'Tunaipinga Standard Group' - Waandamanaji wanaounga mkono Serikali wajaribu kuvamia HQ ya Media House

'Tunaipinga Standard Group' - Waandamanaji wanaounga mkono Serikali wajaribu kuvamia HQ ya Media House

Ikariiah

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2019
Posts
287
Reaction score
314

Kundi la waandamanaji wanaodai kuunga mkono Serikali ya Rais William Ruto lilifika katika Makao Makuu ya Standard Group pembeni mwa barabara ya Mombasa Rd Jijini Nairobi likilalamikia kile walichokitaja kama utangazaji wa upendeleo dhidi ya utawala wa Ruto.

Waandamanaji hao walifika wakiwa na mabango na matawi ya miti, huku baadhi yao wakijaribu kufika ndani ya jengo la kampuni hiyo. Polisi waliingilia kati na kuwazuia kuingia katika eneo la Standard Group.

Kwa upande wao, waandamanaji waliishutumu Standard Group kwa kutoa taarifa wanazodai ni hasi kuhusu Serikali, wakitaja pia miradi ya Serikali kama mradi wa kiwanda cha mafuta cha Dangote Lamu kama mfano wa kile walichodai kuwa ni taarifa zisizo na uwiano.

Lakini Standard Group imechukulia tukio hilo kwa uzito mkubwa. Kampuni hiyo ilisema waandamanaji waliwatukana na kuwanyanyasa wafanyakazi wake, na ikaeleza tukio hilo kama shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari, demokrasia na biashara halali. Standard pia ilisisitiza kuwa kukosoa uandishi wa habari ni haki, lakini kutishia au kujaribu kuingia kwa nguvu katika ofisi za chombo cha habari ni jambo tofauti.

Tukio hilo pia liliibua makabiliano nje ya jengo baada ya watetezi wa haki za binadamu kufika kuunga mkono Standard na kutetea uhuru wa vyombo vya habari.

Hii si mara ya kwanza kwa Standard Group kukumbana na msuguano kuhusu uandishi wake wa habari. Siku chache zilizopita, Rais Ruto mwenyewe aliikosoa Standard kuhusu kile alichokiita "extortionist propaganda" katika namna inavyoripoti kuhusu Serikali yake. Standard, kwa upande wake, imeendelea kutetea uhuru wake wa uhariri.

Je, raia wana haki ya kupinga au kukosoa namna Standard Group inavyoripoti kuhusu Serikali? Ndiyo! Lakini je, maandamano hayo yanavuka mstari yanapogeuka kuwa jaribio la kuingia katika ofisi za media house na kuwafanya waandishi wajisikie kutishiwa?

Hilo ndilo suala linalofanya tukio hili kuwa muhimu zaidi kuelekea uchaguzi wa 2027. Kwa sababu kama kila kundi la kisiasa litachukulia habari lisiyoipenda kama “propaganda” na kujibu kwa kuizingira newsroom, uhuru wa habari utabaki kuwa na maana gani katika uchaguzi ambao Wakenya wanahitaji taarifa huru ili kufanya maamuzi?

Na swali lingine kwa Standard Group yenyewe: ni kwa kiwango gani media house inapaswa kusikiliza lawama za upendeleo kutoka kwa Serikali na wafuasi wake bila kuruhusu shinikizo la kisiasa kuathiri uhuru wake wa uhariri?
 
Back
Top Bottom