Tulichomfanya Yule Mchawi hatokuja kusahau kamwe - 3
Baada ya kuambiwa yale maneno na yule jamaa kiukweli ilibidi niwe na tahadhari ingawa mpaka wakati huo sikutaka kabisa kuamini mambo ya kishirikina.
Sasa nakumbuka Jumamosi moja kama kawaida niliamka na shughuli za hapo nyumbani zilichukua nafasi ikiwemo kwenda lamboni kuchota maji na kuleta hapo nyumbani.
Headmaster ambaye alikuwa ba'mdogo wangu yeye ijumaa tu alikuwa ameshaondoka kuelekea mjini kuiona familia yake, kama nilivyowaambia ya kwamba, kila ilipofika Ijumaa ya kila wiki alikuwa akiondoka na kurejea jumapili jioni kwa ajili ya mambo ya shule!
Sasa siku hiyo kulikuwa kuna mechi kati ya Arsenal na Blackburn ambayo ilikuwa inachezwa saa 12 jioni, lakini pia kulikuwa na mechi nyingine!,kama kawaida ilipofika saa 11 jioni nilimwambia jamaa tuondoke tukacheki gemu akagoma akadai ataenda kusoma baadae kwao na demu wake! Basi nikachukua zangu tochi au taa ya sola kwa ajili ya kumulika njiani pindi nitakaporudi maana ingekuwa usiku.
Kipindi kile kulikuwa na vile vitaa vya sola ambavyo ulikuwa unaviweka juani vinapata chaji halafu usiku vinamulika kama taa ya umeme, vilikuwa na mwanga sana!,sasa hapo nyumbani vilikuwepo 2,moja alikuwa anaitumia Headmaster chumbani kwake na nyingine alikuwa anaitumia jamaa kule kwenye chumba alichokuwa akilala.
Ile nyumba ilikuwa na chumba na sebule pamoja na stoo,lakini kwa nje pia kulikuwa na chumba kimoja ambacho pembeni yake kulikuwa na jiko ambalo humo humo ilikuwa stoo. Kulikuwa na milango miwili mikubwa, mmoja ulikuwa wa mbele ambao mara zote ulikuwa ukifungwa lakini pia kulikuwa na mlango wa nje ambao ulikuwa umeshikamanishwa na ukuta wa fensi,huu mlango ndiyo ulitumika mara zote kutoka na kuingia!
Sasa wakati naondoka nilimwambia jamaa anipe kile kitaa chake niende nacho halafu yeye angetumia kile cha Headmaster.
Niliondoka zangu kuelekea kucheki boli kama kawaida,ijapokuwa jamaa alinionya kuhusu ile njia sikutaka kabisa kuacha kwasababu ilikuwa fupi kuliko ile aliyokuwa amenielekeza ya kupitia lamboni ambayo ilikuwa ya mzunguko!.Wakati huo mvua ilikuwa imemaliza kunyesha kama siku mbili zilizopita,hivyo bado ardhi ilikuwa na unyevunyevu wa kutosha!
Nilifanikiwa kufika lakini nilikuta tayari mechi imekwisha kuanza. Sasa baada ya kutazama mechi ya Arsenal ambayo tulishinda 2-0,nilitazama na mechi nyingine. Mpaka namaliza kutazama mechi ilikuwa yapata saa 3 usiku,nikaamua sasa ni wakati wa kurudi nyumbani.
Kabla sijaondoka niliwaza nipite njia ipi kati ya zile mbili,lakini nilifikiria ile njia ya lamboni ilivyo ya mzunguko ingenichukua muda mrefu kufika,nikaona nirudi na ileile niliyoizoea,nikajifariji kwa kuwa nilikuwa na taa ya sola hivyo kisingeharibika kitu!
Basi bana nikaanza mdogo mdogo kupiga kwato huku nikimulika mulika kwa madaha njia nzima,nina tochi tena!,utaniambia nini!.Sasa kadri nilivyokuwa nikisogea ndivyo utulivu na ukimya ulivyo tawala,kama kawaida nikawa nimeikaribia ile miembe miwili ambayo kila nikifika hapo moyo wangu unashituka sana,sasa safari hii sikuona moto wala nini, nikasonga kuikaribia ile miembe,sasa nilipofika katikati ya ile miembe mikubwa nikahisi kuna mtu nyuma yangu na nikageuka ghafla lakini sikuona mtu, nikahisi yalikuwa mawenge tu ya kitete,kiukweli nilikuwa nasisimkwa na nywele sana kila nikifika hilo eneo!.
Sasa ili kujiamini na kutoa uoga,niliamua kunyanyua kile kitaa na kuanza kumulika juu ya ile miembe angalau nione kuna nini ili nipite kwa amanj, nilipomulika sikuona chochote, sasa ile nashusha tochi chini ghafla nikajikuta nimejikwaa kwenye kitu ambacho sikukiona hapo awali, kiukweli nilianguka pale chini na ile taa ikawa imeanguka kwa mbele na kuzimika, ndala moja pia ikawa imechomoka mguuni nikawa nimebakiwa na moja, sasa nikawa najiuliza nini kile ambacho kimefanya nimejikwaa mpaka nimeanguka, niliamka kwenda kuchukua kile kitochi nikawa nakiwasha nimulike kutafuta ndala yangu ili nivae niondoke lakini kinagoma kuwaka,sasa ikabidi nianze kukipiga piga nikadhani uenda kilipata hitilafu!
Nimekipiga piga sana hatimaye kikawa kinawaka na kuzima, kinakaa muda kinawaka halafu kinazima, nikaendelea kukipiga tena sasa kikawaka kama ilivyokuwa mwanzo, ikabidi nianze kumulika kuitafuta ndala yangu itakuwa imehangukia wapi!,sasa ile namulika kwa nyuma nikaona mtu amelala akiwa uchi wa mnyama!,daaah nikashituka sana na nikataka kukimbia lakini nikajikaza na kuanza kuita kwa nguvu "wewe ni nani?" Niliita sana lakini mtu yule alikuwa hasemi wala hatikisiki,nikagundua uenda ndiye aliyefanya nikadondoka ingawa wakati najikwaa nilihisi kitu kama jiwe na maeneo yale hakukuwa na mawe!.
Sasa akili yangu ikadhani uenda yule mtu alikuwa mlevi ambaye alikuwa amekunywa pombe zikamzidi akawa amelala pale chini,nilisahau kutafuta ile ndala akili yangu ikaamia kwa yule jamaa,nilimsogelea na kuanza kumtikisa kwa mguu huku nikisema " wewe....wewe....wewe" lakini hakuamka,nilipomulika vizuri nikagundua ile ilikuwa maiti na hakuwa mlevi kama nilivyodhani.
Hakuna siku ambayo sitakuja kuisahau kama ile siku na ndipo nikaamini kuna wachawi!,sikumbuki nilifikaje nyumbani mpaka wakati huo maana nilipopata kumbukumbu nilijikuta nipo kwenye mlango wa nyumbani nikiwa ninahema balaa! Kibaya zaidi pale nyumbani nilikuta jamaa hayupo na mlango wa kuingia ndani ukiwa umefungwa kwa nje na kofuli,niliamua kukaa chini kwanza ili kutuliza presha nikawa najiuliza kile nilichokiona kilikuwa kweli au uenda nilikuwa naota? Baada ya kutulia kwa dakika kadhaa, kujiangalia chini nilikuwa peku na kile kitochi nacho sina mkononi!.
Sasa nikawa nimekaa pale nje kwa uoga mwingi,kwakuwa jamaa aliniambia angeenda kwao demu wake kusoma nikaondoka kuelekea kwao yule demu wake ili nikachukue funguo nirudi kulala,wakati naenda nilipitia njia ya lamboni lakini sikutaka kabisa kutembea ilibidi nikimbie maana ilikuwa usiku wa saa 4 kuitafuta saa 5, kiukweli nilikuwa nikifika kwenye vichaka nilikuwa napita kwa spidi kali mno kama ngiri!
Nilipofika kwa na yule demu wake jamaa nikaona mbwa wanaanza kubweka kwa sana!,sasa ile boma yao ilikuwa imezungukwa na miti na katikati kulikuwa na zizi kubwa la ng'ombe,nyumba aliyokuwa akilala yule binti na mdogo wake ilikuwa kwa pembeni ambako ilinibidi kufanya kazi ya kuzunguka ili kuwakwepa wale mbwa!
Nilipofika kwa nyuma nilichungulia kwenye upenyo wa kidirisha nikaona kuna mwanga,basi angalau moyo wangu ukatulia nikajua walikuwa wakijisomea.Nilianza kugonga nikimuita jamaa ili asikie aje anipe funguo za nyumba,sasa wakati nagonga na kumuita jamaa yule demu wake aliuliza "we nani?"
Mimi " Mimi Umughaka"
Demu " oooh,ngoja nije"
Basi yule demu akafungua nyumba akaniambia "Zunguka huku mbele".
Kwakuwa alikuwa ametoka nje,sikuwa tena na mashaka kuhusu wale mbwa.
Mimi " Mambo Debo"
Deborah "Poa umughaka"
Deborah "vipi mbona usiku?"
Mimi " Mwambie ema aniletee funguo"
Deborah "Kwani hayupo nyumbani?,na wewe kwani ulikuwa wapi?"
Mimi " Mimi natoka senta kuangalia mpira,wakati naondoka aliniambia angekuja huku kwa ajili ya kujisomea"
Baada ya yale maelezo yule demu akaniambia wala huyo jamaa aliyeitwa emmanuel hakwenda kwake,sasa akaniambia huenda alienda kwa rafiki yake mmoja alikuwa akiitwa maganga.
Mimi "Duuu sijui nitafanyaje na mlango amefunga"
Deborah " Kwani kwao maganga hupafahamu?"
Mimi " mimi napajua hapa kwenu tu Debo,kwao marafiki zake sipajui!"
Debo "Nisubiri nivae nije nikupeleke".
Mimi "Kama ni mbali tusiende ni bora nikarudi ili nisije kupishana nae njiani"
Debo " Yule mimi naijua akili yake,unadhani anarudi muda huu,utakaa nje mpaka uchoke,wewe subiri nije nikupeleke"
Basi baada ya Deborah baada ya kujiandaa alitoka ndani na taa ya chemri tukandoka kuelekea kwa huyo Maganga ambaye ni rafiki yake na jamaa ambapo Deborah aliyekuwa demu wa jamaa alidhani uenda angekuwa hapo!
Tulipofika hapo kwao Maganga tulianza kumgongea,cha ajabu jamaa akatoka akionyesha kabisa alikuwa amelala!.
Maganga " Mambo vipi"
Deborah " Poa,Ema yuko wapi?"
Maganga "Alipita hapa mida fulani akaniambia anaenda kupiga buku kwao Jackson"
Deborah "Jackson yupi?"
Maganga "Jackson Mashida"
Maganga "Kwani kuna nini?"
Deborah "Aah ameondoka na funguo za nyumba,sasa ndugu yake alikuwa anazihitaji!"
Maganga " Nendeni kwao Jack mtamkuta"
Basi tuliondoka tena nikifuatana na binti Jasiri Deborah,ingawa ilikuwa saa 5 ya usiku lakini Deborah hakuonyesha kabisa kujali hilo,nadhani kwakuwa wao walikuwa wamezaliwa vijijini na kukulia huko haikuwa taabu kwao!.
Haikupita muda tukawa tumefika kwa huyo dogo tuliyeelekezwa kwao.
Tulipofika Deborah aligonga mlango na hatimaye mlango ulifunguliwa!.
Jamaa "Oooh Debo mambo"
Debo "Poa,vipi"
Debo " Ema yuko wapi?"
Jamaa akaanza kuita "Oyaa ema,njoo unaitwa huku"
Sasa kile kinyumba kilikuwa na chumba na sebule halafu juu kimeezekwa kwa nyasi,mimi wakati huo nilikuwa nimesimama kwa mbali kidogo,Deborah yeye alikuwa pale mlangoni.
Jamaa haikuchukua muda akawa ametoka nje.
Aliponiona akaanza kusema " Aaah kaka,nilijisahau nikaondoka na funguo,ila ningewahi kurudi"
Sasa anasema angewahi kurudi wakati muda huo ni saa 5 ya usiku!,nilimtazama kwa jazba lakini ilibidi nikaushe,sikutaka kunyesha kuchukizwa!
Sasa kumbe wakati ameenda kuchukua funguo ndani si ikasikika sauti ya binti,nadhani kuna kitu alikuwa akimuiliza na jamaa akimjibu.
Kumbe wakati huyo Jackson yeye akipiga buku hapo sebuleni,ema yeye alikuwa akivinjari na kibinti fulani kule chumbani!.
Aliponiletea funguo ndipo Deborah akaanza kumuuliza " Ema huyo ni nani?"
Jamaa akawa anajifanya kama hajasikia "Unasema?"
Baada ya kukabidhiwa funguo nilikuwa namsubiria Debo tuondoke lakini binti wa watu akaanza kuwaka,akaiweka ile taa chini akasukuma mlango akazama mpaka ndani!,baada ya muda akatoka amemkwida binti fulani ambaye alikuwa yupo na chupi tu!,ngumi na makonde ya kike yakaanza kurindima hapo na matusi juu!.
Sehemu ya Nne