DOKEZO Tulioajiriwa kati ya mwaka 2013 na 2016 tuliambiwa tusubiri miaka mitano kabla ya kupandishwa vyeo

DOKEZO Tulioajiriwa kati ya mwaka 2013 na 2016 tuliambiwa tusubiri miaka mitano kabla ya kupandishwa vyeo

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'
A

Anonymous

Guest
Sisi ni miongoni mwa watumishi walioajiriwa kati ya mwaka 2013 na 2016, ambao ni miongoni mwa waajiriwa wa mwanzo kupitia mfumo wa Wakala wa Ajira Serikalini (Ajira Portal). Hata hivyo, kundi hili limekuwa likikumbwa na changamoto za kutopandishwa vyeo kwa wakati, licha ya kutumikia Serikali kwa miaka mingi. Isipokuwa taasisi chache, watumishi wengi wa kundi hili wameendelea kunyimwa haki zao za kupanda vyeo.

Kila tunapofuatilia suala hili, tunapewa majibu kwamba tulikuwa miongoni mwa walioathiriwa na zuio la kupandisha vyeo lililowekwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano. Kwa lugha rahisi, ni kana kwamba vyeo vyetu vilipotea na hakuna anayewajibika kuvirejesha.

Kwa utaratibu wa kawaida, watumishi wa umma wanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya kupandishwa vyeo baada ya kila miaka mitatu ya utumishi, huku kwa waajiriwa wapya kipindi hicho kikihusisha muda wa majaribio (probation).

Hata hivyo, sisi tulioajiriwa kati ya mwaka 2013 na 2016 tuliambiwa tusubiri miaka mitano kabla ya kupandishwa vyeo, wakati walioajiriwa baada yetu walirejea kwenye utaratibu wa miaka mitatu. Hali hii imezua maswali kuhusu usawa na haki katika usimamizi wa watumishi wa umma.

Baadhi ya taasisi, kupitia usimamizi mzuri wa rasilimali watu, zilijitahidi kuwafidia watumishi hao baada ya Serikali kufungua dirisha la kupandishwa vyeo na marekebisho ya madaraja mwaka 2021. Hata hivyo, zipo taasisi ambazo hazijachukua hatua za kurekebisha hali hiyo, huku mamlaka zinazohusika na usimamizi wa utumishi wa umma zikionekana kutolipa uzito unaostahili suala hili.

Kwa sasa, changamoto nyingine imejitokeza kupitia mfumo wa PEPMIS, ulioanzishwa Julai 2023 kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa watumishi. Tuna wasiwasi kuwa mfumo huu unatumika kama kigezo cha kuwanyima baadhi ya watumishi haki na stahiki zao, ikiwemo kupandishwa vyeo, bila kuzingatia mazingira na changamoto zilizokuwepo katika kipindi cha nyuma.

Jambo lingine linalokatisha tamaa ni kwa watumishi wanaoamua kujiendeleza kielimu. Kwa mfano, mtumishi wa kada ya afya anapoenda kusomea ubobezi wa juu zaidi wa kitaalamu (super-specialization) na kurejea kazini, mara nyingi anakuta suala la kupandishwa cheo halijazingatiwa ipasavyo. Hali hii inavunja moyo na kuwakatisha tamaa watumishi wanaotaka kujiendeleza kielimu, hasa wale wanaohitaji kwenda kusoma masomo ya muda wote (full-time).

Kinachoshangaza zaidi ni kuona watumishi walioajiriwa miaka ya baadaye wakiendelea kupandishwa vyeo na hata kuwazidi madaraja wale walioajiriwa kati ya mwaka 2013 na 2016.

Ombi letu kwa Serikali na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa utumishi wa umma ni kupitia upya suala hili, kuchunguza ucheleweshaji wa kupandishwa vyeo kwa kundi hili na kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa. Hatupaswi kuendelea kuadhibiwa kikazi kwa changamoto za kiutawala zilizotokea miaka iliyopita. Tunahitaji majibu ya wazi, hatua za kurekebisha hali hii na utaratibu wa kuhakikisha hakuna mtumishi anayenyimwa haki zake kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake.
 
Back
Top Bottom