Asante sana mzee FMES kwa kutufahamisha mengi kuhusu huyu mwanamuziki mahiri tuliyewahi kuwa naye. Kuna mengi yaliyokuwa yanatokea Dar siyafahamu hasa kwa vile wakati huo mimi nilikuwa naishi huko Tabora, na nilikuwa nafika Dar kwa msimu tu kutumia treni inayosafiri siku mbili njiani usiku na mchana. Hata hivyo, naona ugumu sana kukubaliana nawe kuwa mtindo wa Koka Koka ulianza mwaka 1976, kwa vile mimi niliandika T-Shirt yangu neno Kokakoka mwaka 1975 nikiwa nalihusisha na Vijana Jazz. Inawezekana huo mtindo wa Kamata Sukuma ulitumika mwanzoni mwa mwaka 1974 na haukuvuma kabisa kwa vile mtindo wa kwanza kujulikana ulikuwa huu wa Koka Koka.
Turudi nyuma tena; kumbuka kuwa kati ya mwaka 1975 na 1976 Vijana Jazz walikuwa wanarekodi nyimbo zao kwa kutumia Label za Moto Moto na kama hii hapa.
Partial listing ya Catalogue ya Moto Moto inaoinyesha santuri zao kwa utaratibu ufuatao:
MOTO 7-907 : Sabina/Niliruka Ukuta - Vijana Jazz Band , 1975
MOTO 7-918 : Magdalina No 2/Miaka Mingi - Vijana Jazz Band , 1975
MOTO 7-922 : Koka Koka No 1/Ujirani Mwema - Vijana Jazz Band , 1975
MOTO 7-923 : Shangazi/Gwe Manetu Fii - Vijana Jazz Band, 1975
MOTO 7-928 : Pili Nihurumie/Zuhura Naondoka - Vijana Jazz Band, 1976
MOTO 7-930 : Unakufa Kiofisa/Wajue Vijana Jazz - Vijana Jazz Band, 1976
Unaona kuwa hata ule wimbo KokaKoka Namba 1 ulipigwa mwaka 1975, mwaka ambao wimbo wa Niliruka Ukuta ulipotolewa pia. Nina imani kuwa Zuhura Naondoka uliopigwa mwaka 1976 bado ulikuwa kwenye mtindo wa Koka Koka. Inawezekana nyimbo nyingine hazikuwekwa kwenye santuri, ila zilirekodiwa RTD tu. Unajua kuwa baada ya kuvunjika kwa EAC (1977,) kuna wakati mpaka wetu na Kenya ulikuwa umefungwa, na hivyo wanamuziki wengi wa Tanzania wakawa hawarekodi nyimbo zao huko Kenya tena; ndipo wakawa wanarekodia RTD kwa ajili ya kupiga redioni tu, wala hakukuwa na santuri tena. Nadhani hiyo ilipunguza sana mapato yao na hivyo kudororesha maendeleo ya Muziki kwa vile studio zote za kurekodi santuri zilikuwa Kenya.
Kwa wale ambao wanasikia jina la wimbo Niliruka Ukuta bila kuufahamu, nimefanikiwa kuupata online:
Gonga hapa uusikilize na kuuangusha (download MP3) kwenye computer yako ukiependa.