Mwaka 2015 nikiwa wilayani BUNDA,mkoa wa MARA, kuna jamaa mmoja tulikuwa tunafahamiana nae sana alikuja kutuambia kuna Tsh 100 ya mwaka 1993 zinahitajika na wazungu fulani,hizo Tsh 100 za mwaka huo kwa ambao wanazifahamu ni kwamba zilikuwa na madini fulani ambapo endapo ungeumwa na nyoka,nge,tandu au wadudu wowote wenye sumu kali,basi ulikuwa ukichanja maeneo ya jeraha na ukiiweka hiyo hela basi inanatia kama sumaku na kunyonya sumu yote,wahenga bila shaka wanazifahamu(Kwa kule kwetu tuliziita BODO).Bila shaka yeyote ikabidi tuunganishwe na huyo mzungu kwa wakati huo alikuwa jijini Mwanza,Tanzania,na tuliongea nae sana japo niliongea kiingereza cha elimu ya form 4 alinielewa nami nilimwelewa na alinihakikishia ni kweli kabisa zinahitajika na endapo nitaipata basi yupo tayari kutupatia milioni 100 za kitanzania!,kiukweli ukiwa umekaa kijijini na umepigika kweli kweli unaweza ikawa kama umeamshiwa mashetani vile!,basi tulikaa chini mimi na ndugu yangu na tulihisi ni utapeli,ilibidi twende kwa jamaa mmoja ambaye tulimfahamu na tulimweleza namna mchongo ulivyo,jamaa alituambia hiyo issue ni kweli kabisa kwa maana kuna kipindi fulani zilihitajika Tsh 20 za mwaka fulani(sikumbuki mwaka) na yupo jamaa mmoja yeye aliipata na akaipeleka na akapewa milioni 10 ya wakati huo ( mwaka 2003),sasa ilibidi mimi na ndugu yangu tuelekezwe kwa huyo jamaa ambaye alipewa hela baada ya kupeleka hiyo sh 20.
Tulifika na tukamkuta na tulimweleza na akatuambia hiyo issue ni kweli kwa maana yeye pia liliwahi kumkita hilo zali na akapewa hiyo milioni 10,na akatuambia hata nyumba tuliyofikia aliijenga kwa hiyo hela milioni 10(kumbuka hapa tulikuja kupata confirmation),jamaa alituambia pambaneni japokuwa ni kazi sana kuipata kwa maana hampo peke yenu wapo na watu wengine, "mi ningwasaidia wadogo zangu kutafuta but for now nina kazi zangu na biashara zangu hivyo mambo hayo nimesha achana nayo kitambo" alisema jamaa.
Ilibidi tuanze kuzunguka kutafuta hiyo 100,tulizunguka maduka yote ya pale Bunda mjini bila mafanikio.
Kuna mama mmoja alituambia mara nyingi hizo hela za zamani zinapatikana kwa waganga,alikuwa akielewana na mganga mmoja yupo huko majita,wilaya ya musoma vijijini alituambia twende anaweza kuwa nayo kwa maana anazo pesa nyingi sana za zamani,ilibdi tulale mapema ili kesho yake tuanze safari mapema.
Tulidamka asubuhi ya saa kumi alfajiri tukaanza kutembea ,tulitembea kwa mguu kwa maana hatukuwa na nauli ya kutufikisha tunapokwenda,mimi nilivaa kanda mbili zangu zilizokuwa zimechoka japo si sana na ndugu yangu yeye alivaa kata mbuga zake alizokuwa akiaminia.
Kumbuka ni safari ya kutoka wilaya ya BUNDA kwenda MAJITA wilaya ya musoma vijijini,umbali bila shaka ni zaidi ya kilometa 95 mpaka ufike huko chaka.
Safari ikaanza na ilipofika saa sita mchana tukawa kama tumefika nusu ya safari ilibidi twende kwenye mji mmoja huko huko njiani kuomba chakula,tulipokewa kikarimu sana na tulisongewa ugali wa muhogo na kisamvu,kiukweli tulikula sana ukizingatia tulikuwa na njaa ya kufa mtu,tulimaliza kula na tukaaga na tukaanza safari,tulifika huko porini saa 4 usiku na kiukweli mi nilikuwa nimechoka sana mithiri ya kufa!,tulilala nje kwa maana hakukuwa na nyumba kubwa,kwa waganga mara nyingi kuna kuwa na tuvijumba tudogo tudogo na vyote vilikuwa na wateja wake,hivyo tulikoka moto tukalala nje!!
Jamani story ni ndefu but nacho taka kusema ni kwamba,SITASAHAU HIYO SAFARI YA UMBALI MREFU,KISA TU MAISHA MAZURI.