Wengi hawafahamu kuwa mwanamuziki aliyekuwa akiongoza mapinduzi kuanzia Juwata na hatimaye Sikinde ni Marehemu Abel Baltazar. Huyu ndiye alichangia kwa kiasi kikubwa kuanzishwa bendi ya Mlimani Park Orchestra! Na ni huyu huyu ndiye aliyeongoza 'mapinduzi' ya kuwahamisha wanamuziki sita wa Sikinde kwenda OSS na kuanzisha mtindo wa Ndekule na inasemekana ni yeye ndiye aliyewapeleka Mwanyiro, Dede na Mulenga Bima Lee. Pamoja na nguvu zote alizokuwa nazo Baltazar hakuwa na tamaa ya madaraka na ndio maana baada ya kuanzishwa 'Nginde' alimwachia Maalim Gurumo uongozi wa Bendi na ndivyo ilivyokuwa huko Ndekule.
Wakati wanamuziki wa Juwata wanahama na kaunzisha Sikinde wakishirikiana na wanamuziki wengine waliotoka Dar International kama Cosmas Thobias Chidumule Bitchuka hakuwemo alibakia Juwata na kuanzisha mtindo wa 'magoma kitakita' Utakubaliana nami kuwa katika zile nyimbo za kwanza za Sikinde sauti ya Bitchuka haikuwemo. Nyimbo kama Selina, Barua kutoka kwa Mama sehemu ya kwanza, Kassim Namba moja sauti ya Bitchuka haimo. Sauti zinazosikika mle ni za Gurumo, Marehemu Khamis Juma (Maalim Kinyasi), Cosmas Thobias Chidumule. Sauti ya Bitchuka utaisikia katika mkupuo wa pili wa kurekodi wa Sikinde. Nyimbo kama Kassim namba mbili unaweza kusikia sauti ya Bitchuka. Wakati Bitchuka anaondoka Msondo Shabaan Dede alikuwa ameshajiunga na ndio akawa akiongoza safu ya Uimbaji. Utakumbuka nyimbo kama Zuleka. Shabaan Dede Kamchape alitokea Dodoma International. Miaka ya Mwanzo ya 80 Msondo walijiimarisha kwa kumchua Moshi William kutoka bendi ya Polisi. Sauti ya Moshi akiwa Polisi Jazz utaisikia katika wimbo ule maarufu wa "Mwaka wa Watoto" ndani ya wimbo ule sauti ya Moshi inasikika ikilalamika... 'Unalewa bila kipimo hata watoto huwakumbuki'
Baadaye Dede alijiunga na Sikinde akitokea Msondo. Pamoja na kwamba Sikinde ilishawahi kuchukua wanamuziki kutoka Msondo tena wengi kwa mkupuo na labda maarufu kushinda Dede. Kuhama kwa Dede kulizua mtafaruku mkubwa sana! Siku moja pale Klabu ya Simba Dede alikuwa amesimama kwenye kituo cha basi, wapenzi wa msondo walimvamia na kumvua 'nguo za msondo' Kumbuka siku zile bendi zilikuwa zikitoa 'yunifomu' na ilikuwa ruksa 'kutoka' nazo mitaani au hata harusini.
Kuvuliwa nguo hadharani ndiko kulikopelekea Dede atunge wimbo wa 'Talaka Rejea' pale Msondo 'walipomwangukia' ili arudi kundini. Dede aliendelea kuwaimba msondo 'kama hana akili nzuri'. Kuna ule wimbo wenye maneno 'watoto wamekimbia nyumbani umebaki na wajukuu pia watasambaa' lilikuwa ni dongo la Said Mabera ambaye hajawahi kuhama Msondo tangu mwaka 1968 alipojiunga nayo.
Wakati Msondo ikipita kwenye kipindi kigumu baada ya kuondoka Dede, ndipo walipomnyakuwa mwanamuziki 'kinda' wakati huo kutoka Dar International. Naye si mwingine ni Fresh Jumbe Mkuu. Kwa taarifa yenu huyu ni miongoni mwa wanamuziki wachache ambao Jabali la muziki liliwapa nafasi ya kuimbisha. Wengi wa wanamuziki wa Marijan Rajabu walikuwa ni waitikiaji. Utakubaliana nami utakapousikiliza ule wimbo wa 'Masudi Jambazi' na 'Nyota Njema'.
Sikinde waliendelea kuishambulia Msondo kwa kumnyakua Fresh Jumbe baada ya Dede kwenda Bima Lee na Chidumule kuhamia Kurugenzi ya Arusha.
Msondo nao kwa kujiimarisha walimchukua Mwanamuziki kipofu kutoka Kenya aliyekuwa na Bendi ya Les Cuban ya Morogoro, Nico Zenge Kala na 'tunda' jingine la Marehemu Marijani, Marehemu Augustino Masenge au kama alivyokuwa akijulikana kama Tino Masinge. Wengi watakumbuka Nico ndiye mwanamuziki mtunzi wa wimbo wa Solemba ambao ndio ulikuja kuzaa maneno ya 'kuachwa solemba' Kuna wakati wanamuziki wa Les Cuban walishawahi kumtorosha Nico na kumrudisha Morogoro. Inasemekana Nico alisusa kula na kudai hatakula hadi amuone Said Mabera. Ilibidi arudishwe.
Kifo cha Nico hadi leo kwa wapenzi wa msondo wanaamini 'mbaya' alikuwa ni Shabaan Dede ambaye naye alisharudi Juwata baada ya kutoka Bima Lee. 'Mashambulizi' yalipomzidi Dede alijiengua msondo na kurudi Sikinde tena. Dede alianza kufanya visa na kisa cha mwisho alichofukuzwa Msondo yeye aliamua kwenda mpirani kuangalia mechi ya Simba na Coastal Union wakati wenzake walikuwa wanaporomosha muziki Amana. Watu walio karibu na Dede wanasema kinachomponza Dede kutopendwa na wenzake ni 'uwazi' alionao. Kama nyimbo zake zilivyo na 'madongo' na kauli zake ziko hivyo hivyo kwa maana nyingine wenzake hawapendi. Pamoja na yote ukweli utabakia kuwa Dede ni mtunzi mzuri wa nyimbo na ametunga nyimbo nyingi kuliko wanamuziki wengine wa Tanzania ukimwondoa TX Moshi William waliovuma kuanzia miaka ya mwisho ya sabini. Sina kumbukumbu nzuri za kina Mbaraka Mwishehe na Salum Abdalla. Naambiwa Mbaraka alikuwa akitungiwa nyimbo na 'ubabe' wake anasema katunga yeye.
Tuendelee. Msukosuko mkubwa ambao sitausahau ulikuwa ni wa Sikinde kupoteza wanamuziki saba kwa mkupuo waliohamia OSS. Suala hapa halikuwa idadi kubwa ya ya wanamuziki bali ni umuhimu wa wanamuziki hao. Majina ambayo bado nayakumbuka hapa walikuwemo, Maalim Gurumo, Hassan Bitchuka, Fresh Jumbe, Benno Villa Anthony, Khamis Kinyasi, (waimbaji) Marehemu Kassim Rashid (Solo) na Charles John Ngosha (Bass) Ukiangalia hapo safu ya waimbaji waliobaki Sikinde walikuwa ni Marehemu Francis (Nasri) Lubua na Maximillian Bushoke.
Ilibidi uongozi wa DDC chini ya Marehemu Mohamed Mpocho, (Meneja Mkuu DDC) Marehemu Hezron Mwampulo (Meneja wa Bendi) wahahe hadi usiku wa manane na kufanikiwa kumrudisha Benno Villa Anthony. Na wakati huo huo kufanya na mawasiliano na Chidumule aliyekuwa Kurugenzi Arusha. Na kwa haraka haraka kuwachukua Marehemu Mohamed Mwinyikondo (sina hakika nadhani alitoka Lola Africa ya Buguruni) na Hussein Jumbe kutoka Urafiki.
Onyesho la kwanza la 'Nginde' baada ya kuondoka kina Gurumo lilifanyika pale DDC Magomeni. Ukumbi ulijaa kuangalia Sikinde itaimba bila 'mastaa' wake. Ukweli ni kwamba mapengo yote yalizibwa. Pengo la Gurumo lilizibwa na Meddy Mwinyikondo, la Bitchuka lilizibwa na Francis Lubua (Mbuyu wa Sikinde) na kina Cosmas na Bushoke waliimarisha sauti ya pili, bila kumsahau Benno. Baadaye sikinde walimchukua Tino Masinge kutoka msondo kuja kuziba pengo la Fresh Jumbe.
Kuna habari zinasema SIkinde kabla ya kuchukuliwa na DDC ilikuwa inamilikiwa na na UwT na ndio maana Volvo nyingi zilikuwa zinajaa pale DDC Mlimani Park. Inaaminika kuwa 'tyuni' ya sikinde haijawahi kubadilika kwa sababu ya kuwepo mwanamuziki marehemu Michael Enock ambaye ndiye alikuwa 'afisa ufundi' mkuu wa kuchanganya sauti. Watanzania hatuna tabia ya kuwaenzi wanamuziki wetu lakini miongoni mwa majina hayatasahaulika ni jina la TX Moshi William au Shaban Muhoja. Huyu jamaa atabakia kuwa ni mwanamuziki wa kihistoria ukiondoa akina Mbaraka labda na Maneti.