KERO Tuliorejesha vitambulisho vya NIDA vilivyofutika tunapigwa 'danadana' kupatiwa vingine

KERO Tuliorejesha vitambulisho vya NIDA vilivyofutika tunapigwa 'danadana' kupatiwa vingine

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua

Kayugumis

Senior Member
Joined
Jun 6, 2022
Posts
160
Reaction score
172
Baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wananchi wengi kudai kuwa vitambulisho vyao vya NIDA vimefutika, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ilijitokeza kujibu kuwa changamoto hiyo imetokana na uzembe wa mzabuni aliyekuwa na tenda ya uchapishaji, aliyesababisha uzalishaji wa vitambulisho vyenye changamoto za ubora.

NIDA iliwataka wananchi waliokumbana na changamoto hiyo kuwasilisha vitambulisho vyao katika ofisi za mamlaka hiyo, hususan katika ofisi walizojisajilia, ili wapatiwe vitambulisho vipya. Kupitia kurasa zao rasmi, NIDA imekuwa ikieleza kuwa mchakato huo unakamilika ndani ya wiki tatu, ambapo mhusika hupatiwa kitambulisho chake.

Hata hivyo, nasikitika kusema kuwa kwangu mimi suala hilo halina uhalisia, kwani ni zaidi ya miezi mitano tangu nirejeshe kitambulisho changu katika ofisi ya NIDA Luguruni, Ubungo, lakini sijawahi kupatiwa kitambulisho changu kipya. Kila ninapofuatilia, napewa majibu yasiyoeleweka, kwamba nivute subira kwa kuwa mkandarasi yupo kazini.

Hali hiyo pia inamkumba rafiki yangu, ambaye alirejesha kitambulisho chake katika ofisi ya NIDA Gongolamboto, Ilala. Majibu anayopata kutoka kwa maafisa ni sawa na ninayopata mimi, huku yeye akiwa amefuatilia suala hilo kwa takribani miezi mitatu bila mafanikio.

Naomba kutoa wito kwa mamlaka husika kuacha danadana hizi na watoe vitambulisho kwa wakati kama wanavyoeleza katika taarifa zao rasmi, badala ya kutoa ahadi zisizo na utekelezaji. Ni vyema watambue kuwa katika mazingira ya sasa, kitambulisho cha NIDA ni nyaraka muhimu sana na ni lazima mwananchi awe nacho karibu wakati wote.
photo_2026-01-29_14-35-47.jpg
 
Back
Top Bottom