Tukibaki Hai, Tutasimulia

aliyemuua hilda atakuwa ni yule bwana wa mitchele aliyekuwa anawafatilia kuanzia kitambo,bado zamu ya richie
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 38.


Na Steve B.S.M


RICHIE aliishiwa nguvu za miguu akajikuta anaketi chini. Kwa muda kidogo hakujua afanye nini kwani akili yake ili-jam, haelewi anachokiona, ni baada ya dakika kadhaa ndipo alipata akili ya kutoa taarifa akapiga 911 na muda si mrefu gari ya wagonjwa ikafika ikiongozana na maafisa wa polisi. Richie akampa taarifa Bryson naye mwanaume huyo akafika katika eneo la tukio si muda mrefu, jasho linamtoka, moyo unamwenda mbio.

Alimkuta Richie yuko pembeni ya gari la polisi, akamfuata ampatie habari kwani yale aliyomweleza kwenye simu alihisi kutoelewa vema.

“Boss, kuna mtu amemuua, Hilda,” Richie alisema kwa uchungu. Macho yake mekundu na anatetemeka mwili mzima. Alimkumbatia Bryson akashindwa kujihimili, akajikuta analia kama mtoto, sasa kazi ya Bryson ikawa kumbembeleza.

Kidogo mwili wa Hilda ukatolewa ndani ukiwa juu ya machela, umefunikwa gubigubi, ukawekwa kwenye gari la wagonjwa alafu gari hilo likatimka, Bryson akalitazama mpaka linaishia, hakuamini ule ndo’ ulikuwa mwisho wa yeye kumwona Hilda. Punde afisa mmoja wa askari akawafuata na kuwataka wanaume hao wawili waelekee kituo cha polisi kwaajili ya kutoa maelezo kama watu wa karibu na mhanga wa mauaji.

Baada ya lisaa wakawa wapo ndani ya ofisi ya mpelelezi, wameketi nyuma ya meza kubwa nyeupe lakini kiti cha mpelelezi kipo tupu. Nje ya ofisi hiyo, koridoni kona ya pili, kulikuwa na ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, ndani ya ofisi hiyo Mkuu alikuwa ameketi kwenye kiti chake jasho linamvuja, mkononi ameshikilia simu inayoita.

Simu iliita kidogo ikapokelewa, Mkuu akauliza moja kwa moja: “Umempata Michael?” mtu wa upande wa pili akamjibu hapana, akaghafirika mno. “Sasa yupo wapi? Anajua kabisa yu mwenyewe hivi sasa na simu hapatikani siku ya pili hii! Sasa kweli hizi kesi nitawapa hawa maafisa wachanga?” kidogo akakata simu, akatoka ofisini kwake kwenda kuonana na afisa mmoja, bwana mdogo ambaye alikuwa miongoni mwa wale maafisa waliofika kwenye eneo la tukio, akampatia maelekezo mafupi kisha bwana huyo mdogo ndo’ akaenda kujumuika na wakina Bryson katika kile chumba cha mpelelezi.

Aliwahoji wahusika wake, mmoja baada ya mwingine, akarekodi kila alichosikia na kila kilichosemwa, baada ya hapo akachukua mawasiliano yao kisha akawaachia. Aliwaambia kwa sasa hawatakiwi kutoka nje ya jiji la New York mpaka pale upelelezi utakapokamilika kwani wanaweza wakahitajika muda wowote, lakini pia aliwataka waongeze uangalifu zaidi kwenye nyendo zao maana hamna anayejua ni nani alihusika na mauaji na lengo lake haswa ni nini.

Wakatoka ndani ya kituo na Bryson akanyookea moja kwa moja kwenye gari yake, akafungua mlango lakini kabla ya kuingia ndani akageuka nyuma kutazama, akamwona Richie amesimama mbali naye akiwa anamtazama tu, hakuelewa bwana huyo anawaza nini ama anafanya nini hapo, akapaza sauti kumuuliza; “vipi kuna shida?”

Richie hakujibu, aliendelea kusimama akimtazama, akakata shauri kumfuata. Alipomfikia akamuuliza nini kimejiri, Richie kwa sauti ya upole akamwambia anataka kwenda nyumbani.

“Sawa,” Bryson akamjibu na kumwambia, “twende nikupeleke.”

Richie akatikisa kichwa na kusema, “Nitaenda mwenyewe.” Kisha akaondoka zake akimwacha boss wake kwenye butwaa.

“Ana nini huyu?” Bryson alijiuliza mwenyewe asiwepo wa kumjibu.



***

Haven of Peace Hotel, New York. Majira ya saa nane mchana.


Mkuu wa upelelezi alitazama barabarani kushoto na kulia akiwa mbele kabisa ya hoteli hii. Bwana huyo alikuwa amesimama hapo mwenyewe, amevalia suti ya kijivu na miwani ya jua.

Alitazama saa yake ya mkononi kisha akatazama tena kushoto na kulia barabarani, upande wa kulia akaliona gari moja ambalo lilimteka hisia zake, SUV nyeusi na maridadi, gari hilo halikuwa na ‘plate number’ na mwendo wake ulikuwa wa wastani. Katika magari yote ambayo yalikuwapo barabarani, hili ndo’ liliteka macho ya mkuu.

Kitambo kidogo gari hilo lilifika mbele ya hoteli, akashuka kijana Babyface. Kijana huyo alikuwa amevalia suti nyeusi maridadi, uso wake hauna matani, alimtazama mkuu wa upelelezi akamsalimu kisha akaendelea na mambo yake, mambo ya kutazama usalama wa hapa na pale. Alipojiridhisha akafungua mlango wa gari akashuka bwana mmoja upesi, bwana huyo alikuwa amevalia shati rangi ya ugoro na suruali nyeusi ya kitambaa, kichwani amejivesha kofia aina ya fedora, rangi yake nyeupe.

Bwana huyo pasipo kumsalimia Mkuu wa upelelezi akaingia ndani ya hoteli moja kwa moja nyuma yake akiwa anafuatwa na Babyface kisha mkuu wa upelelezi kwa nyuma kabisa.

Alitembea kwa ufupi akiwa ametupa mgongo, alipofika mahali anapoelekea, chumba kidogo cha makutano, ndipo akavua kofia yake na kumtazama mwenyeji wake hapa. Kumbe bwana huyo alikuwa ni Brendan Garret, mkuu wa shirika la ujasusi wa nje nchini Marekani, yaani CIA. Ni wazi hakuwa hapa kwa kikao maalum cha serikali, nguo alizovaa zilisema hivyo; hayupo eneo hili kiofisi.

Mhudumu, mwanamke aliyevalia sare nadhifu, alifika akawasikiliza wateja wake, wateja wakaagiza maji akaenda zake, hapo ndo’ maongezi rasmi yakaanza.

“Umefikia wapi kuhusu Mpelelezi?” Garret aliuliza akimtazama Mkuu wa upelelezi, kando yake ameketi Babyface, wote sura zao zimejifunga kwa umakini. Mabwana hawa walikuwa wanamtazama Mkuu huyu kana kwamba ‘drafti’ linalodai akili.

“Well …” Mkuu wa upelelezi akafungua kinywa, “nimefanya kila jitihada zilizopo ndani ya uwezo wangu na nimethibitisha kuwa kweli amekufa.”

“Kivipi?” Garret akauliza. “Umethibitishaje kuwa amekufa?”

Mkuu wa upelelezi akatoa mkoba wake ambao ulikuwa chini ya meza kwa muda wote huo, na hilo likathibitisha bwana huyu alikuwapo hapa kwa kitambo kidogo. Katika mkoba huo alitoa bahasha moja ya kaki, akamnyooshea bwana Garret, Babyface akaidaka kwanza na yeye ndo’ akaifungua kutazama ndani. Alitoa picha kadhaa akamkabidhi bwana Garret kisha akatoa na karatasi kadhaa zenye maelezo na mihuri, akamkabidhi pia bwana Garret.

Mkuu wa upelelezi akasema, “huo ni uthibitisho. Mahali ambapo mwili wake ulipokelewa na kuhifadhiwa, mpaka na vipimo vya DNA vya mabaki ambayo hayakuwa na uwezekano wa kutambulika kwa macho ya kawaida, vyote vinathibitisha alikuwa ni mpelelezi. Ni bayana ame---” akasita kumalizia, mhudumu alikuwa anaingia na yale alokuwa ameagizwa, alipoyaweka na kuweka kila kitu sawa aliondoka zake Mkuu wa upelelezi akaendelea habari yake, habari ya kuthibitisha kuwa mpelelezi amefariki kwenye ajali ile mbaya.

Maelezo yake pamoja na vielelezo alivyotoa vikamkosha bwana Garret, aliamini hamna shaka sasa kuhusu kifo cha mpelelezi. Alimkabidhi nyaraka zile Babyface, naye bwana huyo akazirejesha kwenye bahasha kisha akatulia nazo.

“Kitu pekee nilichokuwa nahofia ni kumbukumbu za mpelelezi,” akasema bwana Garret, “laiti angelikumbuka hata lepe ya yale yaliyotokea nyuma ambayo najua hata wewe unayafahamu vema basi tungekuwa katika matata makubwa. Nashukuru mpaka kifo chake hilo halikupata kutokea, sijilaumu kwanini nilingoja. Lakini pili nashukuru hakupata kitu chochote kumhusu yule mwanamke tunayemtafuta, hata kama alipata kitu basi hivi sasa hakina maana tena, mwili mfu hausimulii hadithi.”

Akaweka kituo anywe maji, alipofanya hivyo akaendelea kunena, mara hii uso wake ukionyesha kuzama kwenye fikra.

“Lakini kipya ninachowaza hivi sasa ni kwamba, unadhani ile ajali ya mpelelezi ilikuwa ni ajali asili? Kama sivyo, ni nani ambaye angetaka kumuua bwana yule na kwasababu zipi?” alipouliza hayo alimtazama Mkuu wa upelelezi akamuuliza, “au unajua lolote?”

Mkuu akamwambia hajui kitu kwani oparesheni ambayo alikuwa anaifanya mpelelezi ilikuwa nje ya utaratibu, alisimamishwa kazi kwa wakati huo kwasababu ya utovu wa nidhamu, haswa kukaidi kuwa mkabala na mshirika ambaye alipatiwa.

Alisema, “Kama kungekuwa na jambo la siri katika tukio lile basi ningelijua, ama nitalijua. Lakini kwa mazingira niliyoyakagua na vijana wangu mpaka sasa, sina budi kuamini ajali ile ilikuwa ni ya asili. Madereva wote wawili walikamatwa na mazingira yote ya ajali yakajieleza bayana, hitilafu ya gari.”

Basi baada ya maelezo hayo, waligongesha glasi zao za maji kwa kujipongeza kisha maongezi yalofuatia baada ya hapo yakawa maongezi mepesi, maongezi ya kusogezea muda zaidi kuliko ya kumaanisha.

Swali likiachwa kwetu, ni kumbukumbu gani ambayo iliwafanya wakuu hawa wawili kuogopa nyendo za Mpelelezi? Lakini je, kama hofu hiyo haikuhusika na ajali ile kwa vyovyote, basi ni nini kilikuwa nyuma ya ajali ile mbaya kupata kutokea?


***

Majira ya Saa kumi na mbili ya jioni:

“Nimeshafika, nipo hapa chini.” Alisema Jamal kwenye simu akiwa ameegamia gari, mbele yake kumesimama jengo kubwa analolitazama, jengo ambalo ndani yake ndimo Richie anapata kuishi.

Muda si mrefu, kama baada ya dakika tatu, Richie akatokea kujiunga na Jamal. Bwana huyo alikuwa amevalia tisheti kubwa na bukta fupi, miguu yake ameisitiri kwenye ‘crocs’. Macho yake ni mekundu sana, haikuhitaji shule kujua ametoka kumwaga machozi muda si mwingi ulopita.

Jamal alimkumbatia bwana huyo kumpa faraja kisha akamuuliza ni nini kimetokea kwani alimvyompigia simu hakumweleza mengi, lakini swala hilo likageuka kuwa mtihani mgumu sana kwa Richie. Kila alipojaribu kueleza alijikuta anakabwa na uchungu kooni, taswira ya mwili wa Hilda usokuwa na uhai haikumuacha akakaa salama.

Kama baada ya dakika kadhaa ndipo angalau aliweza kumudu kifua chake akafungua kinywa na kuongea:

"Jamal, Bryson amemuua Hilda."

Jamal akatoa macho kwa butwaa. Richie akaongezea,

"Nina uhakika aslimia mia, yeye ndo' kamuua Hilda."


***
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…