Tunapaswa Kuondoa Pazia la Imani za Kijamii na Kidini Zinazofunika Tatizo la Ndoa za Lazima

Tunapaswa Kuondoa Pazia la Imani za Kijamii na Kidini Zinazofunika Tatizo la Ndoa za Lazima

The Sheriff

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2019
Posts
747
Reaction score
2,112
Ndoa za Lazima Duniani.jpg


Inasikitisha kuwa katika karne hii ya 21 bado kuna jamii duniani ambazo zinahalalisha na kuwalazimisha wanawake wanaobakwa kuolewa na wabakaji wao, au kuwalazimisha mabinti kuolewa na watu wasiowapenda.

Shirika la Kazi Duniani (ILO) linakadiria kuwa watu milioni 40.3 ni watumwa duniani kote. Kati ya hao, milioni 15.4 wako katika hali ya ndoa za kulazimishwa.

Ndoa ya kulazimishwa hutokea wakati mtu, bila kujali umri wake, amelazimishwa kuingia kwenye ndoa bila ridhaa. Ingawa ndoa za kulazimishwa zinaathiri jinsia zote, ILO inaripoti kuwa asilimia 84 ya waathiriwa ni wasichana na wanawake.

Shirika hilo pia linakadiria kuwa 37% ya wale wanaoishi katika ndoa za kulazimishwa walikuwa ni watoto wakati wa ndoa, na asilimia 44% ya watu hao walikuwa chini ya umri wa miaka 15.

Kuna aina kadhaa za ndoa za kulazimishwa: ndoa za kulazimishwa za watu wazima, ndoa za mapema au za utotoni, na usafirishaji haramu unaolenga kuwaingiza wasichana katika ndoa wasizozitaka.

Lakini pia, kuna sababu nyingi zinazopelekea ndoa ya kulazimishwa hutokea. Hizi ni pamoja na kufutiwa (ma)deni, kutatua migogoro, kutekwa nyara - kama ilivyokuwa kwa wasichana wengi waliochukuliwa na Boko Haram – udanganyifu n.k.

Nchini Tanzania, ndoa za kulazimishwa ni jambo ambalo bado linapaswa kuzungumzwa kwa sauti kubwa kwani matukio hayo yamekuwa yakiendelea kuripotiwa licha ya kuwa ni suala linaloleta wasiwasi mkubwa wa kuedelea kukandamizwa kwa uhuru na haki za wanawake.

Ukimya unaozingira suala hili unachangiwa na kutofaulu katika kuwatambua, kuwachunguza, kuwafuatilia na kuwafungulia mashtaka wahalifu. Ndoa za kulazimishwa zinaathiri wanawake na wasichana, na ni aina ya ubaguzi wa kijinsia. Ndoa hizi mara nyingi huhusisha ulanguzi wa wanawake na wasichana - kwa maneno mengine, ni utumwa wa kisasa.

Vitendo hivi vina athari mbaya za kielimu, kiuchumi na kiafya pamoja na kumvua mtoto utoto wake na kudhibiti maisha yake ya baadaye. Wasichana wanapoolewa, mara nyingi huacha shule, na hivyo kuwasababisha fursa finyu za kiuchumi.

Zaidi ya hayo, kutokana na umri wa mabinti wengi kuwa mdogo na hivyo kukosa nguvu ya maamuzi katika mahusiano ya kingono, kunaweza kuwa na matatizo makubwa ya afya yanayotokana na mimba za mapema kabla ya mwili kuwa tayari kwa uzazi.

Hii ni pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao wasichana wengi na wanawake wanavumilia, ikiwa ni pamoja na kazi za kulazimishwa, ubakaji, utumwa wa nyumbani, na unyanyasaji wa kimwili na matusi, na kushindwa kuondoka.

Infographic Ndoa za Lazima (2).png

Kukomesha ndoa za kulazimishwa hakutaashiria tu hatua kubwa katika vita dhidi ya utumwa wa kisasa na biashara haramu ya binadamu, lakini pia kwa usawa wa kijinsia.

Hii inaonekana katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambapo kukomesha biashara haramu ya binadamu na ndoa za utotoni zimejumuishwa katika Lengo la 5 la "kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana wote."

Ili kukomesha ndoa za utotoni na za kulazimishwa, tunapaswa kwanza kuelewa mifumo, kanuni na tabia zinazoendesha fikra hizo, na nini kifanyike kuzikomesha katika mazingira tofauti.

Mabadiliko ya haraka na ya kudumu zaidi yanaweza kupatikana ikiwa wale walioathiriwa na ndoa hizo watasikilizwa, lakini pia kuwepo ushirikiano na sekta na washikadau mbalimbali katika ngazi zote ili kukomesha mila hiyo.

Wanawake – katika utofauti wao wote – lazima wawe kiini cha suluhisho la kukomesha ndoa hizo. Familia na jumuiya lazima zishiriki katika kubadilisha mitazamo hasi ya kijamii ambayo huzuia wanawake kufanya machaguzi yao wenyewe. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kupanua usawa wa kijinsia nyumbani na katika maeneo ya umma.

Ili kufanya mabadiliko kwa kiwango kikubwa, mashirika ya kimataifa, serikali, na viongozi wa kisiasa na wa kidini wanahitaji kujitolea kuweka viwango vya haki za binadamu katika vitendo duniani kote.

Hii inamaanisha kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata elimu bora, huduma ya afya ya uzazi, mifumo ya ulinzi wa kijamii inayozingatia jinsia na soko la ajira la haki na sawa.
 
Back
Top Bottom