TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 24
Na Steve B.S.M
Kabla hawajakaa vema, kitasa kikasukumwa. Wote wakatazama huko mlangoni.
Lakini kwasababu mlango ulikuwa umefungwa na funguo, haukufunguka. Badala yake ulilalama na kutulia tu.
Hilda akapaza sauti kuuliza ni nani aliyemlangoni huku uso wake wenye mashaka ukimtazama Richie.
Wote walikuwa na wazo moja. Mtu aliyekuwepo mlangoni ni boss Bryson, naye amekuja hapo kwaajili ya kazi alompa Hilda.
Jambo la bwana huyo kukaa kimya wakati aliahidi atawapigia muda si mrefu liliwafanya wakaamini hivyo.
Wakaogopa sana kwani kazi haikuwa imeisha wala hamna dalili ya kufikia kuimaliza masaa ya hivi karibuni.
Hapa hata Hilda akajutia kwanini alimpa Richie penzi lake. Kama muda huo wangekuwa wanafanya kazi basi wangekuwa wamesogeasogea hata kidogo.
Ona sasa ...
Alijilaumu kwa ujinga huo ... Lakini angefanya nini? Alifahamu fika Richie ni mwanaume anayempenda kwa dhati, hivyo kumpatia penzi kungemteka akawa anamfanyia kazi zake bwerere huku yeye akiwa anapokea pesa taslimu toka kwa Bryson.
Sasa, kwa kitambo kidogo, alijutia. Atamweleza nini Bryson?
Hofu ...
Hofu ya bure.
"Mimi Jamal!" Alisema mtu aliyekuwa amesimama mlangoni.
Hakuwa anatania.
Sauti yake ilishuhudia.
Richie anaijua vema hata akishtuliwa usingizini. Bwana huyu amesoma naye kwa miaka kadhaa.
Yeye ndo' akaamka na kwenda mlangoni upesi.
Alivyokuwa anatembea, nguo yake ya ndani ilikuwa inapepea kana kwamba pazia la ufukweni.
Miguu yake membamba ilimfanya aonekane amevaliwa na chupi na siyo yeye kaivaa chupi.
Alifungua mlango akakutana uso kwa uso na Jamal. Bwana huyo alikuwa amevalia tisheti nyeusi yenye maneno meupe: I RUN NEW YORK.
Chini amevalia jeans iliyopauka na raba kali nyeupe, chapa ya New Balance.
Nguo zilikaa katika mwili wake kana kwamba amezitengeneza yeye, ama aliziwekea 'order' kiwandani.
Mgongoni mwake alibebelea begi jeusi lenye mikanda membamba ... Begi lililoonekana tupu kwa kiasi chake kikubwa.
Bwana huyo alistaajabu kumwona Richie katika mavazi yale. Macho yake yakauliza lakini kinywa chake hakikufunguka.
Akakaribishwa sebuleni alipoketi na kuuliza moja kwa moja alipo mwenyeji wa makazi hayo, hapo kidogo akatokea Hilda akiwa amevalia gauni jepesi, usoni amevalia tabasamu changa.
Alimsalimu akamkaribisha.
"Richie ameniambia mengi kuhusu wewe," alisema akimkarimu mgeni huyu, kisha na kuongezea, "lakini nashangaa alikuwa hajui kama unakuja mpaka akanijengea hofu nani anagonga mlango majira haya?"
Baada ya hayo majadiliano mafupi ya nani aliyekuwa mlangoni, huyu akisema hivi na yule akisema vile, na Richie akijitetea kuwa alisahau kabisa kwasababu ya kumezwa na kazi, wakaenda kwenye kile kilichowakutanisha hapa.
Jamal akasema ameitikia wito wa Richie kuja kuibeba kazi kwaajili ya mwendelezo wa pale walipoishia, hivyo kama ipo tayari basi apewe aondoke zake.
"Ngoja kidogo," Richie akamtuliza. "Kazi bado hatujaimaliza. Hata hapa bado tulikuwa tunahangaika nayo kwasabau inatakiwa muda si mrefu."
Alipofikia hapo, Richie akamwomba Jamal kuwa kama itawezekana awasaidie kuongeza nguvu kwenye kuimaliza kazi ile ili wapishe ratiba zingine.
Kidogo Jamal akawa mgumu.
"Lakini haya ni nje ya makubaliano yetu."
Richie akambembeleza akimwomba kama rafiki na sio mwenza wa kikazi sasa. Jamal akaridhia japo kishingo upande.
Alipiga mahesabu kichwani kwake akaona ni vema tu afanye hivyo kwani asipofanya basi hatopata kazi ya kuondoka nayo.
Na asipopata kazi hiyo maana yake hamna pesa.
Pesa anaitaka.
Basi wakiwa watatu wakaishambulia kazi hiyo kwa kasi waliyoimudu, kila mmoja katika uwanja wa tarakilishi ... Richie na Hilda wakitumia tarakilishi mpakato wakati Jamal akitumia ya mezani ilokuwepo hapa sebuleni.
Wakiwa wanafanya hivyo, bado Hilda akawa wa kutazama simu yake mara kwa mara.
Hakuna aliyepiga.
Hakujua kwanini lakini alihisi kuna kitu hakipo sawa.
Shaka hili alisema na moyo wake ...
----
Majira ya saa sita ya usiku ...
Taa za gari zilimulika kwa makali yake wakati gari likikata kona hii ya mwisho ya barabara kabla ya kuingia katika mtaa huu wa makazi.
Baada ya hapo, likatembea kwa kama mita ishirini hivi kisha likasimama na kuzima taa.
Mahali hapa palikuwa na ukimya wa usiku japo watu wachache hawakukosa kuonekana huku na kule wakikatiza mmojammoja, haswa kwa wanaume.
Majengo ya ghorofa yalokuwepo hapa yalikuwa yamewasha taa zake kwenye madirisha lukuki ya vyumba ... ni vyumba vichache tu ndo' vilibakiwa na kiza kwa ndani yake.
Bwana dereva akashuka toka kwenye gari yake na kuendea ghorofa mojawapo kwa mwendo wake wa kasi.
Hatua zake zilikuwa pana na mwendo wake wa ukakamavu kana kwamba mwanajeshi.
Alikwea ngazi na ghorofa ya pili tu, akawa amefika anapoelekea ... Mbele ya mlango, chumba namba 524.
Korido hili lilikuwa na mwanga hafifu. My
Taa ilikuwapo moja tu, japo ilikuwa na mwanga mkali lakini haikutosha kumulika korido yote kwa usawa.
Taa zingine zilishageuka kuwa historia. Ukizitazama unajua tu hazijaaribika leo, jana wala juzi, bali 'mamiezi' yalopita.
Yalishageuka kuwa maskani za buibui.
Bwana akagonga mlango mara moja na kabla hajaitikiwa, akabinua kitasa aufungue mlango.
Mlango haukufunguka.
Akaingiza mkono wake mfukoni na kuutoa ufunguo.
Kabla hajauzamisha ufunguo huo katika kitasa chake, akatazama kwanza kushoto kwa udadisi ... Hapo angalau akaonekana ni nani kwani mwanga ulokuwepo upande huo ulinawirisha uso wake japo kwa udogo.
Alikuwa ni bwana Bryson!
Alouchomeka ufunguo na kutegua kitasa. Mlango ukafunguka akaingia ndani kwa dhamira dhabiti.
Sebule ilikuwa na mwanga wa kutosha lakini hamna mtu hapo.
Ilikuwa ni tupu.
Tarakilishi iliyokuwepo mezani ilikuwa inawaka, na kwenye kochi kulikuwa na tarakilishi ya kupakata ikiwa imefungwa.
Bryson aliifuata tarakilishi hiyo akaishika ... ilikuwa ya moto.
Haikuwa imefungwa muda.
Akaielekea tarakilishi ilokuwepo mezani lakini kabla hajafika, mlango wa chumbani ukafunguka, akatoka Hilda.
Alikuwa amevalia taulo jeupe kifuani. Kichwani ana kiremba cha taulo pia. Uso wake mnene upo uchi bila ya miwani.
Akastaajabu,
"Oh ... Bryson!"
Kisha akaanza kujielezea kwa haya,
"Nilikuwa nangoja simu yako, nilijua utapiga si muda mrefu. Mbona ukawa kimya? ... Ooh ulikuwa unaendesha sio? Usingeweza kupiga simu ..."
Akatabasamu. Wakati huo Bryson aliendelea kutazamatazama huku na kule mara kadhaa kana kwamba kuna kitu anashuku.
Hakuchukua muda, wala kusema mambo mengi, akamwambia Hilda kuwa amefuata kazi hiyo mwenyewe.
Anaihitaji awekewe kwenye 'Flash drive'.
Akaitoa flash hiyo na kumpatia.
"Kwahiyo vipi tena kuhusu barua pepe?" Hilda akauliza, "Umeghairisha? ...." A
Kisha akacheka kidogo tusijue hata ni nini kilochomfurahisha "... Ilikuwa ni kazi kubwa sana, boss. Laiti ningepumzika basi nisingeweza kuimaliza kwa wakati kabisa ..."
Aliendelea kuongea mwenyewe mpaka mchakato wa kuhamisha taarifa ulipomalizika.
Akampatia Bryson flash akisema,
"Lakini boss, kwanini usiku wote huu na ghafla hivi?"
Bryson akamwambia alipata dharura, baada ya hapo akaenda zake.
Hilda akamtazama kwa maswali yaliyoendelea hata baada ya mwanaume huyo kufunga mlango wake.
Akaufuata mlango na kuufunga kwa ufunguo, alipogeuka akakutana na Richie aliyetoka mafichoni.
Kidogo naye Jamal akaungana naye.
"Atakuwa amegundua?" Richie akauliza.
"Sidhani ..." Hilda akajibu akipandisha mabega yake. "Lakini si kawaida yake kutokukaa ..." Akamalizia akiketi kitini.
Macho yamezama kwenye mawazo akijaribu kuelewa kinachoendelea.
"Inaonekama ana haraka sana," Richie akasema na kuongeza, "lakini amewezaje kufungua mlango na uliufunga kwa funguo? ... Ina maana ana ufunguo wako?"
Hilda hakujibu.
Badala yake alinyanyuka akaelekea zake chumbani.
Richie akakubaliana na nafsi yake kwamba hapa kuna kitu kinaendelea.
Kitu fulani asichokijua.
----
Alipojiweka tu kwenye kiti, akaubamiza mlango wa gari kuufunga alafu akatulia hapo kidogo.
Akawa anawaza.
Taratibu akayapitia yale matukio aliyotoka kuyaona kule kwenye makazi ya Hilda, akashindwa kujua nini kinajiri.
Kwanini Hilda aliongopa ametoka kuoga ingali mgongo wae ulionekana kuwa mkavu, haujapata hata tone la maji? ... Ni kifua chake ndicho kilikuwa na matonetone kuonyesha ametoka bafuni.
Kama hakutoka kuoga, kwanini alikawia kuja sebuleni alipofungua mlango? Alikuwa anafanya nini?
Tarakilishi mbili sebuleni zilizokuwa zinafanya kazi, moja ikiwa imezimwa muda si mrefu ... sehemu kubwa ya kiti kikubwa cha sebuleni kubonyea ... Hivi vikampa mashaka.
Kweli Hilda alikuwa mwenyewe?
Kama hakuwa mwenyewe alikuwa na nani? Na huyo mtu anafahamu kuhusu kazi wanayoifanya?
Na kama anaifahamu ...
Hapa akasita ... Aliona panatisha ... akabamiza kichwa chake akilaani anachokiwaza...
Akawasha gari lake na kuondoka upesi.
Akiwa njiani, akajilazimisha sana kuyasahau haya yaliyotokea hapa ili aweze kufikiria namna ya kunusuru afya za watoto wake.
Kwenye hilo, kama alivyokuwa amepanga hapo awali, akawaza hii 'data' alonayo mkononi ahakikishe haitumi kwa namna yoyote ile.
Badala yake ashinikize kuonana na mwanamke yule ili apate fursa ya kumweleza shida zake.
Kwa alivyokiwa anajua, kila anapopewa kazi ya kufanya, basi huchukua siku mbili kabla ya kuanza kuulizwa kama imekamilika au lah.
Hivyo Jua likichomoza, kabla halijafika katikati ya anga, atapokea simu ya kumuuliza hilo, na hiyo itakuwa mara ya kwanza kusema kazi imekwisha.
Tangu amefanya kazi hiyo hajawahi tumia siku mbili tu kuikamilisha.
Na kwasababu hana uwezo wa kuwasiliana na mteja huyo mpaka yeye mwenyewe mteja atakapopiga, basi hiyo itakuwa ni fursa adhimu kwake.
Kwasababu kazi imekwishakukamilika, basi atakata shauri kumwona.
Akaendesha gari njia nzima akiwaza hilo.
Hiyo ndo' ilikuwa njia yake ya pekee ya kupata pesa kubwa anayoitaka.
---
"Unadhani atagundua?" Richie aliuliza.
Hilda alikuwa amesimama kando akiwa ameshika kiuno. Jamal alikuwa ameketi kwenye kochi anawatazama kana kwamba ni 'telemundo' mbele ya macho yake.
Hilda akashusha pumzi fupi. Akatembea hatua nne na kurudi tano. Akatembea tena na kurudi tano.
Kichwani mwake kulikuwa kumejaa.
Mawazo pomoni ...
Alikuwa anajenga ghorofa kichwani mwake kwa mawazo lukuki.
Richie akasema,
"Tatizo alikuja ghafla sana. Hatukuwa na muda wakuhamisha data zote kwa pamoja. Mpaka mlango unachokonolewa na funguo nilikuwa nimeweka data yangu na yako tu, ile ya Jamal sikupata muda kabisa. La sivyo angetukuta hapa!"
Kisha akauliza tena,
"Unadhani atajua kwamba data haijakamilika?"
Akajijibu mwenyewe.
"Hatajua bana ... Enh? Tusiwe na hofu sana, n'na hakika hajui hata kilichomo ndani."
Hilda akamtazama kwa macho makali,
"Serious?" Kisha akauliza.
"Na je, huyo aliyempa hiyo kazi? Yeye hatojua kuwa ni pungufu?"
Swali likawa gumu.
***