajajibu, Michael akamwonyesha picha ya van hiyo, picha ambazo zilidakwa na CCTV camera, akasema: “Bila shaka sio gari ngeni machoni pako. Sasa naomba kujua, gari lilitokaje yard ukiwa unalinda na ni nani aliyelichukua.”

Anthony akamtazama Michael usoni, macho yake yalikuwa yanasema jambo lakini hakufungua mdomo kutamka, Michael akamsihi kama hatoonesha ushirikiano basi na yeye atajumuishwa kama mshirika wa mauaji, ‘an accomplice in murder’, kusikia hivyo bwana Anthony akashuku na kujitetea:

“Sijui nani alichukua hilo gari. Lilibiwa tu! … liliibiwa na mtu ambaye sikumwona.”

“Liliibiwa?” Michael akauliza kwa kejeli. “na ulinzi wote ule niliouona pale kwenye yard, gari liliibiwa vipi? Liliwezaje kupita kwenye mageti matatu mpaka nje pasipo kugundulika wakati wewe ndo’ mtu pekee unayetoa ruhusa ya kitu chochote kukatiza getini? Ina maana hukuliona au ulishiriki katika wizi huo?”

Anthony akashusha pumzi, hakuwa na cha kujibu. Alifikiria njia ya kujinasua na kikombe hiki lakini hakupata cha maana kichwani mwake. Michael aliendelea kumhimiza aseme ukweli ili ajiepushe na kesi ya mauaji, alimuahidi bwana huyo kuwa atamlinda na kumsaidia endapo tu akitoa ushirikiano kamili.

“Naamini kuna mtu nyuma ya maamuzi yako, Anthony. Niambie. Unaweza kuniamini.”

Anthony alifikiri. Akakumbuka familia yake nyumbani, mke na mtoto, chozi likamshuka. Aliisikia sauti ikisema kichwani mwake kumkumbusha maagano yake yake ya kazi ya kuwa uhai wa familia yake utakuwa rehani kama akienenda kinyume, akajikuta anatoa chozi zaidi.

Kabla hajasema kitu kingine, risasi ilipasua kioo cha nyuma ya gari kisha ikatua kichwani mwake na kumfumua ubongo! Yani ndani ya sekunde tu, bwana huyo akawa maiti ndani ya gari akimwaga damu pomoni. Afisa Michael akabaki ameduwaa. Hakukaa vema, mdunguaji aliyetoka kufanya tukio la mauaji, akamweka afisa huyo katika ‘target’ yake.

Kisha akavuta pumzi moja ndefu.


******

Kwenye Majira ya Saa tano usiku:

Hilda alijigeuza kitandani akalala chali, mikononi mwake ameshikilia tablet anatazama filamu humo ndani. Mwanamke huyo aliyekuwa amevalia nguo nyepesi ya kulalia, macho yake yalikuwa yamepwaya kwa uchovu wa usingizi lakini hakutaka kusalimu amri, alichokuwa anakifanya ni kubadilisha tu mapozi lakini tablet haiachii mkononi.

Katika chumba hiki hakukuwa na mwanga mwingine isipokuwa mwanga wa tablet pekee. Vitu vingine humu ndani havikuwa vinaonekana vema isipokuwa uso wa Hilda tu ambao ulikuwa unaangazwa na mwanga wa chombo hicho.

Mwanamke huyo akitazama filamu yake, alijisemea: “Nikifika katikati nalala. Nimechoka sasa.” Kisha akapiga mihayo miwili kwa mkupuo. Anapambana na macho asilale.

Katika dirisha la chumba hiko, kwa chini kabisa kuna gari lilionekana likisogea karibu na maeneo haya. Gari hilo lilikuwa ni van nyeusi isiyokuwa na maandishi, vioo vyake vyote ni tinted kiasi cha kutokuona aliyekuwemo ndani ama dereva anayeendesha.

Gari hilo lilisonga na lilipofika karibu na malango ambayo yanatumika kuingilia ndani ya makazi ambamo Hilda yumo, lilijiegesha na kuzima taa, kisha kidogo likazima na injini, kukawa kimya kama vile hakuna kitu.

Hilda alijitahidi kutazama filamu yake lakini kadiri alivyokuwa anasonga mbele akawa anazidiwa, usingizi ulimzidi nguvu mno, ilifikia kipindi aliachia tablet yake ikamwangukia usoni akashtuka kama mbwa aliyetupiwa jiwe, hapo ndo’ akakata shauri, acha tu alale.

Alizima kifaa chake akajilaza lakini kabla hajapotelea usingizini, alisikia mlango wake ukiita kengele keng-keng-keng-keng-keng! Akashtuka, akajiuliza ni kweli amesikia kengele ama ni mang’amung’amu yake ya usingizi, basi akakaa kusikiliza kwa umakini, kidogo kengele ikaita tena, kumbe si mang’amung’amu bali ni uhalisia, mlangoni pake kulikuwa na mgeni. Mgeni katika majira haya ya usiku.

“Nani huyu saa hii?” alilalamika akinyanyuka kitandani, akauendea mlango wake wa sebuleni na kabla hajafungua akachungulia nje kwa kupitia kitundu kilichopo mlangoni hapo, nje akaona sura ya mtu, mtu anayemjua, lakini hakujua kwanini mtu huyo yupo hapo muda kama huo, alitafakari upesi kama kuna jambo lililoenda kombo lakini hakulipata. Alifungua mlango wake akisema, “Karibu.”

Lakini uso wake, dhahiri shahiri, haukuonyesha kumaanisha kile alichokitamka ila hilo halimkuzuia mgeni wake kuingia ndani, aliingia na mlango ukafungwa. Korido ikabakia tupu na kimya.


****

East Hampton, New York. Saa saba usiku.


Bryson alizima gari lake kisha akatulia humo ndani kwa dakika kadhaa. Kuna jambo alikuwa analiwaza. Aliegemea kiti akitafakari, kidogo akashusha pumzi ndefu kisha akaufungua mlango wa gari na kwenda nje. Alihakikisha ame-lock gari yake kwanza ndipo akaelekea ndani. Alipofika mlangoni, alitaka kuweka ‘codes’ za kufungua mlango wake lakini akabaini kuna kitu hakipo sawa.

Taa ya sebuleni ilikuwa inawaka.

Akajiuliza kifuani mwake ni nani aliyekuwapo hapo, basi upesi akaweka codes na alipoingia alitembea upesi mpaka sebuleni, hapo akastaajabu kumwona mke wake amejilaza kwenye kochi. Mwanamke huyo amejikunyata akijifunika shuka.

Kabla hajasema jambo, mwanamke huyo alifungua macho yake na katikati ya giza jepesi la sebuleni akamwona mume wake amesimama kama mnara, akamuuliza: “Umetoka wapi muda huu, Bryson?”

Bryson akaketi, naye mke wake akanyanyuka na kukaa kitako.

“Umerudi saa ngapi kutoka hospitali?” Bryson aliuliza na kuongezea, “mbona hukuniambia kama unarudi nyumbani? Mtoto vipi?”

Mke wake aliguna kwanza alafu akamtaka mumewe atazame simu yake, Bryson akaitoa na kutazama, kwenye kioo kulikuwa na ‘missed calls’ takribani kumi toka kwa mkewe, tena na ‘messages’ kadhaa.

“Ulitaka nikuambiaje, Bryson kama hupokei simu zangu wala kujibu messages zangu?” mke akauliza. “nimejaribu sana kukutafuta, napiga na natuma ujumbe lakini kimya, ulitegemea ningefanya nini kama sio kuja nyumbani? Ajabu nakuja nyumbani haupo na unarejea majira haya? Ina maana huu ndo’ muda wako unaorudi nyumbani mimi nikiwa hospitali kumuuguza mtoto? Bryson!”

Bryson alikaa kimya, mke akaendelea kuongea akilalamika ya kwamba amemkuta mtoto aliyebakia nyumbani akiwa na njaa na amelala peke yake majira hayo ya usiku, alipomaliza kulalamika hayo akarejea kwenye swali lake, Bryson alikuwa ametokea wapi muda huo? Na akaongezea, kwanini hakuwa hapokei simu yake wala kujibu messages zake?

Bryson alikosa cha kujibu kwa muda huo, aliona kama kichwa chake kinafanya ziiiiii – ziiiiii- ziiiiii asielewe hata cha kufanya, upesi mke wake akanyanyuka kama radi na kumwendea kwenye kochi alilokaa, akampokonya simu na kuifungua, moja kwa moja akaenda kwenye ‘call logs’, huko akakuta mtu wa mwisho mwanaume huyo kuwasiliana naye alikuwa ni Hilda!

Mwanamke huyo akaanza kudondosha machozi kama mito ya baraka. Aliitupa simu ya mume wake kwenye kochi kisha akaenda zake chumbani. Korido nzima anavuta makamasi ya kilio. Aliamini kabisa kuwa Hilda ashamchukulia mwanaume wake. Moyo wake ulisinyaa kwa maumivu.

Bryson aliketi pale sebuleni kwa muda kidogo akiwaza mambo haya yanayojiri mbele ya macho yake. Alitaka kusimama kumwendea mke wake lakini akienda huko atamwambia nini akamwelewa? Hakuona jibu. Alikaa hapohapo sebuleni na nguo alizotoka nazo kazini mpaka usingizi ukamsomba, akakoroma kama nguruwe mdomo akiuacha wazi.

Jua linapokucha, aliamka akijikuta hapohapo kwenye kochi, akakurupuka kana kwamba amemwona mwizi. Alipotazama saa yake akashangaa kuona ni saa mbili kasoro asubuhi, upesi akanyanyuka kwenda kumtazama mke wake chumbani, hakumkuta! Akaenda pia kwenye chumba cha mtoto wake lakini pia vilevile hakumkuta, nyumba nzima alikuwa mwenyewe, mke hayupo na pia mtoto aliyekuwa amebakia naye hapa nyumbani hayupo. Akahisi kuchanganyikiwa.

Alipiga simu ya mkewe ikaita lakini haikupokelewa, akawaza kwenda hospitali lakini akienda huko itakuwa nini? Baada ya kufikiria kwa kina akaona ni stara kwenda kazini kuendelea na majukumu yake alafu akitoka huko, majira ya jioni, apitie hospitali kuungana na familia yake, pengine mke wake atakuwa amepunguza jazba. Akajiandaa na muda si mrefu, kama dakika arobaini na tano, akawa amefika kazini.

Huko akakutana na Richie. Alikaa hapo ofisini kwa kama dakika kumi na tano pasipo Hilda kutokea, akamuuliza Richie kama ana habari yoyote kumhusu mwanamke huyo, Richie akasema aliwasiliana naye mara ya mwisho jana mapema, hakupata kuwasiliana naye tena hivyo hajui kinachoendelea, siku ikazidi kusonga, wanaume hawa wawili, wote, wakiwa katika maswali na mashaka. Kila mmoja katika muda wake alimtafuta Hilda pasipo mafanikio, simu ilikuwa inaita lakini haipokelewi.

Yalipofika majira ya mchana, wakati wa mapumziko ya kupata chakula cha mchana, Richie akautumia muda huo kwenda nyumbani kwa Hilda kumjulia hali. Hakuweza kuvumilia mpaka jioni wakati wa kutoka kazini. Kila dakika iliposogea alijikuta anazidiwa na hofu na anapaliwa na woga. Alipofika huko, akaukuta mlango wa Hilda ukiwa wazi pasipo kufungwa na funguo, alitegua kitasa akaingia ndani na punde kidogo akabaini jambo ambalo hakulitegemea.

Jambo la kutisha.

Aliukuta mwili wa Hilda ukiwa kitandani, hauna uhai, damu zimetapakaa kwenye godoro na shuka. Maiti ya mwanamke huyo imeachama mdomo na macho wazi!



***
aliyemuua hilda atakuwa ni yule bwana wa mitchele aliyekuwa anawafatilia kuanzia kitambo,bado zamu ya richie
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 38.


Na Steve B.S.M


RICHIE aliishiwa nguvu za miguu akajikuta anaketi chini. Kwa muda kidogo hakujua afanye nini kwani akili yake ili-jam, haelewi anachokiona, ni baada ya dakika kadhaa ndipo alipata akili ya kutoa taarifa akapiga 911 na muda si mrefu gari ya wagonjwa ikafika ikiongozana na maafisa wa polisi. Richie akampa taarifa Bryson naye mwanaume huyo akafika katika eneo la tukio si muda mrefu, jasho linamtoka, moyo unamwenda mbio.

Alimkuta Richie yuko pembeni ya gari la polisi, akamfuata ampatie habari kwani yale aliyomweleza kwenye simu alihisi kutoelewa vema.

“Boss, kuna mtu amemuua, Hilda,” Richie alisema kwa uchungu. Macho yake mekundu na anatetemeka mwili mzima. Alimkumbatia Bryson akashindwa kujihimili, akajikuta analia kama mtoto, sasa kazi ya Bryson ikawa kumbembeleza.

Kidogo mwili wa Hilda ukatolewa ndani ukiwa juu ya machela, umefunikwa gubigubi, ukawekwa kwenye gari la wagonjwa alafu gari hilo likatimka, Bryson akalitazama mpaka linaishia, hakuamini ule ndo’ ulikuwa mwisho wa yeye kumwona Hilda. Punde afisa mmoja wa askari akawafuata na kuwataka wanaume hao wawili waelekee kituo cha polisi kwaajili ya kutoa maelezo kama watu wa karibu na mhanga wa mauaji.

Baada ya lisaa wakawa wapo ndani ya ofisi ya mpelelezi, wameketi nyuma ya meza kubwa nyeupe lakini kiti cha mpelelezi kipo tupu. Nje ya ofisi hiyo, koridoni kona ya pili, kulikuwa na ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, ndani ya ofisi hiyo Mkuu alikuwa ameketi kwenye kiti chake jasho linamvuja, mkononi ameshikilia simu inayoita.

Simu iliita kidogo ikapokelewa, Mkuu akauliza moja kwa moja: “Umempata Michael?” mtu wa upande wa pili akamjibu hapana, akaghafirika mno. “Sasa yupo wapi? Anajua kabisa yu mwenyewe hivi sasa na simu hapatikani siku ya pili hii! Sasa kweli hizi kesi nitawapa hawa maafisa wachanga?” kidogo akakata simu, akatoka ofisini kwake kwenda kuonana na afisa mmoja, bwana mdogo ambaye alikuwa miongoni mwa wale maafisa waliofika kwenye eneo la tukio, akampatia maelekezo mafupi kisha bwana huyo mdogo ndo’ akaenda kujumuika na wakina Bryson katika kile chumba cha mpelelezi.

Aliwahoji wahusika wake, mmoja baada ya mwingine, akarekodi kila alichosikia na kila kilichosemwa, baada ya hapo akachukua mawasiliano yao kisha akawaachia. Aliwaambia kwa sasa hawatakiwi kutoka nje ya jiji la New York mpaka pale upelelezi utakapokamilika kwani wanaweza wakahitajika muda wowote, lakini pia aliwataka waongeze uangalifu zaidi kwenye nyendo zao maana hamna anayejua ni nani alihusika na mauaji na lengo lake haswa ni nini.

Wakatoka ndani ya kituo na Bryson akanyookea moja kwa moja kwenye gari yake, akafungua mlango lakini kabla ya kuingia ndani akageuka nyuma kutazama, akamwona Richie amesimama mbali naye akiwa anamtazama tu, hakuelewa bwana huyo anawaza nini ama anafanya nini hapo, akapaza sauti kumuuliza; “vipi kuna shida?”

Richie hakujibu, aliendelea kusimama akimtazama, akakata shauri kumfuata. Alipomfikia akamuuliza nini kimejiri, Richie kwa sauti ya upole akamwambia anataka kwenda nyumbani.

“Sawa,” Bryson akamjibu na kumwambia, “twende nikupeleke.”

Richie akatikisa kichwa na kusema, “Nitaenda mwenyewe.” Kisha akaondoka zake akimwacha boss wake kwenye butwaa.

“Ana nini huyu?” Bryson alijiuliza mwenyewe asiwepo wa kumjibu.



***

Haven of Peace Hotel, New York. Majira ya saa nane mchana.


Mkuu wa upelelezi alitazama barabarani kushoto na kulia akiwa mbele kabisa ya hoteli hii. Bwana huyo alikuwa amesimama hapo mwenyewe, amevalia suti ya kijivu na miwani ya jua.

Alitazama saa yake ya mkononi kisha akatazama tena kushoto na kulia barabarani, upande wa kulia akaliona gari moja ambalo lilimteka hisia zake, SUV nyeusi na maridadi, gari hilo halikuwa na ‘plate number’ na mwendo wake ulikuwa wa wastani. Katika magari yote ambayo yalikuwapo barabarani, hili ndo’ liliteka macho ya mkuu.

Kitambo kidogo gari hilo lilifika mbele ya hoteli, akashuka kijana Babyface. Kijana huyo alikuwa amevalia suti nyeusi maridadi, uso wake hauna matani, alimtazama mkuu wa upelelezi akamsalimu kisha akaendelea na mambo yake, mambo ya kutazama usalama wa hapa na pale. Alipojiridhisha akafungua mlango wa gari akashuka bwana mmoja upesi, bwana huyo alikuwa amevalia shati rangi ya ugoro na suruali nyeusi ya kitambaa, kichwani amejivesha kofia aina ya fedora, rangi yake nyeupe.

Bwana huyo pasipo kumsalimia Mkuu wa upelelezi akaingia ndani ya hoteli moja kwa moja nyuma yake akiwa anafuatwa na Babyface kisha mkuu wa upelelezi kwa nyuma kabisa.

Alitembea kwa ufupi akiwa ametupa mgongo, alipofika mahali anapoelekea, chumba kidogo cha makutano, ndipo akavua kofia yake na kumtazama mwenyeji wake hapa. Kumbe bwana huyo alikuwa ni Brendan Garret, mkuu wa shirika la ujasusi wa nje nchini Marekani, yaani CIA. Ni wazi hakuwa hapa kwa kikao maalum cha serikali, nguo alizovaa zilisema hivyo; hayupo eneo hili kiofisi.

Mhudumu, mwanamke aliyevalia sare nadhifu, alifika akawasikiliza wateja wake, wateja wakaagiza maji akaenda zake, hapo ndo’ maongezi rasmi yakaanza.

“Umefikia wapi kuhusu Mpelelezi?” Garret aliuliza akimtazama Mkuu wa upelelezi, kando yake ameketi Babyface, wote sura zao zimejifunga kwa umakini. Mabwana hawa walikuwa wanamtazama Mkuu huyu kana kwamba ‘drafti’ linalodai akili.

“Well …” Mkuu wa upelelezi akafungua kinywa, “nimefanya kila jitihada zilizopo ndani ya uwezo wangu na nimethibitisha kuwa kweli amekufa.”

“Kivipi?” Garret akauliza. “Umethibitishaje kuwa amekufa?”

Mkuu wa upelelezi akatoa mkoba wake ambao ulikuwa chini ya meza kwa muda wote huo, na hilo likathibitisha bwana huyu alikuwapo hapa kwa kitambo kidogo. Katika mkoba huo alitoa bahasha moja ya kaki, akamnyooshea bwana Garret, Babyface akaidaka kwanza na yeye ndo’ akaifungua kutazama ndani. Alitoa picha kadhaa akamkabidhi bwana Garret kisha akatoa na karatasi kadhaa zenye maelezo na mihuri, akamkabidhi pia bwana Garret.

Mkuu wa upelelezi akasema, “huo ni uthibitisho. Mahali ambapo mwili wake ulipokelewa na kuhifadhiwa, mpaka na vipimo vya DNA vya mabaki ambayo hayakuwa na uwezekano wa kutambulika kwa macho ya kawaida, vyote vinathibitisha alikuwa ni mpelelezi. Ni bayana ame---” akasita kumalizia, mhudumu alikuwa anaingia na yale alokuwa ameagizwa, alipoyaweka na kuweka kila kitu sawa aliondoka zake Mkuu wa upelelezi akaendelea habari yake, habari ya kuthibitisha kuwa mpelelezi amefariki kwenye ajali ile mbaya.

Maelezo yake pamoja na vielelezo alivyotoa vikamkosha bwana Garret, aliamini hamna shaka sasa kuhusu kifo cha mpelelezi. Alimkabidhi nyaraka zile Babyface, naye bwana huyo akazirejesha kwenye bahasha kisha akatulia nazo.

“Kitu pekee nilichokuwa nahofia ni kumbukumbu za mpelelezi,” akasema bwana Garret, “laiti angelikumbuka hata lepe ya yale yaliyotokea nyuma ambayo najua hata wewe unayafahamu vema basi tungekuwa katika matata makubwa. Nashukuru mpaka kifo chake hilo halikupata kutokea, sijilaumu kwanini nilingoja. Lakini pili nashukuru hakupata kitu chochote kumhusu yule mwanamke tunayemtafuta, hata kama alipata kitu basi hivi sasa hakina maana tena, mwili mfu hausimulii hadithi.”

Akaweka kituo anywe maji, alipofanya hivyo akaendelea kunena, mara hii uso wake ukionyesha kuzama kwenye fikra.

“Lakini kipya ninachowaza hivi sasa ni kwamba, unadhani ile ajali ya mpelelezi ilikuwa ni ajali asili? Kama sivyo, ni nani ambaye angetaka kumuua bwana yule na kwasababu zipi?” alipouliza hayo alimtazama Mkuu wa upelelezi akamuuliza, “au unajua lolote?”

Mkuu akamwambia hajui kitu kwani oparesheni ambayo alikuwa anaifanya mpelelezi ilikuwa nje ya utaratibu, alisimamishwa kazi kwa wakati huo kwasababu ya utovu wa nidhamu, haswa kukaidi kuwa mkabala na mshirika ambaye alipatiwa.

Alisema, “Kama kungekuwa na jambo la siri katika tukio lile basi ningelijua, ama nitalijua. Lakini kwa mazingira niliyoyakagua na vijana wangu mpaka sasa, sina budi kuamini ajali ile ilikuwa ni ya asili. Madereva wote wawili walikamatwa na mazingira yote ya ajali yakajieleza bayana, hitilafu ya gari.”

Basi baada ya maelezo hayo, waligongesha glasi zao za maji kwa kujipongeza kisha maongezi yalofuatia baada ya hapo yakawa maongezi mepesi, maongezi ya kusogezea muda zaidi kuliko ya kumaanisha.

Swali likiachwa kwetu, ni kumbukumbu gani ambayo iliwafanya wakuu hawa wawili kuogopa nyendo za Mpelelezi? Lakini je, kama hofu hiyo haikuhusika na ajali ile kwa vyovyote, basi ni nini kilikuwa nyuma ya ajali ile mbaya kupata kutokea?


***

Majira ya Saa kumi na mbili ya jioni:

“Nimeshafika, nipo hapa chini.” Alisema Jamal kwenye simu akiwa ameegamia gari, mbele yake kumesimama jengo kubwa analolitazama, jengo ambalo ndani yake ndimo Richie anapata kuishi.

Muda si mrefu, kama baada ya dakika tatu, Richie akatokea kujiunga na Jamal. Bwana huyo alikuwa amevalia tisheti kubwa na bukta fupi, miguu yake ameisitiri kwenye ‘crocs’. Macho yake ni mekundu sana, haikuhitaji shule kujua ametoka kumwaga machozi muda si mwingi ulopita.

Jamal alimkumbatia bwana huyo kumpa faraja kisha akamuuliza ni nini kimetokea kwani alimvyompigia simu hakumweleza mengi, lakini swala hilo likageuka kuwa mtihani mgumu sana kwa Richie. Kila alipojaribu kueleza alijikuta anakabwa na uchungu kooni, taswira ya mwili wa Hilda usokuwa na uhai haikumuacha akakaa salama.

Kama baada ya dakika kadhaa ndipo angalau aliweza kumudu kifua chake akafungua kinywa na kuongea:

"Jamal, Bryson amemuua Hilda."

Jamal akatoa macho kwa butwaa. Richie akaongezea,

"Nina uhakika aslimia mia, yeye ndo' kamuua Hilda."


***
 
Back
Top Bottom