Tulichomfanya Yule Mchawi hatokuja kusahau kamwe! - 16.
Wakati tunaondoka Monica alikuwa amechukia sana na haikuwa kawaida yake,niliwaza sana itakuwaje maana niliona Ema ameondoka kwa hasira kuelekea nyumbani baada ya mimi kufika pale!.Basi nilikuwa mpole huku binti wa watu akiniongoza kuelekea nisikokufahamu.
Mimi "Tunaelekea wapi?"
Monica "Wewe twende acha hayo maswali yako".
Mimi "Lakini si tunawahi kurudi?"
Baada ya kuona maswali yamekuwa mengi,Monica alisimama akawa ananisukuma sukuma kwa mkono akiniambia "Hivi lini utafunguka hayo macho yako?,hivi wewe unajiona upo kawaida?"
Monica "Huku nimekuja kwa ajili yako,kama unataka hurudi kwenu wewe rudi lakini kitakachokukuta utajua mwenyewe!"
Mimi "kwani kuna nini Moni?"
Monica "Yaani unataka kuwa tahira kama huyo ndugu yako"
Aliendelea "Nishakwambia kila kitu tangu jana kwamba nitakulinda usiku na mchana lakini unajitoa ufahamu!"
Monica "Kama unanipenda na unaniamini twende,lakini kama huniamini rudi kwenu,njia hiyooo nyeupe".
Monica alikuwa mkali sana baada ya kuona kama namchosha kwa maswali ambayo yeye aliamini kabisa majibu yake uenda nikawa nayafahamu,sikuwa na namna ikabidi nijifanye kondoo niongozane nae kusikofahamika.
Mimi "Mbona jamaa alikuwa amekasirika?"
Monica "Achana nae mjinga yule,itakula kwake"
Monica "Mimi leo nimemueleza ukweli kwamba wewe ni mpenzi wangu"
Mimi " Siulisema lakini iwe siri Moni?"
Monica "Nimefika pale kwa mambo mengine kabisa,sasa yeye akaanza kuleta mambo yake ya niache kumsumbua,mimi nikamwambia sijaja hapa kwa sababu hiyo,kilichonileta sicho unachofikiria,na kama ni mapenzi kwasasa mpenzi wangu ni umughaka siyo wewe"
Aliendelea "Basi ndiyo kama ulivyotukuta,alipokuona akasema niongee na wewe na kwa hasira akaondoka,sasa mimi ulitaka nifanyeje?".
Mimi "Ninavyo mjua yule,hatutaongea mwaka mzima".
Monica "Nimekwambia achana nae,utakipata".
Basi tulitembea kwa muda mrefu kidogo huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale,yule binti Monica kiukweli mpaka wakati huo nilikuwa nampenda sana toka ndani ya moyo wangu!,na alikuwaga jasiri sana asiyeogopa chochote!.Sasa kwakuwa alikuwa amenihakikishia ulinzi kama mpenzi wake,sikuwa na hofu kama angeweza kunifanyia jambo lolote!.
Baada ya safari ya dakika kadhaa,tuliiacha njia na kuingia kwenye shamba moja kubwa la mihogo,tulitembea mle kwenye lile shamba kwa takribani dakika 2 tukawa tumefika kwenye mji mmoja ambao ulikuwa umezungukwa na mashamba ya mihogo,sasa baada ya kufika pale ghafla nikawaona wanawake watatu ambao kwa haraka haraka sikuweza kuwatambua kwakuwa walikuwa kwa mbali kidogo!.Monica aliniambia nisubiri hapo pembeni na yeye akawa amewafuata wale kinamama na kuanza kuzungumza nao kisukuma.
Sasa ghafla nikaona wale kina mama wananikimbilia na walipofika wakawa wamenishika kwa kunitaka nifanye haraka nisogee walipokuwepo wao.Basi wakamwambia Monica kwa kisukuma kwamba aingie ndani na alete jamvi ili nikalie.Sasa wale kina mama nikawa nimewatambua baada ya kuwa nimewaona kwa karibu,mmoja alikuwa mama yake Monica,na wale wawili walikuwa wale kina mama ambao nilionana nao njiani wakati natoka kuchukua miwa kwa mzee masumbuko ile Asubuhi,kumbuka hao wote akiwamo na mama yake Monica walikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wakicheza ngoma ule usiku pale kwao Monica.
Sikuelewa kwa nini Monica alinipeleka pale na sikufahamu ni kitu gani kilikuwa kikiendelea!.Baada ya lile jamvi kuletwa na kuwekwa chini,mama yake Monica akaniambia nisimame na nivue nguo zangu zote nibaki kama nilivyozaliwa!.Basi ikabidi nifanye kama alivyoniambia.
Sasa baada ya kumaliza kuvua nguo,akaniambia nikae pale katikati ya jamvi;Mama mmoja kati ya wale niliokutana nao ile asubuhi nikaona anachukua maji kwenye chungu akawa anakunywa kwa kupiga fundo kisha ananitemea,alinitemea yale maji mwili mzima mpaka yalipomalizika kwenye kile chungu!.Baada ya hilo zoezi la kutemewa maji walinizunguka wote wale kina mama akiwemo mama Monica wakaanza kunipaka vitu ambavyo sikuelewa ilikuwa ni kitu gani,harufu yake haikuwa nzuri kiukweli na nilibaki kushangaa tu!.
Waliendelea kunipaka kwa haraka na walipomaliza,mama mmoja akaniambia nisimame.Sasa baada ya kusimama yule,yule yule mama ambaye ndiye alikuwa akinitemea yale maji,niliona mkononi ameshika kitu kama usinga wa mnyama na akaanza kuchovya ule usinga kwenye chungu kiingine kilichokuwa pembeni akawa kama ananichapa na ule usinga uliojaa yale maji aliyokuwa akichovya kwenye kile chungu.
Wakati anaendelea kunitandika na ule usinga alikuwa akinuia kwa kisukuma.
Sasa baada ya lile zoezi la kuchapwa na usinga,mama yake Monica alimwambia binti yake aingie ndani awashe kibatari alete,baada ya kuletwa kile kibatari kukawa angalau na mwanga pale nje,sasa mama yake Monica akanisogeza kwa pembeni kulipokuwa na jiwe lilikuwa lichongwa kama kigoda akaniambia nikae.(Lile jiwe nadhani ni yale mawe ambayo huwa wanasagia nafaka kama mtama,udaga, na ulezi,lilikuwa ni jiwe fulani ambalo lilikuwa limekaa kama bakuri).
Basi baada ya kukaa hapo akaanza kunichanja kwa kisu kilichokuwa kikali mithili ya wembe,amenipiga chale za kutosha karibia mwili mzima.Baada ya kumaliza lile zoezi nikatakiwa nikae kwanza uchi ili niendelee kukauka kisha ndipo nikatakiwa kuvaa nguo.Sasa baada ya kuwa nimemaliza kuvaa nguo ndipo mama yake na Monica na wale kina mama wakaanza kuzungumza na mimi,kile kitendo kilikuwa ni kitendo cha haraka sana ambacho hakikuchukua hata saa nzima!.
Mama Monica "Mkwe wangu hujambo mwanangu"
Mimi "Sijambo mama,shikamoo"
Mama Monica "Maraba mwanangu"
Mama Monica "Baba huu ulimwengu una watu wabaya sana,lazima tukulinde mwanangu".
Basi mimi nikawa nimetulia tu sikusema jambo lolote,mama yake Monica akaanza kuongea na mwanaye kisukuma na nadhani alimwambia aniambie kilichokuwa kinaendelea!.
Monica "Umughaka dhumuni la mimi kukuleta huku kama nilivyokwambia ni kukulinda mpenzi wangu,sitaki baya lolote likukute kwasababu nakupenda na wewe ndiye mama yangu anataka unioe!"
Aliendelea "Unakumbuka kile kishindo cha jana kilichofanya mpaka ukakimbia?"
Mimi "Ndiyo,nakumbuka!"
Monica "Basi yule mtu alikuwa ametumwa na baba yake ili waje kukuchukua,ndipo nikamuwahi kupambana nae kabla hajaleta madhara,sasa aliponizidi nguvu nilimuita mama yangu akaja kunisaidia na akawa ameondoka naye"
Aliendelea "Sasa lile jambo limeleta shida kwa huyo mshirika mwenzao na mama na kuna vita inaendelea"
Kiukweli nilikuwa nimekodoa macho huku nikiendelea kusikiliza kinaga ubaga ile stori ya Monica ambayo nilikuwa hata siifahamu.
Monica "Kuna mzee mmoja ambaye naye jana alikuwa akicheza ngoma na hutoweza kumfahamu,sasa yule mzee kumbe wakati wakiwa kule miembeni alimuagiza mwanaye aje akuchukue akupeleke kwake wakakufanyie michezo yao".
Aliendelea kusema "Sasa baada ya yule mzee kuona mwanaye amedhibitiwa alikasirika sana na mama anasema walikaa kikao wakamtaka atoe sadaka kwa kufanya lile jambo kwa mshirika mwenzie".
Monica "Sasa yule mzee alisema kwa wenzie kwamba anataka aisambaratishe nyumba ya mwalimu na lazima awapeleke mbele ya kamati iliyomuagiza sadaka nyinyi nyoote ingawaje alitumwa mtu mmoja tu kama fidia"
Sasa baada ya kusema yale maneno nilishituka sana na ndipo akili yangu ikafunguka kwa haraka sana!,kwa haraka nikamuwaza uenda atakuwa ni mzee makono kwasababu ndiye niliyekutana naye akawa amenipa vitisho vingi kuhusu tulichomfanyia mwanaye!,pia nikajua uenda atakuwa ndiye maana usiku nae alikuwa miongoni mwa wacheza ngoma pale kwao Monica!.
Mimi "Kuna mzee mmoja anaitwa Makono,je mama mnamfahamu?"
Baada ya kuuliza vile lile swali wakashituka sana na mama yake Monica akaniambia "Unamjua mzee Makono?"
Mimi "Ndiyo mama"
Mama yake Monica "Ndiyo huyo huyo anataka kukutoa sadaka mwanangu,sitakubali!"
Basi wakaanza kuzungumza kwa kisukuma huku wakionekana kusikitika!.
Mimi "wakati natoka senta nimekutana naye jioni akanitisha sana kuhusu mwanae"
Mama Monica "Ndiyo maana tumekuleta hapa maanangu tukutengeneze vizuri,huyo makono ni mtoto mdogo sana kwetu,nitamshughulikia".
Basi kwakuwa hali haikuwa nzuri siku hiyo kutokana na Makono na genge lake kupanga kwenda kufanya uhalifu wa kichawi pale nyumbani,mama yake Monica na wale kina mama wakaniambia leo sipaswi kabisa kukanyaga pale nyumbani na nitalala hapo kwa hao kina mama mpaka asubuhi!.
Mimi "Je sitaonekana"
Mama Monica "Baba hapa ni kiboko,hakuna wa kukanyaga hapa"
Aliendelea "Tumekupika na hakuna wa kukusogelea na hata wakija hakuna wa kukuona,ondoa shaka mwanangu"
Mama Monica "Huyu huyu makono tuliyemfundisha kazi anataka kuniulia mwanangu na mkwe wangu?,atanijua mimi ni nani,nitamuaibisha mpaka atajuta"