ippmedia.com/sw/makala/mamlaka-ya-ukamataji
April 17, 2018
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA YA UKAMATAJI
KWA mujibu wa Sheria Namba 9 ya Mwaka 1985 ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyofanyiwa masahihisho mwaka 2002,...
Ukamataji ni kitendo cha kumzuia mtu au kumnyima mtu uhuru wake wa kwenda anakotaka, ili afikishwe Kituo cha Polisi kwa ajili ya upelelezi na hatimaye afikishwe mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Mtu atahesabika kuwa amezuiliwa ikiwa atakuwa mikononi mwa Afisa wa Polisi, kwa madhumuni yanayohusiana na upelelezi wa Kosa la Jinai na atakuwa chini ya ulinzi kutokana na kosa analotuhumiwa kutenda au kulifanya.
Pia, mtu atahesabiwa kuwa amezuiliwa kihalali au kisheria, iwapo atakuwa ameongozana na afisa wa Polisi au atakuwa na afisa wa Polisi anayesafiri naye katika gari kwa madhumuni ya upelelezi.
Wanajamii wanapaswa kutambua kuwa kuna mamlaka ya kukamata bila hati aliyonayo Polisi, Hakimu na Raia.
Wote hawa wana mamlaka ya kumkamata muhalifu pindi anapofanya au anapotenda kosa mbele yake.
Ifahamike kuwa kila raia pia ana uwezo wa kukamata kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha sheria ya mwenendo ya makosa ya jinai.
Kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepewa uwezo wa kumkamata mtu yeyote ambaye atatenda kosa mbele yake na endapo wakati huo kutakuwa hakuna askari katika eneo hilo.
Pia kifungu cha 31 cha Sheria hii kinaelekeza kwamba; raia yoyote mara baada ya kumkamata mtuhumiwa atamkabidhi kwa Afisa wa Polisi au atamkabidhi kwenye Kituo cha Polisi kilicho karibu naye.
Kama hakuna Kituo cha Polisi kilicho karibu; atamkabidhi mtuhumiwa kwa walinzi wa amani walio karibu yaani Mahakama au Hakimu, Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji au Mtaa au hata kwa Mwenyekiti wa Mtaa au Kitongoji.
Uhuru huu unaotolewa kwa mujibu wa sheria kwa raia, haupaswi kutumiwa vibaya kwa kujichukulia sheria mkononi au kuchukua nafasi ya mahakama na kutoa hukumu dhidi ya mtuhumiwa kwa kumpiga, kumjeruhi au kumuua. Sheria hii haimruhusu raia yeyote kujichukulia sheria mkononi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa amesema “
inashangaza sana pale raia anapopewa mamlaka ya kumkamata muhalifu pindi anapotenda kosa mbele yake na raia huyo kuamua kujichukulia sheria mkononi kwa kuanza kumpiga, kumdhuru na wakati mwingine kumuua mhalifu jambo ambalo ni kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Ukamataji. Ni marufuku raia yeyote kujichukulia sheria mkononi kwani kwa kufanya hivyo kutapelekea kujikuta upo mikononi mwa dola.”
Afisa wa Polisi amepewa uwezo wa kukamata bila hati ya kukamatia chini ya kifungu cha 14 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Afisa wa Polisi anao uwezo wa kumkamata mtu endapo mtu yeyote anatenda kosa au kusababisha uvunjifu wa amani mbele yake.
Pia anaweza kumkamata mtu endapo, mtu huyo anajaribu kutoroka kutoka katika ulinzi halali mbele ya Afisa wa Polisi na mtu yeyote ambaye atamzuia Afisa wa Polisi kufanya kazi yake.
Mtu yeyote atakayekutwa katika mazingira yanayoashiria wazi uvunjifu wa amani au katika dhamira ya kutenda kosa au anazurura barabarani kwenye viunga vya bustani za mji nyakati za usiku, mtu yeyote ambaye atakuwa na vyombo vinavyosadikiwa ni vya uvunjaji wa nyumba au atakuwa na silaha za hatari maungoni mwake pia ataweza kukamatwa na Afisa wa Polisi.
Vievile Polisi ana mamlaka ya kumkamata mtu yeyote atakayekutwa na mali au vitu vinavyodhaniwa ni vya wizi au vimepatikana kwa njia isiyo halali na kumkamata mtu yeyote ambaye anaamini kuwa hati ya kukamatwa imetolewa dhidi yake.
Mtu yeyote ambaye Afisa wa Polisi anaamini anakashifu Nembo za Taifa, Fedha au kwa namna yeyote ile inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani na mtu yeyote ambaye anaamini kwa sababu za msingi kuwa ni mzururaji, mbabaishaji na kwamba hana anuani maalum wala shughuli za kujipatia kipato halali.
Hakimu naye ana uwezo wa kukamata kwa mujibu wa Kifungu cha 17 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinatamka bayana kuwa hakimu anao uwezo wa kumkamata mtu yoyote anayetenda kosa la jinai mbele yake.
Pia, Hakimu anao uwezo wa kutoa hati ya kumkamata mtu yeyote ambaye ataamini kwa sababu za msingi kuwa ametenda kosa la jinai lakini uwezo huo wa kukamata na kutoa hati ya kumkamata mtu, unaishia kwenye mipaka ya himaya ya mahakama husika.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam.