Millionaire Mindset
Member
- Apr 19, 2018
- 83
- 115
KIGEZO #1: MAHITAJI YA NJIA YA FOLENI
Ukisikiliza swaga za watu wa njia ya foleni ni kama hizi; “Nikasomee kitu gani, kitakachonifanya nipate mshahara mkubwa?”, “Hivi ni kampuni gani nikaajiriwe, inayolipa vizuri kuliko nyingine?”, “Nikiajiriwa serikalini itakuwa poa sana, Nitakuwa na uhakika wa nafasi yangu (Job security) na mafao ya kutosha uzeeni (Pension)”.Ukiyasikiliza mawazo hayo hapo juu yote yanaanza na kiwakilishi “Nika” au “Nita”, viwakilishi hivi vinaonyesha kuwa msemaji, anajizungumzia yeye mwenyewe. Hivyo basi watu wengi wa njia ya foleni wanafanya maamuzi kwa kujiangalia wao binafsi. Hivi wewe hushangai kwa nini wengi wamejazana kwenye njia moja na kila mmoja anang`ang`ania kuwa mbele ya mwenzake(vyeo vikubwa kuwazidi wenzako) au “Corporate Ladder”, na wakati kuna njia ziko tupu kabisa au zina wadau wachache sana?
Kwenye njia ya foleni unakuwa na uhakika wa Pesa ukiishapata nafasi kwenye mfumo (system), na kushiriki kama sehemu ndogo ya gurudumu la uzalishaji(the cog in the wheel). Na kisha kuongeza nafasi yako taratibu, mwaka mmoja mpaka mwaka mwingine (kupanda cheo), wakati hou huo ukizidi kupata nyongeza ya mshahara kidogo kidogo. Lakini pia kuna ahadi ya Mafao ya uzeeni, utakayoyapata wakati ufanisi wako wa kufanya kazi umepungua kwa kiasi kikubwa, na nguvu za kufanya kazi hauna tena.
Kwenye njia hii haufikirii habari za matatizo ya jamii inayokuzunguka, au la ukijitahidi (kama umelazimika) hasa kwenye nafasi za kisiasa; unafunika kikombe kwa kufanya mambo madogo madogo yanayoonekana na kutangazwa kwenye televisheni na redio, halafu ukiisha kupigiwa kura unarudi kula bata. Suala hili ndilo lililopelekea viongozi wengi wa kisiasa kutoa suluhu ya muda mfupi ya matatizo(short term solutions), ili mradi tu, hali iwe shwari mpaka pale atakapostaafu na kuondoka kwenye nafasi yake na burungutu kubwa la pensheni.
KIGEZO #2: NAMNA YA KUINGIA KWENYE NJIA YA FOLENI
Uingiaji wa njia ya foleni una changamoto kidogo, jambo lililopelekea wenzetu wa njia ya watembea kwa mguu tuliokwisha jifunza habari zao kwenye masomo yaliyopita, kushindwa kuingia huko. Njia hii unaweza kuingia kwa kutumia chombo cha usafiri kama vile, Taaluma au ujuzi ambao umeambatana na karatasi inayoitwa “Cheti”.Kipimo cha taaluma yako au ujuzi wako ni “Cheti”, na ndiyo maana kila mtu aliyeko na anayeelekea kwenye njia hiyo anapambana kadri ya uwezo wake kuhakikisha cheti kina mabanda ya kutosha(A) au miwani kadhaa(B). Huku “FOLENI” hatuangalii uwezo wako wa kutatua matatizo yanayotuzunguka kwenye jamii, hatujali juu ya ubunifu wako, tunachotaka kwenye njia hii ni ustahimilivu wako wa kukaa jela ndogo kila siku kuanzia saa moja au saa mbili asubuhi mpaka jioni, muda wa kutoka humo.
Kwenye njia ya foleni tunahitaji watu wenye uwezo wa kuitamka kauli ya “Yes Boss!”, hata kama mara nyingine kitu tunachokwambia ufanye kiko nje ya makubaliano yetu ya awali (mkataba wa ajira), huku ukijifanya mjuaji au unauliza maswali au kudadisi dadisi mambo tunakutimua. Hata kama una kipaji cha kutatua matatizo yaliyoko kwenye mfumo wetu au gurudumu letu la uzalishaji, kiweke kipaji hicho mfukoni ukakitumie nyumbani kwako kwa mume au mke wako na watoto wako siku mbili za weekend tulizokupatia. Huku tanataka watu wenye uwezo wa kukaa kwenye reli, hata kama reli yenyewe imevurugwa.
Usiniulize vipaji vingi vya watoto wetu vinafia wapi? Nenda kakague njia ya foleni, kajionee mwenyewe. Utashangaa!. Mtu ana kipaji “X” anafanya kazi “Y” kwa sababu kazi hiyo ina mshahara mkubwa au kaambiwa na mjomba. Unafikiri masuala ya mtu kuumwa mguu, akaenda kupasuliwa kichwa yalitokea wapi? Huku “FOLENI” tunafanya kazi kwa stress kama mashine, tunakimbizana sana na kitu kinachoitwa DEAD line (Msitari wa kifo), msitari huu unahatarisha nafasi yako kwenye foleni na ndiyo maana tukiuona msitari huo unakaribia, tunakimbizana kwenye makorido kama tuna wazimu!
KIGEZO#3: SUALA LA MUDA KWENYE NJIA YA FOLENI
“Muda tunaoujali sana huku ‘FOLENI’ ni ule wa kila siku, yaani saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni utatukuta tuko bize kweli kweli. Tunafanya nini? Hilo usituulize, kwa sababu mara nyingine tunafanya hivyo ili tuonekane kwa bosi na kumridhisha ili atuongezee mshahara na kutupandisha cheo. Usitulaumu kwa hilo, kwa sababu hata tukijaribu kuonyesha vipaji vyetu kutatua matatizo ya maana, tutaonekana kimbelembele, halafu wengi wetu tunaogopa sana kurogwa”.Muda wa watu wa njia ya foleni unauzwa ili kupata pesa, na ndiyo maana wanatoa masaa hayo ya kazi kila siku ili kuja kulipwa mwisho wa mwezi. Kwa kifupi wanamkopesha bosi wao siku thelathini, halafu anakuja kuwalipa mwisho wa mwezi. Haya ndiyo maisha yao waliyoyachagua; “Maisha ni kuchagua” wao wamechagua hivyo.
Muda wa maisha (Muda wa wastani wa kuishi binadamu) kwenye njia hii ya foleni hauangaliwi sana, na ndiyo maana watu wa njia hii wana ubavu wa kuuza masaa yao mengi tu ili walipwe pesa. Lakini pia wana kiburi kingine cha kurudi shule miaka mitatu, minne na kuendelea ili kupata cheti kitakachotumika kubadilisha kazi, kupandishwa cheo na kuongezewa mshahara. Kwenye njia hii muda unachezewa kihivyo utafikiri watu wamekubaliana na Mungu juu ya siku zao za kuishi.
KIGEZO #4: UENDESHAJI WA MAISHA YA NJIA YA FOLENI
Maisha ya huku “FOLENI” huyaendeshi wewe bali ni mtu mwingine, muda wa kuanza kazi unapangiwa, muda wa kurudi nyumbani unapangiwa, muda wa kustaafu unapangiwa na kazi za kufanya unapangiwa. Kwa kifupi kauli mbiu ya uendeshaji (control) ya maisha kwenye njia hii ni; “Mikononi mwako nayaweka maisha yangu”Mara nyingi watu wa huku, stress za kazini wanarudi nazo nyumbani. Uchungu wa mambo yote waliyokutana nayo kwenye ‘Jela ndogo’, unaenda kuishia nyumbani kwa mume, mke na watoto. Suala hili ni hatari sana kwa malezi ya watoto na mwenendo wa familia zetu.
KIGEZO #5: SKELI (UKUBWA) WA NJIA YA FOLENI
Njia ya foleni, ina watu wengi sana kwa sasa lakini uwezo wa njia hiyo kuwamudu watu wote hao ni mdogo sana na unazidi kupungua kila iitwapo leo. Walioingia tayari huko ni wengi, kiacha kundi kubwa la vijana wadogo wanaosubiria kwa hamu kuingia kwenye njia hiyo. Wengi wao wametumia gharama kubwa na miaka mingi (zaidi ya 20) kununua vyombo vya usafiri (Vyeti, Taaluma na ujuzi) ili wavitumie vyombo hivyo kuingia kwenye njia hiyo.Kuna haja ya kuanza kuwaanda vijana wetu kwa namna ya tofauti. Wanafanya jambo la busara kuandaa vyombo vya usafiri (Taaluma na Ujuzi), lakini namna wanavyovitumia vyombo hivyo ndiyo haswaa kuna tatizo kubwa.
Vyombo vyao ni vipya na vina “Speedometer” yenye uwezo mkubwa tu, kwa hiyo vinafaa viingie kwenye mwendo kasi. Lakini kwa namna tulivyowajaza maneno tangu wakiwa wadogo, tukiipamba kwa maua ya kila namna njia ya foleni, wengi wa vijana hawa wameyaamini maneno yetu na wanasukumana kuingia kwenye njia ya foleni huku wakiiacha njia ya mwendokasi nyeupe pee!
Huenda tungewaambia tangu mwanzo kuwa njia ya foleni imekwisha jaa, na inazidi kusinyaa kila kukicha, vijana wetu wangejiandaa kisaikolojia. Huenda wengi wao wangejikoki vizuri na kununua vyombo vizuri vyenye uwezo wa kumudu mikiki mikiki na spidi za mwendokasi, na tatizo la njia ya foleni lingepungua sana. Lakini wengi wao hawajui kuhusu hilo, wamemezeshwa walichomezeshwa na wanakitapika kwa vitendo.
Hitimisho
- Mahitaji ya njia ya foleni ni binafsi (personal), unachokifanya ni kujiangalia wewe na nafsi yako, kitu gani kitakuzalishia pesa kubwa na kuunga trela kuelekea huko. Hakuna haja ya kuumiza kichwa kutatua matatizo ya wengine.
- Kuingia kwenye njia ya foleni ni mpaka uwe na kibali maalum kinachoitwa “Cheti”, kibali hiki kikiwa kinang`aa kwa mabanda ya kutosha kitakusaidia kuingia kwenye njia hii. Sema siku hizi kuna ushindani mkubwa sana, kwa hiyo unahitaji kamba za ziada kama marefa au ndugu anayekujua akusaidie kuingia kwenye njia hiyo
- Suala lamuda kwenye njia ya foleni linachukuliwa kama biashara tu, kwenye njia hii, watu wanauza muda ili walipwe pesa na kuongezewa vyeo
- Ukiingia njia ya foleni, uendeshaji wa maisha yako unamwachia mwingine, kazi yako ni kujifunza kutmia kauli ya “Yes Boss!” na kutulia kwenye reli. Ukiingia huku usijifanye mjuaji.
- Njia ya foleni ina watu wengi kiasi kwamba njia hiyo haiwezi kuwamudu watu wote hao. Lakini pia idai ya wadau wa njia hii inazidi kuongezeka kila siku.