Tatizo la uwezo wa kufikiri na utatuzi wa mambo, lawama haiwezi kwenda moja kwa moja kwa CCM bali unaanzia kwa mtu binafsi yeye mwenyewe kujitambua. Unapojitambua wewe ni nani, majukumu yako katika maisha, na nini unatakiwa ufanye uwezesha kukupa utayari wa kuchukua hatua chanya ya mabadiliko.
Watanzania hatutaki kufikiri nje ya boksi. Tunafanya mambo mengi kwa mazoea. Hatuna jipya. Watu ni wavivu kutafuta fursa. wanataka mtelemko. Nakumbuka miaka ya nyuma kidogo wakati nasomea utaalamu fulani niliwapa wazo wanachuo wenzangu. Ambao tulikuwa tunaelekea kumaliza. Nikawambia tuungane tukitoka hapa tuanzishe jambo fulani kwa pamoja. Nikawapa mikakati na namna ya kuanza.
Kilichofuata nilichekwa kwa dharau na wao kusema jambo hilo haliwezekani. Niliamua kuuza wazo langu kwa mtu fulani. Yule mtu alishawahi kuwa mkufunzi wangu. Akalitumia na alifanikiwa saana katika maisha. Baada ya miaka mitano kupita wale walionicheka ndo akili zikawaijia na kusema ooh! Tungejua tungefanya ulicho shauri. Nilicheka tu kwani muda haukuwepo tena na tumeisha sambaratika.
Je, hii ni CCM? Sikatai asilimia mia moja kwamba CCM inachangia lakini ebu sisi wenyewe tubadilike. Mbona wazee wetu walitawaliwa na wakaloni. Nyakati hizo hizo waliamua kupambana nao. Hawakuweka lawama mbele bali mikakati ya ushindi.
Leo sisi hata hivyo vyama vya upinzani ni kama vile wanaiabudu CCM, wanajipendekeza kwa CCM, wanaangalia maslahi yao na si upinzani asilia. Mfano. Unategemea nini hawa wapinzani walimpinga sana Magufuli. Baada ya Magufuli kufariki wakashabikia sana juu ya Rais Samia. Walisahau kuwa Samia nae ni CCM. Watu waliwashangaa!
Wapinzani washindane na mfumo wa CCM si mtu binafsi. Mtu binafsi uondoka, na kuja mwingine kuendeleza ule mfumo. Wakati wa Ukoloni wapigania uhuru hawakushindana na mtu binafsi sijui Gavana au Malkia bali walishindana na kupinga mfumo wa kikoloni. Ndiyo maana walifanikiwa.
South Afrika hawakushindana na mtu au Rais wa wakati huo makaburu wakitawala walishindana na mfumo na kuupinga mfumo wa kibaguzi.
Wapinzani wa Tanzania hawana mikakati ya kuiondoa CCM kwenye mfumo au madaraka. Wanadhani kujenga chuki kwa kiongozi mmoja ambae ndo Rais basi watafanikiwa kuiondoa CCM madarakani. Niseme kwa staili yetu hii ya upinzani ni ngumu kuiondoa CCM madarakani.
Wapo viongozi wengine wa upinzani. Akija mwenye itikadi ya kidini kama wao, uwasikii wakipinga lolote, watakaa kimya na zaidi ni kushabikia tu. Harafu tutegemee CCM kuiondoa madarakani. Tunaviongozi wa upinzani ambao wapo kwa maslahi yao si Taifa. Wengine wanawaza tu urais na si vinginevyo.
Haya yote ni kwakua watu hawafikirii nje ya boksi. Hata vyama vya upinzani vimebaki kudhani mikutano ya hadhara ndo njia pekee ya kuwakomboa watanzania. Toka mfumo wa vyama vingi vianze wao kutwa kucha mbinu yao ya mwisho ni kuona watu wengi wakihudhuria mikutano yao. Wanasahau mtu kuja kwenye mkutano si kwamba anakuunga mkono. Hapana wengine ufika ili kujua nini utaongea wakupime. Lakini si kwamba wako na wewe.
Hii mbinu imepitwa na wakati. Vyama vya upinzani vimekuwa na viongozi kwa muda mrefu. wakati kuna vijana wengi wapo walio na mawazo mapya, hawapewi nafasi. Hivi mtu ukakaa sehemu muda mrefu na huna mbinu nyingine pisha basi waje wengine wavushe chama. Yaani Tanzania watoto wamezaliwa na kukua viongozi wa vyama ni wale wale. Unajiuliza hawa kama hawafuati katiba za vyama vyao je ukiwapa nchi itakuwaje?
Tanzania hatuna vyama vya siasa ambavyo vinawaandaa vijana wao kushika madaraka ya nchi. Tumejenga vijana kuwa machawa, kujipendekeza na kutukana unapoongea kitu tofauti na wanavyotaka.
Mtu anataka kuwa Rais lakini huyo huyo anawatukana polisi au mapolisi kwa kuwadharau badala kutumia mbinu, kuwabadili polisi mawazo na kufanya hao polisi wajione kweli tunatumika na CCM ngoja tubadilike. Lakini kama huoni thamani yao unadhani nao wataona thamani yako? Ha ha ha! hapa tusahau,
Si kwamba polisi wote wanaipenda CCM, na si kweli kwamba Polisi hawawezi badilika na kusimama na vyama vya upinzani. Ila approach ni mbaya.
Nakumbuka uchaguzi wa mwaka 2010 jijini Mwanza. Polisi wakati huo Kamanda Sirro akiwa RPC waliungana na wananchi kuhakikisha alie kuwa waziri wa mambo ya ndani wakati huo anaangushwa. Polisi waliwaacha wananchi wafanye watakalo. Kwani nawao walishachoshwa na huyu waziri amabe nae alikuwa akiwadharau polisi.
Kuiondoa CCM madarakani kunahitajika mbinu mpya na mikakati maalum ambayo si hii tuliyoizoea. Hapo CCm itaondoshwa kiulaini.
Vijana wa Tanzania tubadilike, tuache uchawa na kusifia sifia vitu visivyo na msingi wowote. Bali tujikite kujijenga katika fikra mpya za kuleta ukombozi kwa Taifa letu.